Na: Lilian Lundo
Wizara
ya Elimu, Sayansi na Teknolojia inaukumbusha Umma kuwa mitihani ya
Taifa ya Darasa la 4 na Kidato cha 2 itaendelea kuwepo na mwaka huu
itafanyika kama kawaida.
Naibu
Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt. Leonard Akwilapo ameyasema hayo leo,
jijini Dar es Salaam alipokuwa akikanusha taarifa za kutokuwepo kwa
mitihani hiyo kwa mwaka 2016.
“Napenda
niukumbushe Umma kuwa mitihani hii ni muhimu sana katika ufuatiliji wa
maendeleo ya wanafunzi wetu. Kwa hiyo mitihani yote miwili itaendelea
kuwepo na mwaka huu itafanyika kama kawaida. Kama kuna watu wanawaambia
kuwa haitafanyika wawapuuze kabisa,” alifafanua Dkt. Akwilapo.
Dkt.
Akwilapo aliendelea kwa kusema kuwa, mitihani hiyo ina umuhimu mkubwa
katika kupima maendeleo ya mwanafunzi kwa lengo la kufanya maendeleo ya
kitaaluma. Aidha kwa wanafunzi ambao watakuwa hawajafikia viwango vya
ufaulu vilivyowekwa watatakiwa kukariri darasa au kidato.
Amebainisha
kuwa Baraza la Mitihani ndilo lenye jukumu la kushughulikia maandalizi
ya mitihani hiyo ikiwa ni pamoja na utungaji, uchapaji, ufungaji na
usafirishaji hadi ngazi ya Mkoa na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na
Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI) ikiwa na majukumu ya kuhakikisha kuwa
uendeshaji na usahihishaji wa mitihani hiyo unafanyika kikamilifu.
0 comments:
Post a Comment