Na: Lilian Lundo - MAELEZO
SERIKALI
kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imewapangia vyuo
wanafunzi wa programu maalum ya ualimu chuo kikuu cha Dodoma (UDOM)
ambao hawakupata nafasi ya vyuo katika awamu ya kwanza, walioagizwa
kuomba mafunzo kulingana na sifa zao kupitia Baraza la Taifa la Mafunzo
ya Ufundi (NACTE).
Hayo
yamesemwa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt. Leonard Akwilapo
leo, jijini Dar es Salaam alipokuwa akitoa taarifa kuhusu wanafunzi
wanaosoma stashahada maalum ya ualimu wa sayansi chuo kikuu cha Dodoma.
“Mtakumbuka
tuliagiza kwamba wanafunzi ambao walikosa sifa za kujiunga na ualimu wa
sayansi waliombwa kuomba mafunzo yanayolingana na ufaulu wao kupitia
NACTE, Lakini baada ya taarifa hiyo tulipokea maombi mengi kutoka kwa
vijana hawa wakiomba kupangiwa vyuo moja kwa moja na Wizara, wizara
imetafakari na kuamua nao wapangiwe vyuo vya Serikali,” alifafanua Dkt.
Akwilapo.
Aliendelea
kusema kuwa, wanafunzi ambao waliachwa awamu ya kwanza na kupangiwa
katika awamu ya pili ni wanafunzi 290 ambao walikuwa wakisomea programu
ya stashahada ya ualimu wa sekondari na wanafunzi 1,181 ambao walikuwa
wakisomea stashahada ya ualimu wa msingi.
Dkt.
Akwilapo amesema kuwa Wizara imeamua kuwapangia wanafunzi hao vyuo
kutokana na kuonyesha nia ya dhati ya kusomea ualimu ambapo wanafunzi
hao wamepangiwa vyuo vya ualimu vya Marangu na Tabora.
Aidha,
Dkt. Akwilapo ameeleza kuwa wanafunzi hao watajigharamia masomo yao
kulingana na viwango vya ada vilivyowekwa na Serikali. Pia amewataka
kutembelea tovuti ya wizara ya hiyo ambayo ni www.moe.go.tz ili kuona
vyuo walivyopangiwa.
Mnamo
tarehe Mei 28, 2016 Serikali iliwarejesha nyumbani wanafunzi 7,805
waliokuwa wanasoma Stashahada Maalum ya Ualimu wa Sayansi na Hisabati
katika Chuo Kikuu cha Dodoma. Katika mchujo wa awamu ya kwanza wanafunzi
382 ndio waliokuwa na sifa ya kuendelea na masomo chuo kikuu cha UDOM
na wengine 4,586 walipangiwa vyuo vya ualimu vya Serikali.
0 comments:
Post a Comment