WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amewataka Wakurugenzi wa halmashauri na Maofisa
Elimu nchini kutowaondoa katika nyadhifa zao Waratibu wa Elimu Kata na
Wakuu wa shule za sekondari wasiokuwa na shahada, walimu wakuu wa shule
za msingi wasiokuwa na diploma badala yake wawahamasishe kwenda kusoma.
“Maofisa
Elimu na Wakurugenzi msije mkawaondoa wale walimu wakuu kwa zile sifa
nilizosema bado muda ukifika tutatangaza.Msije mkawakurupusha sasa hivi
waacheni waendelee na kazi zao tutatoa muda ili wajipange viziri,” aliema.
Agosti
20 mwaka huu Waziri Mkuu alisema Waratibu wa Elimu katika ngazi ya Kata
na Wakuu wa shule za sekondari wanatakiwa kuwa na shahada huku walimu
wakuu kwenye shule wanatakiwa kuwa na diploma.
Waziri
Mkuu ametoa agizo hilo jana jioni (Jumatano, Agosti 24, 2016) wakati
akizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye
kiwanja cha Mandela katika jimbo la Sumbawanga mjini.
Alisema
Mratibu wa Elimu katika ngazi ya Kata ni lazima awe na shahada ili
aweze kutekeleza majukumu yake ya kusimamia utolewaji wa elimu katika
shule za sekondari na msingi.
“Wakuu
wa shule za sekondari na waratibu wa elimu kata wasiokuwa na shahada
wasiondolewe katika nafasi zao kabla ya kupewa nafasi ya kwenda
kujiendeleza kwa masomo ili waweze kuwa na vigezo vya kuendelea kushika
nyadhifa hizo,” alisema.
Alisema
katika kuboresha maslahi ya walimu Serikali imetenga zaidi ya sh.
bilioni tano kwa mwezi ambazo ni posho ya madaraka. Waratibu Elimu Kata
wanapewa sh 250,000 kwa mwezi huku Wakuu wa shule za sekondari na walimu
wakuu katika shule za msingi wanapewa sh. 200,000.
Waziri
Mkuu alisema badala ya kuwaondoa kwenye nyadhifa hizo ni vema
Wakurugenzi wakawahamasisha walimu hao kwenda kusoma ili na wao
wanufaike na posho ya madaraka iliyoanza kutolewa na Serikali hivi
karibuni.
Katika
hatua nyingine Waziri Mkuu amewataka wazazi na walezi kwenda
kuwaandisha watoto wenye umri wa miaka mitano katika shule za awali
ambapo watapata fursa ya kujengewa msingi mzuri wa masomo kabla ya
kuanza darasa la kwanza.
Pia
aliagiza shule zote za msingi nchini zisizokuwa na madarasa ya awali
kuhakikisha wanaanzisha madarasa hayo haraka na kuanza kutoa elimu hiyo.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
ALHAMIS, AGOSTI 25, 2016.
0 comments:
Post a Comment