Madudu
mengine yameibuliwa katika Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknlojia baada
ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serilali (PAC) kupitia taarifa za
Manunuzi na za kihasibu za wizara hiyo wakati sakata la wanafunzi hewa
likiendelea kufukuta.
Kamati
hiyo imebaini kuwa shilingi bilioni 1.2 zilitumika kwa ajili ya kuandaa
hafla ya harambee ya Wizara hiyo nchini Marekani, tukio ambalo hata
hivyo halikufanyika.
Kwa
mujibu wa maelezo ya wizara hiyo, harambee hiyo ilitarajiwa kukusanya
zaidi ya dola milioni 3 za Marekani ambazo ni sawa na shilingi bilioni 6
za Kitanzania.
Wajumbe
wa PAC walihoji matumizi ya fedha hizo. Hivyo, Gerald Mwaja ambaye
anahusika na mipango alilazimika kutoa majibu ambayo hata hivyo
yalionekana kutowaridhisha wajumbe wa Kamati hiyo.
Alisema
kuwa fedha hizo zilitumika kwa ajili ya mradi huo ambao ulikuwa na
malengo matatu, kati ya malengo hayo lengo moja la kufanya harambee hiyo
lilishindwa lakini malengo mengine mawili yalifanikiwa.
“Mradi
wenyewe ulikuwa na malengo matatu; kuongeza matumizi ya teknolojia ya
Mawasiliano, kuja na mbinu za kufundishia na pia kukusanya fedha kwa
awamu,” alisema.
Alisema malengo mawili yaliyotimia ni kuongeza matumizi ya teknolojia ya mawasiliano pamoja na mbinu ya kufundishia.
Katika
hatua nyingine, PAC imebaini kuwa Wizara hiyo ilitenga kiasi cha
shilingi bilioni 2.1 na kuingia mkataba na Kampuni ya Ujenzi ya Magereza
mwaka 2014 kwa ajili ya kujenga jengo la ghorofa tatu la ofisi za
wizara hiyo Mkoani Dodoma lakini jengo hilo halijajengwa hadi sasa.
Mbunge
wa Vwawa (CCM), Josephat Asunga alisema kuwa wamebaini kuwa sheria ya
manunuzi ya umma haikufuatwa na kwamba mkandarasi alilipwa kiasi
shilingi milioni 780.6 kwa ajili ya ujenzi wa jengo hilo hata kabla ya
mkataba kusainiwa.
Aliongeza
kuwa hakukuwa na maelezo yoyote yanayoonesha kulikuwa na mshindani
katika zabuni hiyo huku fedha nazo zikilipwa kwenye akaunti ya mtu
aliyetajwa kwa jina la Mang’ula badala ya akaunti ya kampuni ya
Magereza.
Pia,
Asunga alieleza kuwa kabla ya ujenzi kuanza mwaka 2015, Wizara hiyo
ilibadili mpango wa kujenga jengo hilo kwa ghorofa tatu na kuwa jengo la
ghorofa nne litakalogharimu shilingi bilioni 4.4.
“Baada
ya Rais Magufuli kuagiza kuwa wote tunahamia Dodoma, wamebadilika
wanasema hawajapata eneo la ujenzi wakati walishasema awali wamepata
eneo,” alisema Asunga.
Aliyekuwa
waziri wa Waziri wa Elimu wakati huo, alieleza kuwa hakufahamishwa
lolote kuhusu ujenzi wa jengo hilo na kwamba hata muhtasari wa mpango
huo hakupewa kwa ajili ya kushauri.
“Mimi
kama Waziri sikujua kinachoendelea katika ujenzi wa jengo, na hata
briefing (muhtasari) ilikosekana ili niweze kushauri,” alisema.
Akijibu
maswali hayo, Afisa Manunuzi wa Wizara hiyo, Audifasy Myonga alikiri
kuwa utaratibu wa manunuzi haukufuatwa na kwamba kulipaswa kuwa na
mshauri mwelekezi ili kutimiza matakwa ya Sheria.
Kaimu
Mwenyekiti wa Kamati ya PAC, Hillary Aeshi aliagiza kupitiwa upya kwa
mchakato wa zabuni ya Jengo la ofisi ya wizara hiyo mjini Dodoma na
kuwasilisha taarifa ya utekelezaji kwenye ofisi ya Katibu wa Bunge kabla
ya Septemba Mosi mwaka huu.
0 comments:
Post a Comment