Thursday 25 August 2016

Mwakyembe Asema Jeshi la Polisi Liko Sahihi Kuzuia Mikutano ya Ndani ya Vyama Vya Siasa,Awataka Watanzania Wasishiriki Maandamano ya UKUTA

...


Waziri wa Mambo ya  Katiba na Sheria Mhe. Dkt Harrison Mwakyembe  amesema amri ya Jeshi la Polisi ya kuzuia mikutano ya nje na ndani ya vyama vya siasa ni halali ambayo kila Mtanzania na mwanachama wa chama chochote cha siasa anapaswa kuitii na kuizingatia na kwamba kutokufanya hivyo ni kuvunja sheria za nchi.

Amesema amri hiyo ni ya kudumu ambayo imelenga kuangalia na kufanya tathmini ya hali ya nchi kutokana na viashiria mbalimbali vya uvunjifu wa amani nchini ambavyo vimeanza kuonekana.

Dkt Mwakyembe alikuwa akijibu swali kutoka kwa Kituo cha Televisheni cha Taifa TBC 1 ambacho kilitaka kupata ufafanuzi  kuhusiana na uhalali wa kauli ya Jeshi la Polisi ya kuzuia mikutano ya ndani na ya hadhara kwa vyama vya siasa nchini.

“Jeshi  la Polisi ni chombo halali cha cha dola kilichoanzishwa kisheria chenye wajibu wa kulinda usalama wa raia na mali zake ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na kuongeza kuwa  uamuzi huo una lengo la kulinda amani ya nchi na endapo kutakuwa na viashiria vya kutishia amani ya nchi yetu lazima hatua za kisheria na kinidhamu zichukuliwe. Ni amri halali na kila Mtanzania na mwanachama wa chama chochote nchini anapaswa kuitii na kuizingatia na kwamba kwenda kinyume ni  kukiuka sheria, ” alisisitiza Mhe. Mwakyembe.

Mhe. Waziri amesema ni haki ya vyama vya siasa kufanya mikutano ila wanatakiwa kutoa taarifa Polisi ili waweze kutoa ulinzi wakati wa mkutano huo na kuongeza kuwa Jeshi la Polisi linaweza kuzuia mikutano hiyo kwa sababu za kiusalama.

Mhe. Waziri pia alisema sio kweli kuwa Mhe. Rais amezuia mikutano ya siasa, bali alichofanya ni kudhibiti uendeshaji wa holela au huria wa shughuli za siasa nje ya maeneo ya uchaguzi ya wanasiasa na kuongeza kuwa Mhe. Rais amefanya hivyo kutokana na kiapo chake cha kuilinda, kuihifadhi  na kuitetea Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Taifa kwa ujumla.

“Mhe. Rais hajapiga marufuku siasa, alichofanya ni kudhibiti uendeshaji holela au huria wa shughuli za siasa nje ya maeneo ya uchaguzi ya wanasiasa husika kuepusha shari na chuki na amefanya hivyo kutokana na kiapo chake cha kuilinda, kuihifadhi na kuitetea Katiba ya Tanzania na taifa kwa ujumla wake. Kwa hatua hiyo Mhe. Rais hajafunga milango ya majadiliano. Milango iko wazi na tulitegemea wenzetu wangekuja na njia mbadala na kulizungumzia hilo badala ya kuitisha maandamano ya nchi nzima," alisema.

Mhe Mhe. Waziri amevitaka vyama vya upinzani nchini kukaa na kuzungumza na Serikali na kuacha kufanya vitendo vya kutishia uvunjifu wa amani kama kuitisha maandamano kwa nchi nzima.
 “Njooni tukae tuzungumze tupime ushauri wenu, hili ni taifa letu sote na milango iko wazi, tuache kuchochea vitendo vya uvunjifu wa amani kama ambavyo inavyoonekana nchini hivi sasa,” alisisitiza.

Amasema Sheria ya Vyama vya siasa hairuhusu kufanyika kwa maandamano kwa nchi nzima, kufanya hivyo ni kuchochea wananchi kuasi “civil disobedience” ni kinyume cha sheria na serikali haiwezi kuivumilia hali hiyo. 
 Mhe. Waziri ametoa wito kwa Watanzania wote kutoshiriki maandamano ya Ukuta ambayo alisema hayatakuwa na tija kwa nchi bali kuleta vurugu katika jamii.
Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger