SERIKALI
imetangaza mwongozo mpya kuwa kuanzia sasa masomo ya sayansi ni lazima
kusomwa na wanafunzi wote wanaosoma elimu ya sekondari kuanzia kidato
cha kwanza hadi cha nne.
Kwa
mujibu wa Sera ya Elimu iliyopo, wanafunzi wanaosoma elimu ya sekondari
wanaweza kuchagua aina ya masomo watakayo wafikapo kidato cha tatu na
kuacha mengine.
Uamuzi
huo ulitangazwa jana mjini Tanga na Waziri wa Elimu, Teknolojia,
Sayansi na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako wakati
akizungumza na mamia ya walimu wa elimu ya msingi kwenye mafunzo ya muda
mfupi kuhusu mtaala mpya wa kufundishia wanafunzi wa darasa la tatu na
nne.
Alisema
hivi sasa nchi imedhamiria kuingia kwenye uchumi wa kati ambao ni wa
viwanda, hivyo suala la sayansi haliwezi kuepukwa kwa sababu ni wakati
sasa wa kuwa na wataalamu wengi wa fani za sayansi watakaoweza
kutosheleza mahitaji ya sekta ya viwanda nchini.
Alisema
kutokana na uhaba wa wataalamu wa sayansi nchini kwenye maeneo mengi,
wizara imeamua kuanzia sasa wanafunzi wote wa elimu ya sekondari kuanzia
kidato cha kwanza hadi cha nne, watalazimika kusoma masomo ya sayansi
na kufanya mtihani wa masomo hayo, na kwamba baada ya matokeo kutoka
ndipo watafanya uamuzi ama wa kuendelea nayo au la.
Hatua
hii kwa mujibu wa Profesa Ndalichako, itamlazimisha mwanafunzi kusoma
kwa bidii ili kuhakikisha anafaulu masomo hayo ingawa hivi sasa
wanafunzi walio wengi wanadai masomo hayo ni magumu, ndiyo maana
wanachagua kusoma masomo ya sanaa.
Alisema
ili kuhakikisha azma ya serikali ya wanafunzi wanapata vitendea kazi
vya masomo hayo, Sh bilioni 12 zimetengwa kwenye bajeti ya fedha ya
mwaka huu kwa ajili ya kununulia vifaa vya maabara kwenye shule zote za
sekondari nchini ili kuwepo na zana za kufundishia kwa ajili ya masomo
ya sayansi.
"Mafunzo
ya vitendo sasa sio mbadala ni lazima, na yatafanywa kama sehemu ya
masomo na wanafunzi wote watalazimika kuyafanya kwa vitendo ili wawe na
uelewa wa walichosoma kwa manufaa ya taifa,” alisema Profesa Ndalichako.
Alisema
Serikali ya Awamu ya tano imedhamiria kuona kiwango cha elimu
kinachotolewa nchini kina hadhi sawa na elimu itolewayo na mataifa
mengine ili kupata wataalamu wenye sifa zinazokidhi mahitaji ya soko
hata kama sio wote wataajiriwa ila hata wale wasiopata ajira wajiajiri
kupitia elimu waliyopata.
Aliwataka
walimu waliohudhuria mafunzo hayo kuhakikisha wanatumia uwezo wao na
elimu waliyopata kufanya kazi kwa mujibu wa maadili ya taaluma ya ualimu
ili kuwajengea msingi mzuri wa elimu wanafunzi wa shule za msingi.
Akizungumzia
kauli ya Profesa Ndalichako, Mwenyekiti wa Wamiliki wa Shule Binafsi
Tanzania (TAMANGOSCO), Mahmoud Mringo alisema ni uamuzi mzuri ila
umekuja kwa kuchelewa kwa sababu mahitaji ya wataalamu wa sayansi nchini
ni makubwa kuliko idadi ya wanafunzi wanaosoma masomo hayo.
Alisema
pamoja na uamuzi huo mzuri uliochukuliwa na serikali, lakini bado
kutakuwa na changamoto ya uhaba wa walimu wa masomo hayo, maabara na
maktaba na kwamba hali hiyo inaweza kusababisha mahitaji ya walimu hao
kutoka nje yakaongezeka.
Katibu
wa Tamangosco, Benjamin Mkonya alisema ni hatua nzuri ingawa
utekelezaji wake utakuwa na changamoto nyingi kwa sababu hali halisi ya
mazingira ilivyo nchini.
Alisema
ikiwa serikali inadhamiria kutekeleza azma hiyo ni vyema kipengele cha
vigezo vya shule kuwepo ambavyo vimeainishwa ndani ya sheria ya elimu
nchini, vikaangaliwa ambavyo ni uwepo wa maabara ya kutosha, maktaba
yenye vifaa na walimu wa kutosha.
Alisema
iwapo vigezo hivyo vikiangaliwa shule ambazo hazijakidhi vigezo hivyo
zikafutwa na vifaa vilivyopo kwenye maabara na maktaba hizo zikaongezwa
kwenye shule zenye vifaa hivyo ili kusaidia utekelezaji wa azma hiyo ya
kufundisha masomo ya sayansi kwa wanafunzi wote kuanzia kidato cha
kwanza hadi cha nne.
Walimu
washiriki wameishukuru serikali kwa mafunzo hayo ambayo walisema ni
mazuri na yameongeza kiwango chao cha uelewa na kuwaongezea mbinu za
ufundishaji sambamba na kukuza morali ya kazi zao.
Pamoja
na kushukuru, wameomba wizara hiyo iangalie jinsi ya kuweka posho kwa
baadhi ya maeneo ya kazi, hususan kwenye vituo vya kazi vilivyopo
pembezoni na kwenye mazingira magumu ili kuwajengea walimu motisha wa
kufundisha maeneo hayo.
Walimu waliohudhuria mafunzo hayo ni 480 wanaotoka halmashauri za Bumbuli, Mji wa Handeni na Halmashauri ya Wilaya ya Handeni.
0 comments:
Post a Comment