Tume ya Haki na Utawala Bora imeandaa kikao cha pamoja kati ya Chadema, CCM, Jeshi la Polisi na taasisi nyingine tatu, wakati joto la Operesheni Ukuta likizidi kupanda kwa viongozi wa Serikali na vyama vya siasa kutoa kauli zinazotofautiana.
Chadema imetangaza kufanya mikutano nchi nzima kuanzia Septemba Mosi katika operesheni iliyobatizwa jina la Umoja wa Kupinga Udikteta Tanzania (Ukuta), ikidai Serikali ya Awamu ya Tano inakandamiza haki na demokrasia nchini.
Kabla
ya kikao hicho, viongozi wa upinzani wamekuwa wakisisitiza umuhimu wa
kuwapo maridhiano katika suala hilo pamoja na Ukawa kususia vikao vya
Bunge vinavyoongozwa na Naibu Spika, Dk Tulia Ackson, lakini kumekuwa
hakuna harakati zozote zaidi ya majibizano.
Hali
hiyo ilizidi baada ya Chadema kutangaza operesheni hiyo ambayo
imesababisha viongozi wa Serikali, hasa wakuu wa mikoa kuanza kutoa
matamko ya kupiga marufuku mikutano yote ya Ukuta kwenye maeneo yao huku
chama hicho kikisisitiza kuwa kitaendesha operesheni yake bila ya
kujali amri ya kuizuia kwa kuwa kina haki kikatiba.
Katika
kile kinachoonekana ni jitihada za kutuliza hali hiyo, Tume ya Haki na
Utawala Bora imeandaa mkutano utakaohusisha taasisi sita, likiwamo
Jeshi la Polisi lililozuia mikutano, CCM inayoendesha Serikali na
Chadema inayopinga maamuzi ya Serikali kwa madai kuwa yanakandamiza
demokrasia na kukiuka misingi ya utawala bora.
Habari tulizozipata
zinaeleza kuwa wanaotakiwa kuhudhuria kikao hicho ni makatibu wakuu wa
vyama hivyo, Abdulrahman Kinana (CCM), Vincent Mashinji (Chadema) na
Ernest Mangu (Mkuu wa Jeshi la Polisi).
Wengine
ni Jaji Francis Mutungi (Msajili wa Vyama vya Siasa), George Masaju
(Mwanasheria Mkuu wa Serikali) na katibu mkuu wa Kituo cha Demokrasia
Tanzania (TCD).
Habari
hizo zinasema kuwa mwenyekiti wa Tume, Bahame Nyanduga, ndiye ambaye
amewaita viongozi hao Jumatano ijayo jijini Dar es Salaam.
Tume
ya Haki na Utawala Bora ina jukumu la kuhamasisha hifadhi ya haki za
binadamu, kuchunguza jambo lolote, kutoa ushauri kwa Serikali na vyombo
vingine vya umma na kuchukua hatua za kukuza, kuendeleza, usuluhishi na
suluhu miongoni mwa watu na taasisi.
Kutokana
na hali ya kisiasa ilivyo sasa, mkutano huo hautaweza kumalizika bila
ya kuzungumzia majibizano yanayoendelea kuhusu operesheni Ukuta na madai
ya ukandamizwaji demokrasia unaodaiwa kufanywa na Serikali.
Alipoulizwa
kuhusu mkutano huo, Nyanduga alimtaka mwandishi kuwahoji kwa kina watu
waliotoa habari hizo kwa sababu yeye hakutoa taarifa yoyote kwa vyombo
vya habari kuhusu ajenda za mkutano huo.
“Sikutoa mwaliko wala taarifa kwenu (wanahabari),” alisema Nyandyga alipoulizwa kuhusu ajenda za mkutano huo.
“Aliyekwambia (suala hilo), akupe taarifa kamili. Nikisema tunajadili nini, haitakuwa na maana ya kuitisha mkutano.”
“Aliyekwambia (suala hilo), akupe taarifa kamili. Nikisema tunajadili nini, haitakuwa na maana ya kuitisha mkutano.”
Mwezi
mmoja uliopita, Rais John Magufuli alitangaza kuzuia mikutano ya
kisiasa wakati akipokea ripoti ya Uchaguzi Mkuu uliopita, akisema
wanasiasa watafanya siasa mwaka 2020 wakati wa uchaguzi mwingine,
akisema wakati huu ni wa kazi na asingependa kuona “mtu yeyote akinizuia
kutekeleza ahadi nilizozitoa kwa wananchi wakati wa uchaguzi”.
Ndani
ya kipindi hicho, Chadema imezuiwa kufanya mkutano wa hadhara Kahama
mkoani Shinyanga, imezuiwa kufanya hafla ya wahitimu wa vyuo vikuu vya
Dodoma na ACT Wazalendo imezuiwa kufanya mkutano wake wa ndani kujadili
bajeti ya 2016/17.
Hatua
hizo zilisababisha Chadema kufungua kesi Mahakama Kuu ikitaka itoe
tafsiri baada ya polisi kuzuia mkutano Kahama na baadaye kuzuia viongozi
wa chama hicho kuingia ofisi za Chadema za wilaya hiyo.
Wiki
iliyopita akiwa njiani kuelekea Kahama, Rais Magufuli alifafanua kauli
yake kupiga marufuku mikutano ya kisiasa, akisema waliozuiwa ni wale
walioshindwa kwenye Uchaguzi Mkuu na kwamba wale walioshinda wafanye
mikutano kwenye maeneo yao na wasialike mwanasiasa kutoka sehemu
nyingine.
Ufafanuzi
huo uliotolewa siku chache baada ya Chadema kutangaza operesheni hiyo
ya Ukuta, umeibuka mjadala mpya, huku Jeshi la Polisi na wakuu wa mikoa
wakitangaza kupiga marufuku mikutano ya Ukuta, huku wakizuia mwaliko wa
wanasiasa kwenye mikutano itakayopata kibali.
Chadema
inasema kuwa ina haki ya kufanya mikutano popote pale kwa kuwa hakuna
sehemu ambayo Sheria ya Vyama vya Siasa inakataza kufanya siasa baada ya
uchaguzi.
Takriban
wiki mbili zilizopita, Mbowe alitangaza mikakati mitatu iliyoazimiwa na
Kamati Kuu ya Chadema, ikilenga kupinga kile ambacho chama hicho
inakiita kuwa ni ukandamizaji wa haki na demokrasia unaofanywa na
Serikali.
Mbowe
alisema moja ya mikakati hiyo ni kufanya maandamano na mikutano nchi
nzima kuanzia Septemba Mosi mwaka huu, kama ishara ya kupinga kauli ya
Rais na polisi kuhusu mikutano na maandamano.
Mbali
na mkakati huo, Chadema imeanzisha operesheni Ukuta, ikitaja matukio 11
inayodai kuwa ya ukandamizaji wa demokrasia nchini na mengine 24 kuwa
yamesababisha kuanzishwa kwa operesheni hiyo.
Mikakati hiyo ya Chadema ilipingwa na viongozi wa CCM na Jaji Mutungi kwa madai kuwa imejaa uchochezi.
Mikakati hiyo ya Chadema ilipingwa na viongozi wa CCM na Jaji Mutungi kwa madai kuwa imejaa uchochezi.
Wakati
CCM ikiwataka Watanzania kutafakari kabla ya kuamua kuungana na
viongozi wa Chadema kudai demokrasia na kugeuka kafara kwa vyombo vya
ulinzi na usalama, Jaji Mutungi alisema kauli za chama hicho cha
upinzani ni kinyume na Sheria ya Vyama vya Siasa.
Wiki
moja iliyopita, Jeshi la Polisi lilitoa kibali kwa Mbunge wa Iringa
Mjini (Chadema), Mchungaji Peter Msigwa kufanya mkutano wa hadhara
jimboni kwake likizuia wanasiasa kutoka maeneo mengine na pia
kuzungumzia chama kingine na kuisema Serikali.
Mkutano
mwingine uliofanyika Ikungi na kuhutubiwa na Mbunge wa Singida
Mashariki, Tundu Lissu, uliisha salama lakini muda mfupi baadaye
mwanasheria huyo wa Chadema alimakatwa na Polisi na kusafirishwa hadi
Dar es Salaam ambako amefunguliwa kesi ya uchochezi.
0 comments:
Post a Comment