MWANAFUNZI
aliyekuwa akisoma Darasa la Saba katika Shule ya Msingi Zimba, Bonde la
Ziwa Rukwa wilayani Sumbawanga, Susana Kauzeni (15) ameuawa baada ya
kupigwa na wazazi wake wakimtuhumu kuwa ni mtoro sugu wa shule.
Ofisa
Elimu wa Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga (Shule za Msingi), Peter
Fusi amesema kuwa mwanafunzi huyo alizikwa kijijini humo Julai 23, mwaka
huu.
“Baba
na mama yake walichangia kumpiga binti yao huyo wakimtuhumu kuwa ni
mtoro sugu wa shule pia nyumbani amekuwa haonekani. Baba yake mzazi
amekimbia baada ya kufanya uhalifu huo huku mama yake akiwa ameshikiliwa
na Jeshi la Polisi,” alieleza Fusi.
Fusi
alieleza kuwa kuanzia Agosti 3 na 4, mwaka huu alitembelea baadhi ya
shule za msingi zilizopo kwenye Bonde la Ziwa Rukwa ikiwemo Shule ya
Msingi Zimba kufuatilia kazi ya utengenezaji wa madawati mapya kwa ajili
ya shule za msingi pia kufuatilia takwimu sahihi za wanafunzi ili
kubaini wanafunzi hewa.
“Nilipofika
kwenye Shule ya msingi Zimba, Mratibu Elimu Kata, Daudi Moga na Mwalimu
Mkuu wa Shule hiyo, Fidelis Mwangurumba walithibitisha kutokea kwa
mauaji hayo ya mwanafunzi huyo,” alisema.
Kwa
mujibu wa Mwalimu Mkuu wa Shule hiyo, Mwangurumba, mwanafunzi huyo
alikuwa ni miongoni mwa wanafunzi watoro sugu shuleni hapo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa, George Kyando amethibitisha kutokea kwa mauaji hayo.
0 comments:
Post a Comment