Wakati Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu akiwa nje kwa dhamana baada ya kupandishwa kizimbani kwa makosa matatu yakiwamo ya uchochezi, Jeshi la polisi mkoani Geita limevamia Hoteli ya KG iliyopo mjini Geita aliyokuwa amefikia Katibu wa Chadema Kanda ya Ziwa, Meshack Miku na Mwenyekiti wa Bavicha Mkoa wa Geita, Neema Chazaile na kuwashikilia kwa tuhuma za uchochezi wa kutumia mitandao ya kijamii.
Taarifa
zilizopatikana kutoka kwa uongozi wa Chadema Mkoa wa Geita na
kuthibitishwa na Kamanda wa Polisi Mkoa, Mponjoli Mwabulambo zimedai
kuwa katibu huyo alikamatwa jana saa 12 asubuhi.
Katibu
wa Chadema Mkoa wa Geita, Sudy Mtanyagala alidai kwamba askari wa
polisi zaidi ya 10 wakiongozwa na Kamanda wa Upelelezi Mkoa (RCO)
waliizunguka hoteli aliyokuwa amelala katibu huyo wakidai wanatafuta
majambazi yenye silaha.
Mtanyagala
alidai kuwa polisi hao waliingia chumba baada ya chumba na walipofika
katika chumba cha mwisho ambacho ndicho alichokuwa amelala katibu huyo
walimkamata na kuchukua simu yake.
Alisema
baada ya kumkamata walisoma nyaraka za chama alizokuwa nazo kisha
kumtaka yeye na mwenyekiti wa Bavicha kuongozana na polisi hadi kituoni
kwa uchunguzi zaidi.
Alisema
katibu huyo wa kanda pamoja na mwenyekiti wa Bavicha mkoa walikuwa
wakijiandaa kwa kwenda katika ziara Wilaya ya Nyang’wale ambako
wangefanya mikutano ya ndani na viongozi wa chama hicho.
Katibu
wa Chadema Wilaya ya Geita, Hellena Thobias alisema walipata taarifa za
kukamatwa kwa viongozi hao asubuhi na kufika polisi.
Alisema
baada ya kufika polisi, maelezo yalibadilika na kuelezwa katibu wao
anatuhumiwa kwa uchochezi kwa kutumia mitandao ya kijamii.
Alisema
wamejitahidi kuomba dhamana lakini imeshindikana baada ya kuelezwa kuwa
watuhumiwa hao watakuwa chini ya uangalizi wa polisi kwa uchunguzi
zaidi.
“Polisi
wametunyima dhamana hadi saa 10 jioni tuko polisi tumeomba dhamana
wamekataa sijui ni sheria gani inayomzuia mtu kupata dhamana lakini pia
sijui ni sheria gani ya polisi kumnyang’anya mtu simu yake bila ridhaa
na kuichunguza. Hatutanyamaza juu ya uonevu huu,” alisema.
Alisema
Serikali imekataza mikutano ya hadhara na kueleza kusikitishwa kwake
na hatua ya jeshi la polisi kufuatilia hadi mikutano ya ndani ya chama
hicho ambayo ni haki yao kikatiba.
Akizungumza
kwa simu na mwandishi, Kamanda Mwabulambo alikiri jeshi lake
kuwashikilia katibu huyo wa Chadema wa kanda na mwenyekiti wa Bavicha
mkoa lakini akasema yupo nje ya ofisi hivyo hawezi kulizungumzia jambo
hilo kwa undani.
0 comments:
Post a Comment