Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amesema
serikali yake haitagawa chakula cha bure kwa wananchi wanaopatwa na
tatizo la njaa pasipo kuwa na sababu za msingi na badala yake amewataka
watanzania wajikite kufanya kazi kwa juhudi na maarifa ikiwa ni pamoja
na kuzalisha chakula cha kutosha.
Rais
Magufuli amesema hayo jana tarehe 31 Julai, 2016 wakati akihutubia
mikutano ya hadhara na kuzungumza na wananchi waliosimamisha msafara
wake akiwa njiani kutoka Mkoani Tabora kuelekea Shinyanga na baadaye
Geita anakoendelea na ziara yake.
Pamoja
na kuwahimiza wananchi kuzalisha chakula cha kutosha ili kuondokana na
njaa Rais Magufuli alisema serikali yake itajikita kuhakikisha
inashughulikia tatizo la uhaba wa maji, ujenzi wa miundombinu hususani
barabara na reli, kuimarisha huduma za matibabu, elimu na kutengeneza
ajira.
Akiwa
Isaka Mkoani Shinyanga Rais Magufuli alisema serikali haitalipa fidia
kwa wananchi waliopatwa na maafa ya mafuriko yaliyobomoa nyumba zao
mwezi Machi mwaka 2015 na badala yake itajielekeza kutatua tatizo kubwa
la uhaba wa maji katika mji huo ambao una makutano ya reli ya kati ya
kutoka Dar es Salaam kwenda nchi za Burundi na Rwanda.
Katika
Mji wa Kagongwa Rais Magufuli alipokea kilio cha wananchi dhidi ya
vitendo vya ujambazi na ametoa siku tano kwa Kamanda wa Polisi wa Mkoa
wa Shinyanga kuhakikisha watu wanaojihusisha na ujambazi wanakamatwa na
kufikishwa katika vyombo vya sheria.
Mjini
Kahama, Dkt. Magufuli aliiagiza Wizara ya Nishati na Madini
kushirikiana na Mbunge wa Kahama Mhe. Jumanne Kishimba kukokotoa
mahesabu vizuri na kubaini kodi ambayo Serikali inastahili kulipwa baada
ya Mbunge huyo kudai kuna kiasi kikubwa cha kodi hakijakusanywa kama
ambavyo sheria inaelekeza.
Aidha,
Rais Magufuli alisema serikali itahakikisha wawekezaji wanaochimba
madini wanaacha kusafirisha mchanga wenye madini kwa lengo la kwenda
kuchakata nje ya nchi na badala yake ametaka uchakataji huo ufanyike
hapa hapa nchini.
Dkt.
Magufuli alizungumza na wananchi vijiji vya Segese na Bukoli na
kuwahakikishia kuwa Barabara ya Kahama, Segese, Kakola hadi Geita yenye
urefu wa kilometa 146 itajengwa kwa kiwango cha lami kama alivyoahidi.
Mjini
Geita, Rais Magufuli alipokea kilio cha wananchi wanaodai kuwekewa zuio
la kutumia mawe yenye mabaki ya madini ya dhahabu (Magwangala) kwa
lengo la kusaga na kuchenjua ili kupata dhahabu, na ametoa wiki tatu kwa
Wizara ya Nishati na Madini kwa kushirikiana na Baraza la Taifa la
Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kufanya tathimini na kuwaruhusu
wachimbaji wadogo kutumia Magwangala.
Rais
Magufuli pia ameiagiza Bodi ya Pamba hapa nchini kuhamisha ofisi zake
zilizopo Jijini Dar es salaam na kuzileta katika Mikoa ya kanda ya ziwa
ambako uzalishaji wa zao la pamba unafanyika.
Dkt.
Magufuli amewaonya viongozi na watendaji wa bodi hiyo dhidi ya vitendo
vya usambazaji wa mbegu za pamba zisizoota na amesema ikitokea tena
watachukuliwa hatua.
Tarehe
01 Agosti, 2016 Rais Magufuli ambaye ameongozana na Mkewe Mama Janeth
Magufuli anatarajia kukamilisha ziara yake ya siku nne katika Mikoa ya
Singida, Tabora, Shinyanga na Geita.
Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Geita
31 Julai, 2016
0 comments:
Post a Comment