Maziko ya Rais wa
Pili wa Zanzibar, Aboud Jumbe Mwinyi (96) aliyefariki dunia juzi jijini
Dar es Salaam yalifanyika jana nyumbani kwake Migombani, Zanzibar huku
vijana wakikataa gari la Jeshi kubeba jeneza lenye mwili wake.
Mwili wa hayati Jumbe uliswaliwa katika Msikiti wa Mushawwar, Mwembeshauri mjini Zanzibar na wakati wanatoka msikitini vijana walimuomba mtoto wa marehemu Mustafa Jumbe kwamba jeneza lisiingizwe kwenye gari badala yake wao watalibeba hadi nyumbani, umbali wa wastani wa kilomita tatu.
Hata
hivyo, walipofika eneo la Kilimani walikuta gari la Jeshi aina ya Land
Rover likiwa limeegeshwa kwa ajili ya kubeba jeneza lakini vijana
walikataa kulipandisha badala yake waliendelea kubeba kwa kupokezana
hadi nyumbani kwa marehemu Migombani ambako alizikwa.
Haikuweza
kufahamika mara moja kwanini vijana hao walikataa gari la Jeshi kubeba
jeneza lakini huenda ilikuwa kutekeleza wosia alioutoa Mzee Jumbe wakati
wa uhai wake kwamba akifariki dunia jeneza lake lisifunikwe bendera
yoyote kama ishara ya maziko ya kiserikali.
“Sitaki katika maziko yangu
kutumbuizwa chochote kiendacho hata kidogo kinyume na mafundisho ya
Uislamu,” aliandika katika wasia.
“Sitaki beni (bendi), sitaki mizinga, sitaki maombolezo wala lolote jingine lenye hata chembe ya kufuru.
Sitaki hivyo nikiwa hai, nitakapoondoka katika dunia. Mwenyezi Mungu
anatosha kuwa shahidi wangu, duniani na akhera.”
Aidha, wakati wa kuweka
mwili kaburini yalitajwa majina ya watoto wanne wa marehemu; Ismail,
Amari, Rashid na Mustafa pamoja na Sheikh Zubeir ambao ndiyo marehemu
aliwaandika kwenye wasia wake kwamba watakuwa na haki ya kuuhifadhi
mwili wake kaburini.
Kabla ya kuupeleka mwili wa marehemu Jumbe katika
makaburi ya nyumbani kwake Migombani kwa ajili ya mazishi, Mufti Mkuu
pamoja na Kadhi Mkuu wa Zanzibar, Sheikh Saleh Omar Kabi na Sheikh
Khamis Haji Khamis waliongoza dua na swala maalumu iliyofanyika saa 6:45
mchana katika Msikiti wa Mushawwar.
Viongozi mbalimbali wa Serikali,
wastaafu, vyama vya siasa na mabalozi walikuwapo kwenye mazishi hayo.
Miongoni mwao ni Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein, Waziri Mkuu
Kassim Majaliwa, Jaji Mkuu Othman Mohamed Chande, Spika wa Baraza la
Wawakilishi Zubeir Ali Maulid, marais wastaafu wa Jamhuri, Benjamin
Mkapa na Ali Hassan Mwinyi, makamu wa Rais mstaafu Dk Mohamed Ghalib
Bilali, Rais mstaafu wa Zanzibar Amani Abeid Karume, waziri mkuu mstaafu
Edward Lowassa na aliyekuwa Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar, Maalim
Seif Sharif Hamad.
Jumbe, aliyechaguliwa kuongoza Zanzibar kuchukua
nafasi ya Rais wa kwanza, Abeid Amani Karume aliyeuawa mwaka 1972,
aliongoza kwa miaka 12 hadi mwaka 1984 alipovuliwa nyadhifa zote
serikalini na ndani ya chama tawala, CCM kutokana na kutofautiana kuhusu
muundo wa Muungano.
Tangu alipovuliwa nyadhifa zake amekuwa akiishi
nyumbani kwake Mjimwema, Kigamboni na hakuwa anaonekana kwenye shughuli
za kiserikali tofauti na viongozi wengine wastaafu. Mara nyingi wakati
akiwa bado ana nguvu alijishughulisha na masuala ya kumcha Mungu.
Walivyomkumbuka
Katika mazishi hayo, viongozi mbalimbali wa serikali,
wanasiasa na wananchi waliohudhuria walimuelezea kuwa alikuwa jasiri,
mnyenyekevu na aliyeishi maisha ya kumcha Mungu.
“Aliishi maisha ya ucha
Mungu, ucha Mungu hauna siasa, hauna chama na hata baada ya kustaafu
alichagua kukaa kimya, alishauri kuhusu maendeleo ya nchi bila kuita
waandishi wa habari. Ni jambo tunalopaswa kujifunza viongozi
tunapostaafu,” alisema Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano,
January Makamba.
Makamba alisema Jumbe ni kiongozi aliyeweka historia ya
Zanzibar kwa kuanzisha Katiba ya Zanzibar na Baraza la Wawakilishi na
kwamba kuna haja ya kuenzi mchango wake.
Lowassa alimzungumzia Jumbe
kama mtu jasiri aliyesimamia kile alichokiamini na kwamba alikuwa
mwaminifu na mwenye kufuata utaratibu.
Maalim Seif ambaye pia ni Katibu Mkuu wa CUF, alimzungumzia Jumbe kama mtu mwenye msimamo, hasa
alipotaka Muungano wa Serikali tatu msimamo aliosema hata yeye anauunga
mkono.
Pia, alisisitiza kwamba Jumbe alikusudia kulinda kikamilifu
heshima ya watu wa Unguja na Pemba.
“Nadhani wananchi watakumbuka Jumbe
alivyoweza kusimama na kujenga hoja juu ya haja ya kuwa na muundo wa
Muungano usiokinzana, yaani wa Shirikisho au kama alivyotaja mwenyewe
‘The partnership’ katika azma ya kuheshimu nchi mbili huru zilizoungana,
Tanganyika na Zanzibar”, alisema Maalim Seif.
Aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu
wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), Dk Ramadhani Dau alisema,
“Marehemu namtamka kwa neno moja tu: Unyenyekevu.”
Dk Dau alisema
maisha ya marehemu Jumbe yalikuwa ya ucha Mungu, alipenda watu na
hakuwa mtu wa kujitutumua kutokana na wadhifa wa urais aliokuwa nao.
Alisema Jumbe aliishi maisha ya kawaida toka nyumba yake ya Mjimwema,
Dar es Salaam na Unguja kwenye nyumba yake ya Migombani.
“Angekuwa
kiongozi mwingine hapa ungeona mbwembwe nyingi, lakini huyu mambo
yamekwenda kawaida, alijitolea kwenye misikiti na shughuli zote za
kidini,” alisema Dk Dau.
Watoto wa marehemu Jumbe, Suleiman na Ismail
walisema kuwa bila shaka baba yao alithamini hatma ya maisha yake ya
baadaye, duniani na akhera na hapakuwa na budi wao pamoja na Serikali
zote mbili kuheshimu kile alichokiamini yeye kama wasia.
Maombolezo siku
saba
Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imetangaza siku saba za
maombelezo zitakazohusisha kupandishwa bendera nusu mlingoti, lakini
shughuli zingine zitaendelea kama kawaida.
Familia ya Mzee Jumbe ilitangaza kuwa viongozi mbalimbali wa dini na Serikali watajumuika pamoja
kesho katika Msikiti wa Mushawwar kwa ajili ya dua ya ziada na khitma ya
marehemu.
0 comments:
Post a Comment