Tundu Lissu, ambaye ni wakili wa Mbunge wa Bunda Mjini, Ester Bulaya
jana alitumia muda wa saa mbili kupangua maombi ya wananchi wanne
wanaopinga matokeo ya Uchaguzi Mkuu yaliyompa ushindi mteja wake.
Kesi hiyo imeanza kusikilizwa tena baada ya Mahakama ya Rufaa kufuta
uamuzi wa Mahakama Kuu uliotupilia mbali hoja za kupinga matokeo hayo,
ambazo ziliwasilishwa na wafuasi wanne wa aliyekuwa mgombea wa jimbo
hilo, Steven Wasira (CCM).
Jaji Mohamed Gwae wa Mahakama Kuu, alitupilia mbali kesi hiyo baada ya
kukubali pingamizi la Lissu kuwa wafuasi hao hawakuwa na haki ya
kisheria kufungua kesi hiyo.
Wakazi hao wa Bunda wanadai kuwa uchaguzi haukuwa huru na haki kutokana
na kugubikwa na vitendo vya rushwa, mgombea wanayemuunga mkono kunyimwa
fursa ya kuhakiki matokeo na pia kuongezeka kwa idadi ya vituo vya
kupigia kura.
Jana, Lissu, ambaye ni Mwanasheria Mkuu wa Chadema na wakili wa
kujitegemea, alitoa majibu ya utetezi mbele ya Jaji Lameck Mlacha
kuanzia saa 4.10 asubuhi na kukamilisha saa 6.02 mchana wakati shauri
hilo lilipoahirishwa kwa muda hadi saa 8:00 mchana kutoa fursa kwa
mawakili wa upande wa wadai, Constantine Mutalemwa kujibu.
Lissu alidai kuwa waleta maombi wameshindwa kutoa hoja mahususi
kuonyesha ukiukwaji wa sheria, kanuni na taratibu za uchaguzi wanazodai
ulikuwepo katika mchakato wa Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, mwaka jana.
Wakili Lissu pia alidai kuwa walalamikaji ambao ni Magambo Masato,
Matwiga Matwiga, Janes Ezekiel na Ascetic Malegele, pia wameshindwa
kuonyesha madhara waliyopata kama wapigakura kuishawishi mahakama
kutengua matokeo yaliyompa ushindi Bulaya dhidi ya mwanasiasa huyo
mkongwe.
“Waleta maombi wanadai uchaguzi haukuwa huru na haki, idadi ya
wapigakura kutofautiana kwa kila kituo na uwepo wa vitendo vya rushwa,
lakini hawabainishi wazi nani mhusika wa mambo wanayoyalalamikia na
madhara waliyopata kwa nafasi yao ya wapigakura,” alisema wakili Lissu.
Alisema vitendo vya rushwa katika uchaguzi ni kosa kubwa linaloweza
kusababisha kubatilishwa kwa matokeo ya uchaguzi mzima, lakini
walalamikaji wana wajibu wa kumtaja mhusika wa vitendo hivyo ili kuipa
mahakama fursa ya kutafsiri vyema sheria na kutoa haki.
“Lakini madai ya juujuu tena ya jumla kuwa aliyetoa rushwa ni wakala wa
mteja wangu, hayakubaliki mbele ya macho ya sheria kwa sababu mtu huyo
hajulikani na jukumu la kuthibitisha madai ni la mleta maombi na
uthibitisho huo haumo kwenye hati yao ya maombi,” alidai Lissu.
Aliomba maombi hayo yafutwe kwa hoja kwamba wadai hawajataja vifungu
vinavyoipa mahakama haki na mamlaka ya kuyasikiliza na kuyaamua.
0 comments:
Post a Comment