Sunday 30 December 2018

SERIKALI KUSAJILI WAKULIMA WOTE NCHINI

...
Waziri wa Kilimo, Mhe. Japhet Hasunga (Mb) amewaagiza Wakurugenzi wa Bodi za Mazao kuanza mara moja zoezi la kuwatambua na kuwasajili wakulima wa mazao yote nchini lengo likiwa kuwatambua ili kupanga mipango sahihi yenye kuongeza tija na uzalishaji katika mazao yote.


Mhe Hasunga amesema hayo Jumamosi 29 Disemba 2018 wakati akizungumza na Wenyeviti wa Bodi za Mazao pamoja na Wakurugenzi wa Bodi hizo za Mazao Jijini Dodoma ambapo amesisitiza kuwa ili kuongeza tija na uzalishaji katika Sekta ya kilimo na kuandaa mipango madhubuti ya kuendeleza mazao yote ni vyema kuwatambua Wakulima wote nchini.

Agizo hilo limekuja baada ya takribani wiki tatu kupita tangu Waziri Hasunga alipotoa agizo kwa Bodi ya Korosho kuandaa daftali maalumu la kuwatambua wakulima wa korosho nchi nzima, ambapo moja ya taarifa ambazo zitajumuishwa katika daftali hilo ni pamoja na jina kamili la Mkulima, Mkoa, Wilaya, Kata na Tarafa anayotoka.

Mambo mengine yanayojumuishwa ni pamoja na Kitongoji, Mtaa au Jina la Kijijini anapotoka, mahali lilipo shamba pamoja na ukubwa wa shamba lake.

“Tumepata changamoto kadhaa wakati wa kuwahakiki wakulima wa korosho katika mikoa ya Mtwara, Lindi, Pwani na Ruvuma na kama Bodi ya Korosho ingekuwa makini kuandaa daftari la Wakulima zoezi la uhakiki lingekuwa rahisi, kwa ajili hiyo niliwaagiza Bodi ya Korosho kukamilisha zoezi hili mpaka Mwezi Machi, 2019 na Bodi za Mazao zilizobaki ukiacha Bodi ya Tumbaku ambao wao tayari walishafanya hivyo, kukamilisha Mwezi June, 2019,” amesema Mhe Hasunga.

Waziri Hasunga ameongeza kuwa mipango sahihi ya kuwaendeleza Wakulima kuanzia kwenye kilimo chenyewe hadi kufikia katika hatua ya kuvuna, kuhifadhi na kulifikia soko ni vyema kuwa na mfumo maalumu wa kanzi data (Database) ya kuwafahamu ili kushughulikia mahitaji yao kisasa na kwa haraka zaidi.

Bodi za Mazao zilizoshiriki mkutano huo ni pamoja na Bodi ya Korosho, Bodi ya Pamba, Bodi ya Mkonge, Bodi ya Pareto, Bodi ya Chai, Bodi ya Kahawa, Bodi ya Tumbaku, Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko na Bodi ya Sukari.

Wakala zilizoshiriki ni pamoja na Wakala wa Taifa wa Mbolea (ASA) Wakala wa Wakulima Wadogo wa Chai (TSHTDA).

Taasisi nyingine za Wizara ya Kilimo zilizoshiriki ni pamoja na Taasisi ya Udhibiti wa Mbegu (TOSCI), Shirika la Ukaguzi na Usimamizi wa Vyama vya Ushirika (COASCO), Taasisi ya Utafiti wa Viuatilifu vya Ukanda wa Kitropiki (TPRI), Mfuko wa Pembejeo za Kilimo (AGITF), Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA), Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea (TFRA), Taasisi ya Utafiti wa Kilimo (TARI), Tume ya Maendeleo ya Ushirika, Tume ya Taifa ya Umwagiliaji, Kampuni ya Taifa ya Mbolea (TFC) na Bodi ya Leseni za Maghala.

Chanzo:Eatv
Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger