Monday 31 December 2018

BWANA HARUSI AFARIKI GHAFLA KANISANI AKISUBIRI KUFUNGA NDOA

...
Sherehe ya harusi iliyokuwa ifanyike juzi jioni katika Kanisa la Nabii wa Utukufu wa Bwana lilipo Olmatejoo, Kata ya Sakina jijini Arusha na kwenye ukumbi wa Sariko Olasiti Garden, iligeuka msiba baada ya bwana harusi kufariki dunia ghafla akiwa kanisani.

Tukio hilo lilitokea majira ya saa 11 jioni katika kanisa hilo ambapo bwana harusi huyo, Heaven Makupa (47) alikuwa kanisani tangu saa saba mchana akisubiri kufunga ndoa na Jane Kimaro.

Hata hivyo, wakati sherehe, nderemo na vifijo vikiendelea vikiongozwa na kikundi cha matarumbeta nje ya kanisa huku bibi harusi akiingia kanisani, Heaven alianza kujisikia vibaya na kupoteza fahamu.

Kutokana na hali hiyo alikimbizwa Hospitali ya St Elizabeth, lakini alifikishwa akiwa tayari amefariki na mwili wake kupelekwa chumba cha kuhifadhia maiti cha hospitali ya Mkoa wa Arusha ya Mount Meru.

Ndoa hiyo ilikuwa ifungwe na kiongozi wa kanisa hilo, Nabii Peter Alayce na tayari taratibu zote zilikuwa zimekamilika tangu mchana alipofika bwana harusi na ujumbe wake.

Wakati kifo hicho kinatokea mamia ya watu walikuwa tayari wamefika katika ukumbi wa Sariko Olasiti Garden kuwasubiri maharusi hao ili kuendelea na sherehe.

Mmoja wa wageni waalikwa, Juliana Mosha alisema kabla ya kifo hicho hakukuwa na taarifa yoyote ya kuugua kwa bwana harusi na walishikiri naye vikao vya harusi hadi dakika ya mwisho. “Hili ni jambo la miujiza, hatujui kilichotokea nadhani hii ni kazi ya Mungu,” alisema Juliana.

Alisema baada ya taarifa kufikishwa ukumbini juu ya msiba huo, watu walianza kutawanyika na kurejea majumbani.






Na Mussa Juma,Mwananchi
Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger