Saturday 29 December 2018

VIGOGO WA CHADEMA WAKAMATWA NA POLISI..YUMO KATIBU MKUU MASHINJI

...
 Jeshi la Polisi wilayani Hai, mkoani Kilimanjaro, linawashikilia Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Vincent Mashinji na viongozi wengine watatu wa chama hicho mkoani humo kwa tuhuma za kufanya mkusanyiko usio halali.

Akizungumza na Mwananchi leo Jumamosi Desemba 29, 2018 mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na wsalama wilaya ya Hai ambaye ni mkuu wa wilaya hiyo, Lengai Ole Sabaya amesema viongozi hao wamekamatwa mchana.

"Ni kweli tumemkamata Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Mashinji, katibu wa Chadema mkoa wa Kilimanjaro, Basir Lema, mwenyekiti wa halmashauri ya Hai, Egra Mchomvu na msaidizi wa mbunge wa Hai, Freeman Mbowe, Irine Lema kwa kufanya mkusanyiko usio halali," amesema.

Sabaya amesema viongozi hao, leo mchana wamekutwa wakifanya mkusanyiko katika eneo la Boma bila ya kuwa na kibali jambo ambalo ni kinyume cha sheria.

"Naomba nitoe wito kwa wanasiasa kuheshimu sheria na taratibu, kama mnataka mkutano kuna taratibu hamuwezi kuvamia na kufanya mikutano kiholela," amesema.

Sabaya amesema katika wilaya yake ya Hai kwa sasa hataruhusu mikutano isiyo halali ambayo inalenga kuwapotosha wananchi kuhusu kazi nzuri ambazo zinafanywa na Rais john Magufuli.

"Waiache serikali ifanye kazi zake, kama wanataka siasa zao wasubiri kwenye kampeni, Hai tunataka maendeleo," amesema.

Baadhi ya wanachama wa Chadema wilaya ya Hai walikiri kukamatwa kwa viongozi hao majira ya mchana hata hivyo hawakuwa tayari kufafanua chanzo cha kukamatwa kwao.

"Mimi nimewaona wakipelekwa polisi sijui kilichowakuta," amesema Lilian Shirima ambaye ni mfanyabiashara mjini Boma.

Na Mussa Juma,Mwananchi 
Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger