Friday 28 December 2018

WAZIRI MKUU AWAAGIZA MAWAZIRI KUFIKA KWENYE MAENEO YA UJENZI

...
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amekutana na Mawaziri na Makatibu Wakuu kwenye eneo la tenki la maji la kutolea huduma katika ujenzi wa mji wa Serikali Mtumba badala ya ukumbi wa Hazina kama alivyokuwa amepanga awali.

Akiwa Ihumwa, Waziri Mkuu amewaagiza Mawaziri wafike kwenye maeneo ya ujenzi wa ofisi zao, watathmini uwezo wa wakandarasi wanaojenga majengo ya wizara na pale watakapojiridhisha kuwa uwezo wao ni mdogo, wawabadilishe mara moja.

Ametoa agizo hilo leo mchana (Ijumaa, Desemba 28, 2018) akiwa kwenye kikao cha kazi (site meeting) na mawaziri 15 na manaibu mawaziri katika eneo la Ihumwa lililoko km. 17 kutoka jijini Dodoma.

“Mawaziri mliopo na makatibu wakuu wote kaeni na wakandarasi wenu hapa site ili waeleze kazi hii itakamilishwa lini. Lengo letu ni kuhakikisha kuwa kazi hii inakamilishwa kwa wakati,” amesisitiza.

Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuwapa mrejesho Mawaziri juu ya changamoto alizokutana nazo jana alipofanya ukaguzi wa ujenzi kwa kila wizara. “Nataka Mawaziri ambao ofisi zao zinajengwa wa watu wa Mzinga, wakae nao na kutathmini uwezo wao na kama mtaona hawawezi, mkabidhi kwa mkandarasi mwingine,” amesema Waziri Mkuu.

Amewataka wakandarasi wahakikishe wanaongeza idadi ya vibarua ili kazi hiyo iweze kwenda haraka. “Wizara iliyofanya vizuri kuliko zote ni ya Utumishi, wao wako hatua nzuri. Kwa maana ya uchapaji kazi, eneo nililokuta lina wafanyakazi wengi ni magereza,” amesema.

Wakati huohuo, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Bw. William Lukuvi alimweleza Waziri Mkuu kwamba kuna wagongaji wa kokoto ambao wamepokea fedha lakini wakaamua kufunga machimbo yao kwa sababu ya sikukuu.

“Waziri wa Madini aongee nao hawa watu ili warejee na kufanya kazi kwa sababu baadhi yao wameshapokea fedha na mahitaji ya kokoto hapa ni makubwa na aliyebakia akifanya kazi ni Nyanza Road Works peke yake,” alisema.

Naye Waziri wa Nishati, Dk. Medard Kalemani alimweleza Waziri Mkuu kwamba wizara yake imetoa transforma tisa za kusaidia kupoza umeme lakini ni wizara nne ambazo zimejitokeza na kulipia line za transforma hizo.

“Wizara yetu tumetoa transforma tisa za kusaidia umeme upatikane eneo la ujenzi. Niwaombe mawaziri waliopo, walipie service line tu ambazo gharama yake ni sh. 921,000 ili wafungiwe transforma na kazi iweze kufanyika mchana na usiku. Hadi sasa, tumeshapokea maombi kutoka wizara nne tu za Maji, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera), Elimu na Nishati ili kazi imalizike ndani ya muda mfupi,” alisema.

(mwisho)

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU
Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger