Hatimaye leo wabunge wote wa vyama
vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) wanakutana na viongozi
wao wa jijini hapa kumchagua mgombea urais atakayeviwakilisha vyama
hivyo katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25.
Mkutano huo wa wabunge umekuja baada ya
vikao kufanyika mfululizo wiki hii, huku kukiwa na mvutano kuhusu nani
au chama gani kisimamishe mgombea urais.
Jana gazeti hili liliripoti kwa uhakika
habari zilizotoka ndani ya vikao hivyo na kuthibitishwa na Mwenyekiti
mwenza wa Ukawa, Dk Emmanuel Makaidi, kuwa vyama hivyo vitaweka wazi
mgombea wake wa urais leo.
“Tumeshakubaliana namna ya kugawana kata
na majimbo 13 yaliyobaki na Jumamosi tutaweka wazi kwa wananchi. Pamoja
na hilo pia tutamtangaza mgombea urais na chama anachotoka,” alisema Dk
Makaidi.
Umoja huo umekuwa ukiongezeka nguvu
tangu wakati wa mchakato wa Katiba mwaka jana, hali inayosababisha
wafuasi wake kuamini kuwa yeyote atakayesimamishwa na umoja huo na
kupigiwa kampeni kwa pamoja anaweza kujikuta anakuwa rais, mbunge au
diwani.
Mvutano
Vikao vya umoja huo vilitawaliwa na
mvutano baina ya wajumbe ndani ya umoja huo hasa katika nafasi ya
mgombea urais baada ya kuwapo kwa watia nia zaidi ya mmoja.
Chanzo cha uhakika kutoka ndani ya umoja
huo kilisema kuwa isingekuwa rahisi vikao vya namna hiyo vikakosa
mvutano huo, kutokana na baadhi ya wajumbe kushindwa kukubaliana na
vigezo vilivyowekwa tangu mikutano ya awali.
Iliilazimu Kamati Kuu ya Ukawa kufanya
kazi ya ziada kuhakikisha kuwa maridhiano yanafikiwa ili kumpata
mgombea, ndipo ikaamuliwa waalikwe wabunge wote wapige kura kupata
mgombea.
Taarifa zaidi zilisema kuwa wajumbe
walio wengi walikuwa wanaipa nguvu Chadema kutoa mgombea urais kutokana
na nguvu yake hasa katika mikoa ya Bara, na ukweli kwamba tayari CUF
imekwishapewa fursa hiyo Zanzibar.
Jana gazeti hili likinukuu vyanzo vya
ndani ya kikao hicho, liliripoti kuwa licha ya kutangaza kugawana kata
na majimbo yaliyobaki, jina la mgombea urais lingetangazwa leo endapo
wajumbe wa Kamati Kuu ya Ukawa iliyokutana jana wangeafikiana.
Akihojiwa na kituo cha televisheni cha
Azam jana, Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa alisema leo
vyama hivyo vitalitangazia dunia chama kipi kitatoa mgombea wa Ukawa.
Siku chache baada ya baadhi ya wabunge
kupewa adhabu ya kutohudhuria vikao vya Bunge na Spika Anne Makinda,
Jumanne ya wiki hii Chadema ilifanya mkutano wa dharura kujadili mambo
kadhaa ya kitaifa.
Siku moja baada ya kikao hicho, viongozi
wa waandamizi wa Ukawa walikutana na kujadili mambo yanayohusu umoja
huo kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba.
Baada ya vikao hivyo, mpaka jana Chadema
iliendelea na vikao vyake vya ndani kujadili mambo kadhaa kabla ya
kikao cha Kamati Kuu ya Ukawa kinachotarajiwa kufanyika leo kupitisha
mgombea urais.
Naibu Katibu Mkuu wa Chadema Bara, John
Mnyika licha ya kuthibitisha kuendelea kwa vikao vya ndani juzi, hakuwa
tayari kusema chochote kwa sababu ajenda bado zinajadiliwa na kwamba
kesho taarifa za uhakika zitatolewa kwa vyombo vya habari.
0 comments:
Post a Comment