UTAKUWA
umesikia au kuona simulizi nyingi zinazowahusu wadada wa kazi
wanazokutana nazo katika familia mbalimbali. Licha ya umuhimu wao
mkubwa, lakini baadhi yao wamekuwa wakichukuliwa kama watu wenye shida,
wasio na maana ambao licha ya kazi yao ngumu na muhimu kwa familia,
wamekuwa wakibezwa, kutukanwa na hata kupigwa.
Filamu ya Kajala inawakilisha aina hii
ya kazi zinazofanywa na wasichana, ambao uzoefu unaonesha wanatokana na
maisha magumu katika familia wanazotoka, yatima au hata manyanyaso
kutoka kwa ndugu wa karibu.
Riyama amecheza kama ndiye msichana wa
kazi akiigiza kwa jina la Kajala, ambaye alijikuta akiifanya kazi hiyo
baada ya kuondoka kijijini kwao na kuja Dar es Salaam akiwa na lengo la
kumtafuta baba yake mzazi, ambaye hakuwahi kumuona kabla.
Ni kazi inayoakisi ukweli, kwani
wasichana wa kazi ni kama watu wenye gundu hivi, kwa mfano katika nyumba
ya kwanza alikokuwa akiwafanyia Kajala Masanja na Haji Adam waliokuwa
wanandoa, msichana huyo wa kazi anajikuta akichukiwa na mwanamke
mwenzake kwa sababu tu mumewe alikuwa akimsifia kwa upishi wake mzuri.
Baada ya kufukuzwa kwa kosa la ‘kupika
vizuri’, Kajala hajui pa kwenda lakini bahati nzuri anakutana na kaka
mmoja ambaye baada ya kujieleza, anagundua kuwa ni watu wa kutoka sehemu
moja, hivyo badala ya kumruhusu kurudi kijijini kwao, anamtaka kuishi
chumbani kwake ili aendelee kutafuta kazi jijini Dar.
Anapata kazi ya usaidizi wa ndani katika
nyumba ya wanandoa wawili ambao kwa bahati mbaya hawakujaaliwa kupata
mtoto. Huko, kama inavyowatokea wasichana wengi, anakutana na mtihani
mkubwa wa kutakwa kimapenzi na baba mwenye nyumba, ambaye anamuahidi
vitu vingi endapo atamkubalia.
Kajala anakataa katakata kiasi hata cha
kutishia kuondoka. Baba mwenye nyumba anamuomba msamaha na kuondoka,
lakini anaendelea kumsumbua msichana huyo kupitia simu yake ya mkononi,
akimpigia na kumtumia ujumbe, ambao siku moja unanaswa na mkewe.
Mkewe anakuja juu bila kujali utetezi
wake, anamfukuza wakati mumewe akiwa kwenye mitikasi. Anarudi nyumbani
akiwa na mawazo mengi, lakini ghafla mtu mmoja anamtupia begi naye
kupotelea kusikojulikana. Alipolifungua, anakuta burungutu la fedha na
kitambulisho kinachoonesha ni cha Mamboleo, yule tajiri aliyesababisha
akafukuzwa.
Anajaribu kwenda kwa Mamboleo ili
kumpelekea hela zake, lakini anafukuzwa na mkewe kama mbwa, akiamini
bado wana uhusiano wa kimapenzi. Mumewe anaporudi nyumbani na kuulizia
alipo Kajala, mkewe anamfahamisha kuwa alimfukuza kwa sababu ya mambo
yao. Anasikitika sana.
Kutopata mtoto kunamfanya Mamboleo
amkumbuke mwanamke aliyempa ujauzito kule kijijini, anakwenda na
kuambiwa kuwa mkewe huyo alishafariki siku nyingi na binti aliyezaliwa
kaenda mjini. Anaoneshwa picha ya bintiye na kukuta ni Kajala!
Ni filamu nzuri ingawa kama zinavyokuwa
nyingi za Kibongo, zina kasoro kadhaa za kiufundi ambazo kama
zingerekebishwa, zingekuwa nzuri zaidi. Kwa mfano, Mamboleo anapomuona
Kajala akiwa kwenye Bajaj anaposhuka na kumfuata, anaonekana akimwelezea
kuwa yeye ni binti yake na anaomba amsamehe kwa yote.
Lakini inashangaza kidogo kwamba wakati
picha inawaonesha kuwa wako mbali, sauti inasikika kama wapo karibu. Na
kitu kingine ni kwenye begi la fedha lililoporwa. Begi hilo lilikutwa
siti ya mbele ya gari, dhahiri kwamba zilikuwa ni fedha za dili, katika
hali ya kawaida mtu unawezaje kuweka kitambulisho chako kwenye begi la
kubebea hela, hata kama alizitoa benki?
0 comments:
Post a Comment