Friday 10 July 2015

Mgombea Urais Ukawa Hadharani Kesho

...
INNOCENT-THE BLOGGER-BOYpic+ukawa
viongozi wanaounda Umoja wa Katiba ya Wananchi ( Ukawa), kutoka kushoto ni James Mbatia,Freeman Mbowe na kulia ni
Profesa Ibrahim Lipumba.
Kwa ufupi
•Taarifa zilizopatikana jana zimeeleza kuwa baada ya kikao cha viongozi wa ngazi za juu wa Ukawa, umoja unaoundwa na NLD, Chadema, CUF na NCCR – Mageuzi kilichofanyika juzi, mambo kadhaa yameafikiwa na kama hakutokuwa na mabadiliko yoyote, mteule wa urais kupitia umoja huo atabainishwa.
Na Julius Mathias – Mwananchi
Posted Ijumaa, Julai 10, 2015 (10:33am)
Dar es Salaam. Baada ya vikao mfululizo wiki hii, hatimaye Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) unatarajia kumtangaza mgombea urais wake kesho.
Taarifa zilizopatikana jana zimeeleza kuwa baada ya kikao cha viongozi wa ngazi za juu wa Ukawa, umoja unaoundwa na NLD, Chadema, CUF na NCCR – Mageuzi kilichofanyika juzi, mambo kadhaa yameafikiwa na kama hakutokuwa na mabadiliko yoyote, mteule wa urais kupitia umoja huo atabainishwa.
Mwenyekiti Mwenza wa Ukawa, Dk Emmanuel Makaidi alithibitisha kuwa tayari makubaliano ya kugawana kata na majimbo kwa nafasi za udiwani na ubunge yamekamilika na kilichobaki ni utekelezaji.
“Tumeshakubaliana namna ya kugawana kata na majimbo 13 yaliyobaki na Jumamosi tutaweka wazi kwa wananchi. Pamoja na hilo pia tutamtangaza mgombea urais na chama anachotoka,” alisema Dk Makaidi.
Siku chache baada ya baadhi ya wabunge kupewa adhabu ya kutohudhuria vikao vya Bunge na Spika Anne Makinda, Jumanne ya wiki hii Chadema ilifanya mkutano wa dharura kujadili mambo kadhaa ya kitaifa.
Siku moja baada ya kikao hicho, viongozi wa waandamizi wa Ukawa walikutana na kujadili mambo yanayohusu umoja huo kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba.
Hata baada ya vikao hivyo, mpaka jana Chadema iliendelea na vikao vyake vya ndani kujadili mambo kadhaa kabla ya kikao cha Kamati Kuu ya Ukawa kinachotarajiwa kufanyika leo kupitisha jina la mgombea urais.
Naibu Katibu Mkuu wa Chadema Bara, John Mnyika alithibitisha kuendelea kwa vikao vya ndani vya chama hicho na kueleza kuwa hawezi kusema chochote kwa sababu ajenda bado zinajadiliwa na kwamba kesho taarifa za uhakika zitatolewa kwa vyombo vya habari.
“Kwa kifupi ni kwamba kikao bado kinaendelea. Nimetoka mara moja tu kupokea simu yako. Mazungumzo yatakapokamilika tutawajulisha (vyombo vya habari),” alisema Mnyika.
Mvutano
Wakati hilo likisubiriwa, zipo taarifa kuwa kuna mvutano baina ya vyama ndani ya umoja huo hasa katika nafasi ya mgombea urais baada ya kuwapo kwa watia nia zaidi ya mmoja.
Chanzo cha uhakika kutoka ndani ya umoja huo kilisema kuwa Kamati Kuu ya Ukawa ina kazi kubwa ya kuhakikisha kuwa maridhiano yanafikiwa ili kumpata mgombea atakayeungwa mkono na vyama vyote katika jitihada za kuiondoa CCM madarakani.
“Licha ya kutangaza kugawana kata na majimbo yaliyobaki jina la mgombea urais litatangazwa pia. Hilo litafanyika endapo mwafaka utapatikana katika kikao cha Kamati Kuu kitakachofanyika kesho (leo). Kikao kikiridhia chama gani kitoe mgombea, basi Watanzania watamjua hiyo Jumamosi,” kilisema chanzo hicho.
Chadema na CUF bado viliendelea na vikao vyake vya ndani jana. Mkurugenzi wa Mipango na Uchaguzi wa CUF, Shaweji Mketo alisema hakuna taarifa ambayo ingeweza kutolewa jana.
Alipoulizwa juu ya makubaliano yaliyopitishwa katika kikao cha Ukawa alijibu: “Hakuna maazimio yaliyofikiwa, bado tupo katika mjadala.”
Kuhusu kuungwa mkono miongoni mwa vyama vingine vya Ukawa kwa Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba aliyetangaza nia, Mketo alisema hana taarifa.
Wenyeviti wenza wengine wa vyama hivyo hawakupatikana kuzungumzia suala hilo. Hata walipopigiwa simu zao za mkononi, ziliita pasi na kupokewa.
Mwananchi: Mgombea urais Ukawa hadharani kesho
Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger