Mbunge wa Monduli kwa tiketi ya CCM na Waziri Mkuu wa zamani, Edward Ngoyai Lowassa (ndani ya gari) akilakiwa na makada wa CHADEMA alipowasili mkoani Arusha juzi jumatano.
Mamia ya makada wa Chama cha Demokrasia
na Maendeleo (Chadema), katika Jimbo la Monduli mkoani Arusha,
wamejitokeza kumpokea Waziri Mkuu wa zamani, Edward Ngoyai Lowassa
(pichani) ambaye ni mbunge wa jimbo hilo kwa tiketi ya Chama Cha
Mapinduzi (CCM). Juzi Jumatano, habari zilizopatikana kutoka kwa mtoa
taarifa wetu jimboni humo zilieleza kuwa, wanachama hao walifikia hatua
hiyo kufuatia jina la Lowassa kuenguliwa kwenye kinyang’anyiro cha
kumpata mgombea urais kupitia chama chake, nafasi ambayo ilichukuliwa na
Dk. John Pombe Magufuli.
ANAKWENDA KUJIANDIKISHA
Baada ya kuwepo kwa taarifa kwamba
Lowassa angeenda kujiandikisha katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura
kijijini kwake, Ngarash, Monduli ndipo wanachama hao wa chama hicho
kikuu cha upinzani walipokusanyika barabarani wakimsubiri.
“Watu walikuwa ni wengi sana. Ukweli
walikuwa ni mamia. Kuna walioweka kambi nyumbani kwake kumsubiri
(alikuwa akitokea jijini Dar). Walikuja kumpokea kwa shangwe. Kila mtu
alikuwa na bendera ya Chadema.
“Wengi wa wanachama wa Chadema
wanaojiita makamanda walikuwa ni bodaboda ambao kila mmoja alikuwa
amechomeka bendera ya Chadema kwenye pikipiki yake, kichwani walikuwa
wamevaa boshori (aina ya kofia) za Chadema. “Wakati mzee (Lowassa)
anajiandikisha, zoezi ambalo kwa sasa linaendelea mkoani humo, nje ya
kituo hicho, wanachama wa Chadema walipaza sauti, wakiimba ‘mzee karibu
Chadema’, karibu CDM, wewe ni jembe, jiwe walilolikataa waashi litakuwa
jiwe kuu la pembeni’ huku wakimalizia na people’s…power,” alisema mtoa
habari wa gazeti hili na kuongeza:
“Walikuwa wakimwambia Lowassa kuwa
Mwalimu Julius Nyerere hakukosea aliposema kuwa upinzani wa kweli
utatoka CCM hivyo wakati ndiyo huu. Ilibidi kuimarisha ulinzi hadi
Lowassa amalize kujiandikisha kwani kwa kadiri muda ulivyokuwa ukisonga
ndivyo watu walikuwa wakiongezeka.”
WATAKA TAMKO LAKE
Mtoa habari wetu alieleza kwamba, baada
ya Lowassa kujiandikisha, alipotoka nje ili kuondoka eneo hilo kuelekea
nyumbani kwake, wanachama hao walimzingira wakitaka kusikia tamko lake,
wakimuomba kujiunga na Chadema.
Alisema kuwa Lowassa aliingia kwenye
gari tayari kuondoka eneo hilo na msafara wake lakini makada hao
waliziba barabara kwa pikipiki wakimuomba aseme neno juu ya kuhamia
Chadema ambacho wanaimani nacho ili roho zao zitulie.
NENO LA LOWASSA
Hata hivyo, Lowassa ambaye hakutaka
kuzungumza chochote huku akionekana mwenye huzuni, alivunja ukimya ili
wamwachie aende zake akawaambia.
“Endeleeni kuwa na imani na chama chenu (Chadema).”
Baada ya kusema maneno hayo, Lowassa
aliondoka kuelekea nyumbani kwake huku wanachama hao wakimsindikiza,
wakiimba people’s power.
DURU ZA KISIASA
Ukiachilia mbali tukio hilo lililovuta
hisia za wengi, duru za kisiasa ziliyaangazia madai kwamba, wanachama
hao hawakukurupuka kwani madai ya Lowassa kuhamia Chadema yalikuwa
yameenea kilakona ya nchi.
Mara tu baada ya kukatwa kwa jina lake
mjini Dodoma mwishoni mwa wiki iliyopita na kurejea jijini Dar, ilidaiwa
kwamba alifanya mazungumzo na viongozi wa ngazi ya juu wa Chadema juu
ya kuhamia kwenye chama hicho na kupata nafasi ya kugombea urais ili
akapimane ubavu na Dk. John Magufuli.
ZOEZI LA KUHAMIA CHADEMA
Habari za kina zilidai kwamba, zoezi
hilo la Lowassa kukihama chama chake ambacho amekuwa kada wake kwa miaka
38 na kwenda Chadema lilikwamishwa kwa namna mbili.
Mosi; ilidaiwa kuwa makubaliano yake na Chadema hayakwenda sawia kwani viongozi hao wa juu wa Chadema hawakuafikiana.
Pili; duru za kisiasa zilieleza kuwa
Lowassa alikutana na wazee wa CCM ambao walimweleza madhara ya kukihama
chama hicho na mustakabali wake wa baadaye kisiasa.
MTU WA KARIBU
Akizungumzia suala hilo la tishio la
kuhamia Chadema, mmoja wa watu wake wa karibu (jina tunalo) aliliambia
gazeti hili kuwa, watu wasubiri muda ukifika Lowassa atautangazie umma
uamuzi wake.
KINGUNGE ASISITIZA
Wakati upepo ukiwa bado haujatulia, kada
mkongwe wa CCM, Kingunge Ngombale Mwiru ameendelea kusisitiza kwamba
Lowassa ndiye chaguo sahihi la chama hicho kwa ngazi ya urais kwani
kitendo cha kuliengua jina hilo kimeacha kasoro na mpasuko ndani ya
chama chake.
Alisema kuwa, licha ya jina lake
kutopitishwa kugombea urais badala yake akapitishwa Dk. Magufuli bado
anaamini yeye ndiye mshindi katika sakata hilo kwa kuwa ndiye mgombea
anayependwa zaidi na Watanzania.
0 comments:
Post a Comment