Karibu
kila mtu anatafuta furaha kwa njia mbalimbali anazoona zinafaa. Wapo
wanaoamini kuwa wakipata wake/waume, kazi, utajiri, wakijenga nyumba,
wakipandishwa cheo na kufaulu mitihani watafurahi sana.
Lakini tafiti zinaonesha kuwa asilimia
87 ya wanaohangaika kutafuta hayo wanayodhani yatawafurahisha huwa
hawafurahi sawa na matarajio yao ya awali.
Wataalamu wanakubaliana kuwepo kwa
furaha katika siku za mwanzo za kutimia kwa malengo ya watu, lakini
kiwango cha furaha kimebainika kupungua kadiri mtu anavyozidi kuishi
ndani ya kile alichokitamani au alichodhani akikipata kitamfurahisha.
Ukubwa wa furaha ya siku ya kuchumbiwa,
kununua gari, kuhamia katika nyumba mpya, kupandishwa cheo, kuongezwa
mshahara, kuolewa au kuoa, hushuka kila siku na hivyo kumfanya mtu
afikie hatua ya kuona alichokipata si kitu cha kufurahisha sana na hivyo
kuingiwa na mawazo ya kutafuta vitu vingine ambavyo atavipa nafasi
kubwa ya kumfurahisha.
Unaposoma haya jaribu kukumbuka moja
kati ya vitu ulivyovihangaikia na hatimaye kuvipata, siku hiyo ulikuwa
na furaha ya kiwango gani ukilinganisha na sasa?
Bila shaka unatambua kuwa ulivyofurahi
siku ulipoolewa ni tofauti na unavyofurahi leo, ingawa ndoa uliyoitafuta
ni ileile na mwanaume uliyenaye ni yuleyule, tena inawezekana mlipooana
mlikuwa na maisha ya chini lakini leo mmefanikiwa isipokuwa furaha
imepungua.
Hapo kuna jambo la kujiuliza kwa nini
wengi wetu tunashindwa kupata furaha ya kweli na kubaki kila siku ni
watu wa kuhangaika kutafuta hiki na kile cha kutufurahisha.
Mara nyingi kwa uzembe wa kuwaza
anachokuwa nacho mtu si bora kuliko kile anachotafuta. Mwanamke mzuri
daima hawi mkeo bali ni wa jirani (mtazamo tu), ndiyo maana wengi
hufumaniwa na kwa mshangao wanawake ambao hufumwa nao huwa si wazuri
ukilinganisha na walio nao.
Kama nilivyoeleza awali kwamba, tuna
kila sababu ya kujifunza namna ya kutafuta na kupata furaha ya kweli,
ambapo leo tutaangali baadhi ya mambo yanayoweza kutusaidia kupata
furaha ya kweli katika maisha yetu ya kila siku. Mambo hayo
tutayatafakari kwa kujiuliza aina hii ya maswali.
A-Je tunapokuwa tunatafuta furaha
tunatumia uwezo wetu wote au kwa kiwango kidogo? Kama tunatumia kiwango
kidogo basi tujue kuwa hata kama tutapata kitu tunachodhani
kitatufurahisha tutajikuta hatufurahi, kwa sababu tulichopata
kimeshindwa kukidhi matakwa yetu. Ili uwe na furaha ya kudumu tumia
uwezo wako wote kutafuta kazi nzuri, biashara nzuri, mke mzuri ili uweze
kufurahi kwa muda mrefu, la sivyo ulichopata kitakukinai mapema.
B- Je, tunafanya sawa katika maamuzi au
tunabahatisha tu? Endapo tutakuwa tunafanya mambo ya kubahatisha ambayo
hatujayahakiki, huzuni yetu itakuwa kwenye makosa na kamwe hatuwezi
kufanikiwa kupata yale tunayotaraji yatufurahishe.
Kuna watu wanatafuta watoto lakini
hawazingatii kalenda za mimba na wengine wanatafuta mali, elimu kubwa,
mke mwema, lakini hawako makini katika kufanya maamuzi kwa usahihi. Ni
vema tukathibitisha uchaguzi wa mambo ili tufanikiwe kupata
yatakayotufurahisha.
0 comments:
Post a Comment