Wednesday 15 July 2015

MZEE KINGUNGE NGOMBALE MWIRU ALALAMA JUU YA KUKATWA KWA JINA LA EDWARD LOWASSA KUWANIA URAIS

...
INNOCENT-THE BLOGGER-BOY
????????????????????????????????????

Mzee Kingune Ngomale Mwiru akizungumza na waandishi nyumabni kwake Victoria leo jijini Dar es salaam kuhusu kukatwa kwa jina la Lowassa kwenye Uteuzi wa jina la Mgombea wa Urais wa jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia CCM 
…………………………………………………………………………
Utaratibu uliotumika kumteua mgombea urais wa Tanzania kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), umekosolewa na mwanasiasa wa siku nyingi  Kingunge Ngombale Mwiru kwa madai Kamati ya Maadili haikuwa na maadili kwa kumwengua Edward Lowassa.
Amesema hayo leo  nyumbani kwake jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari akelezea alichokiita  kuparaganyika kwa CCM kutokana na kukatwa jina la mwanachama aliyemwamini ndiye anafaa kuongoza chama na serikali.
Katika kuonyesha ameudhika na kamati zilizoundwa na chama hicho kupitisha na kukata wagombea, Kingunge amesema anasikitika kuona Tanzania ni nchi yenye watu wapole wasiojua kulalamika wala kuhoji hivyo amejitokeza kuhoji kwa niaba yao.
“Lakini yaliyotokea Dodoma safari hii ni mapya, kazi ya kupeleka majina matano ilifanywa na chombo kisicho na mamlaka, Kamati Kuu ilipewa majina bila kuwahoji wagombea. Kamati ya Maadili ni kitengo tu hakina nguvu zaidi ya Kamati Kuu, NEC au mkutano mkuu.
“Kitendo cha kuinyang’anya Kamati Kuu mamlaka yake ni kibaya, wanajiita kamati ya maadili wakati kamati yenyewe haina maadili, hii nchi ni yetu sote hata chama ni chetu sote wachache tuliowapa madaraka ndani ya chama na serikali wanadhani nchi ni yao,” alisema Kingunge.
Aliweka wazi kuwa anawaheshimu viongozi wastaaafu Ali Hassan Mwinyi, Benjamin Mkapa na Amani Abeid Karume kutokana na umahiri wao waliouonyesha katika mchakato huo lakini akadai nao wamepotoshwa kwa sababu wameshinikizwa kulikata jina la Lowassa kutokana na taarifa zisizo sahihi.
Akikumbushia yaliyotokea katika mchakato wa kutafuta mgombea wa CCM mwaka 1995, Kingunge alisema “yalipoletwa majina sita katika mkutano wa NEC mwaka 1995 yalionekana majina ya Benjamin Mkapa, Jakaya Kikwete, Pius Msekwa, Cleopa Msuya, Mark Bomani na Joseph Warioba. Wajumbe wakahoji jina la Lowassa liko wapo.
“Lowassa alijiuzulu kuwajibika kisiasa lakini pia likageuzwa na watu kuanza kuimba wimbo wa ufisadi, mimi nilipoona anaonewa nikaamua kukaa kimya na kumshauri ajiuzulu kwa sababu nilishapata taarifa kuwa wanataka kumchafua. Nikamwambia kabla lengo lao halijatimia bora ajiuzulu kulinda hadhi na mustakabali wake kisiasa.”
Aliongeza kuwa Lowassa anakubalika ndani nje ya chama, hata kashfa anazopewa kuwa alitumia fedha nyingi wakati wa kutangaza nia hadi kurudisha fomu si za kweli anasingiziwa tu, Kingunge anamtaja kada huyo amelelewa na chama hivyo anakijua vema kuliko wagombea wengine waliopita kwenye tano bora.
“Tunapomtafuta rais kupitia CCM ikumbukwe pia tunamtafuta mwenyekiti wa chama, maana yake tukimpata mgombea mwingine inabidi tuwe na kazi ya ziada kujifunza masuala ya chama. Mkasa huu wa viongozi wa chama na serikali kutumia nguvu nyingi kuzuia mapenzi ya wananchi wajue kuwa huyo waliyemkusudia hawatampata,” alisema.   
Alipoulizwa ikiwa anakubali uteuzi wa Joseph Magufuli, alisema kwa sasa hana budi kuwaomba wanachama wote kuunga mkono uteuzi huo kwani walioingia katika tano bora hawana makosa hata wao walichaguliwa tu.
Kingunge ametoa angalizo kuwa baada ya uchaguzi kuisha lazima suala hilo lijadiliwe kwa sababu chama kimegawanyika vipande vipande kutokana na mgombea aliyekubalika na wanachama wengi kukatwa bila kufuata taratibu.
“Kwa upande wangu naona ni kama Lowassa ndiye aliyeshinda katika ushindani huu kwa sababu watu ndaNi na nje ya nchi wameona namna anavyokubalika, Lowassa ni kipenzi cha watu na hakuna kitu kizuri kama kupendwa,” alisema.
Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger