Jamani
mbona tunajisahau na kuamini kabisa kinachotokea leo tunaonewa. Mzazi
jamani anazungumza mpaka mdomo unataka kupasuka lakini mtoto ndiyo
kwanza kama katiwa moto anaambiwa afanye.
Juzi nimemkuta mama mtu mzima akitokwa
na machozi baada ya mabinti zake kushindwa kumsikiliza kila alilokuwa
akiwaambia, lilikuwa likipitia kulia na kutokea kushoto.
Nilipofika aliniomba nimsaidie kuwaeleza wanaye ili wamwelewe.
Ni kweli hii ndiyo kazi yangu
kuwakumbusha watu waishi vipi katika uhusiano wao au familia zao. Siku
zote samaki akikunjwa mdogo, ukubwani hupati kazi, ila ukifanya makosa
akiwa mdogo akikua una kazi ya ziada.
Shoga yangu ni mtu niliyemfahamu vizuri
alikuwa tofauti na mimi, yeye aliolewa na mtu mwenye uwezo. Hakuwa na
majivuno ila alijitahidi kwenda na wakati kwa vile ankra ilikuwa
inamruhusu.
Mavazi yake hayakuwa tofauti na
machangudoa, ukikutana naye ghafla utajua yupo kwenye mawindo. Watoto
wake aliwalea kizungu, heshima ilikosa nafasi, kwake kukaa nusu utupu
hata mbele ya watoto wa kiume haikuwa tabu. Hali ile iliendelea mpaka
mumewe alipofariki ghafla.
Ilibidi arudie hali ya zamani ya
ustaarabu, siku hizi swala tano lakini wanae wa kike hawashikiki kwa
mavazi ya aibu hata heshima imepotea, midomo yao imekosa staha,
hawamsikii mama yao kwa kila jambo.
Baada ya kupewa kazi hiyo naomba wiki
hii nizungumze na wazazi wanaojisahau ili wiki ijayo nizungumze na
watoto wenu. Wazazi wengi ambao Mungu amewaangalia kwa jicho la neema,
wamekuwa wakijisahau na kuhadaika na kile walichokuwa nacho kwa muda
ule.
Neema ile imewafanya kudharau mila na
desturi yao, wengi tumekuwa tukiishi kizungu, kuvaa nguo zisizostahili
kuvaliwa mbele ya watoto na jamii inayotuzunguka. Tumekuwa tukitokwa na
maneno machafu bila kujua lile ni somo tosha kwa wanetu.
Mtoto anapokuwa na mzazi wake hujifunza
mambo mengi ambayo huyaona anapenda kuyafanya. Kama mama ukiwa na
heshima basi mwanao atakuwa na heshima, kama ukiwa msafi au kupenda
kupika vilevile mwanao atajifunza kutoka kwako.
Lakini ukiwa hujiheshimu, huna staha na
maneno yako, mvivu unapenda maisha ya starehe, mwanao lazima atachukua
hivyo kwa vile ameviona kwako.
Tunajisahau kuwa kila kukicha ndivyo umri unavyokwenda.
Umefika wakati ni mtu mzima mambo ya
kijinga hutaki tena na umegundua uliyofanya ni ya kijinga, sasa unataka
kuisaidia familia yako isifanye uliyoyafanya kwa vile hayana faida.
Lakini kila ukisema hawakusikii na hata
ukitishia kuwatolea radhi hawakuelewi, unajua kwa nini? Kwa sababu tabia
hizo wamejifunza kwako.
Jamani wazazi wenzangu hebu tuwe mfano
bora kwa watoto wetu ili tusipate wakati mgumu katika kuwanyoosha. Ni
kweli dunia sasa hivi imevaa msuli, watoto wa kike wamekuwa mtihani.
Lakini tukiwalea vizuri tangu mwanzo kwa kukemea lolote unaloliona
linakwenda vibaya kwa nguvu zote itasaidia sana kutengeneza kizazi
chenye heshima na kujifahamu. Lakini mama hujiheshimu, mwanao heshima
ataitoa wapi. Tubadilike ili tutengeneze familia bora.
Yangu kwa leo yanatosha. Ni mimi Anti Nasra Shangingi Mstaafu
0 comments:
Post a Comment