Staa wa Filam za Bongo, Jacob Steven 'JB'.
MPENZI msomaji, wiki iliyopita tulikomea pale JB alipokuwa anasimulia jinsi alivyojibizana na wazazi wake hadharani baada ya kuambiwa jambo ambalo aliona kabisa halikuwa sahihi kwa wakati ule. Je, ni jambo gani hilo? Teremsha macho hapa chini.
“Waliniambia kuwa wamefikiria na kuona nafaa kurudi tena shuleni, jambo lililonipelekea kubishana nao kwa wazi na kwa mara ya kwanza kabisa maishani mwangu, tangu niwe mtu mzima,” anasema JB na hapohapo namuona akichukua simu yake ya gharama na kubonyeza kwa muda kabla ya kuiweka sikioni na kuzungumza na mtu wa upande wa pili.
“Eee mama, nipo na mwandishi wa habari hapa, tunazungumzia maisha yangu yote na hapa tumefikia kwenye kipengele ambapo nilijibizana na ninyi mkitaka nirudi tena shuleni baada ya kuhitimu mafunzo ya kijeshi na kukaa nyumbani kwa muda mrefu bila kazi,” anasikika JB akizungumza na mama yake kupitia simu yake, mbele yangu wakati mahojiano yakiendelea huku akiwa ameweka mfumo wa sauti ya juu (loud speaker).
“Aaah, nawe Jacob, mambo ya zamani huko bado unayo hadi sasa? Haya bwana nyie endeleeni lakini na mimi umenikumbusha nyuma kidogo,” inasikika sauti ya mama yake na JB kupitia simu ya mwanaye jambo lililoongeza msisimko wa mazungumzo yangu na gwiji huyo wa sanaa ya uigizaji kwa sasa.
“Mmh, sasa ikawaje kaka?,” namuuliza huku nikikohoa kidogo kuliweka sawa koo langu.
“Basi bwana, baada ya msuguano wa hapa na pale nikakubali kwa shingo upande lakini sikudumu sana shuleni na tayari kwa kipindi hicho akili yangu ikawa inawaza kitu kingine kabisa tofauti na mambo ya shule,” anasema.
JB anasema, baadaye aliamua kujiingiza kwenye biashara ya kuuza nafaka kama mpunga na mahindi, biashara iliyokuwa ikifanywa na kaka zake tangu yeye akiwa shuleni. Hata hivyo, wazazi wake waliamua kumuunga mkono kwa kumnunulia mashine za kusaga unga na kukoboa, hali ambayo kwa kinywa chake anakiri kumuongezea morali wa biashara.
“Ikawa ni kama wamemkabidhi rungu kichaa, nikajikita zaidi kwenye biashara, nikawa nafuata mpunga huko Mbeya, na wakati mwingine nafuata mahindi mkoani Tanga,” anasema lakini safari hii akionesha hali ya kupoteza furaha na munkari ya kuongea ghafla.
“Mbona kama umepoa tena kaka, kulikoni?,” namuuliza huku nikimtazama usoni kwa umakini.
“Kuna kitu nimekumbuka hapa, unajua wakati naanza kufuata mahindi huko Tanga, kuna wakati nilikuwa nakumbana na mazingira magumu sana na hatimaye kupelekea kuugua fangasi miguuni, miguu ilivimba na hadi sasa kuna alama kadhaa kuanzia kwenye nyayo kuja hadi sehemu za juu huku,” anasema JB na hapohapo namuona akishika mguu wake wa kushoto.
JB alikunja suruali na kushika gidamu (kamba za viatu) kabla ya kuzilegeza na kuvua viatu na soksi kwa lengo la kunionesha alama za miguuni zilizotokana na kuugua vibaya fangasi.
“Unaona mdogo wangu, usije ukadhani naongea tu kwa lengo la kujipatia sifa za kijinga, I hate cheap popularity (nachukia umaarufu wa bei nafuu),” anasema JB huku akizidi kunionesha alama hizo nami nikimtazama kwa jicho la udadisi zaidi.
“Unajua mdogo wangu, watu wengi sana hukosea jambo moja maishani,” anasema lakini kabla hajaendelea, anapaliwa na kitu hali iliyompelekea kukohoa.
“Dah, sijui nani tena ananisema bwana, lakini nataka kusema kitu kimoja kwamb….(anakohoa tena, safari hii mfululizo hadi machozi yanamtoka).
“Pole sana kaka,” nikajikuta nikimunea huruma.
Je, ni kitu gani ambacho JB anataka kukisema hapa? Usikose kufuatilia tena wiki ijayo kwenye simulizi hii tamu ya nguli huyu wa filamu hapa Bongo.
. Ramadhani Kareem!
0 comments:
Post a Comment