Tuesday 15 July 2014

TRAFIKI WA KIKE: ATEKWA JIJINI DAR

...
INNOCENT-THE BLOGGER-BOY


Alexander Msowoya (35), ambaye ni mkazi wa Chang’ombe, jijini Dar es Salaam, amefikishwa katika Mahakama ya Mwanzo Magomeni akikabiliwa na shtaka la kumteka nyara askari wa kike wa usalama barabarani.

Akiwa anaendesha gari, mshtakiwa huyo anadaiwa kumteka Kostebo Ester katikati ya maeneo ya Tameke na Chang’ombe kabla ya kukamatwa maeneo ya katikati ya Mabibo na Ubungo baada ya msako mkali wa polisi waliokuwa wakitumia redio za upepo.

Hati ya mashtaka iliyosomwa mbele ya hakimu Mwanaidi Ngoda ilidai kuwa Julai 11, mwaka huu, saa 9:00 alasiri, eneo la kati ya Temeke na Chang’ombe, mshtakiwa alimteka nyara askari polisi Konstebo Ester, alipotakiwa kuonyesha leseni yake.

Ilidaiwa kuwa Afande Ester alimkamata mshtakiwa huyo akiwa anaendesha gari lenye namba za usajili T 495 BKJ na kumtaka aonyeshe leseni yake, lakini hakufanya hivyo.

Baada ya hapo, ikadaiwa kuwa trafiki huyo wa kike akamwamuru dereva huyo aliyekuwa anaendesha gari aina ya Rav4 ya rangi ya bluu kuweka gari lake pembeni, lakini alikaidi kwa kudai ana haraka.

Kutokana na hali hiyo, ilidaiwa kuwa askari aliingia ndani ya gari kwa kupitia kwenye mlango wa nyuma na kuamuru waende kwenye kituo cha polisi Chang’ombe.

Hata hivyo, ilidaiwa kuwa badala ya kuelekea alikoelekezwa, mshtakiwa alianza kwenda anakokujua yeye, hivyo kukiuka amri halali ya polisi na kitendo hicho kuhesabika kama ni utekaji nyara.

Awali, kabla ya kesi hiyo kusomwa, askari polisi mmoja alimwambia mwandishi wa habari hizi kuwa kilichomuokoa afande Ester ni redio ya mawasiliano aliyokuwa nayo, ambayo kwa kiasi kikubwa ilifanikisha kujua walipo na wanakoelekea.

Hivyo, walikuwa wakifanya mawasiliano na askari wengine waliokuwa maeneo mbalimbali gari linapopita na ikasaidia kukamatwa.

“Afande amepumzika nyumbani kwake. Kwa sasa hali yake si nzuri ana presha kutokana na tukio hili,” alisema askari mmoja wa kiume mahakamani hapo, ambaye hakutaka kutaja jina lake.

Hata hivyo, alidokeza kuwa kuna uwezekano mkubwa kesi hiyo ikapelekwa kwenye mahakama za juu kutokana na uzito wake, kwani ni ya utekaji nyara.

Mshtakiwa alikana shtaka hilo na kupelekwa rumande. Kesi hiyo imepangwa kuendelea tena Julai 27, mwaka huu.
Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger