Tuesday 15 July 2014

CCM 2015:SUMAYE AMSHUKIA JANUARI AULIZA NANI HAJAWAHI KUWA KIJANA ADAI KWA KANUNI ZA CCM JANUARI NI MZEE

...
INNOCENT-THE BLOGGER-BOY
WAZIRI Mkuu wa zamani, Frederick Sumaye, amewashukia wale wanaotumia kete ya umri kuwania urais na kwamba, hawafai kuwa viongozi wa taifa la Tanzania.
Kauli hiyo, inaonekana ni kujibu mapigo ya Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba (40), ya kuwataka wazee wakae pembeni na kuwachia vijana kuwania urais katika uchaguzi mkuu ujao.
Sumaye, aliyasema hayo jana wakati akihojiwa na kituoa cha runinga cha Star cha jijini Mwanza jana.
“Nakumbuka mwaka 2005 wakati Rais Jakaya Kikwete hajawa Rais, akigombea nafasi hiyo kulitawala msemo huo wa kumtaka kwa turufu ya kusema ni kijana, huku wakati huo alikuwa na miaka 55, wengine tukawa tunajiuliza hivi, kumbe mwenye miaka 55 ni kijana,” alihoji Sumaye.


Alibainisha kuwa, kwa kufuata misingi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), hafikirii kama kuna kijana hata mmoja ambaye ana sifa ya kuwa Rais, kwani chama hicho kinamtambua kijana ni yule mwenye miaka 18 hadi 35.
“Kwa misingi hiyo, sijajua kama kijana anayemaanishwa kwa sasa ni huyo au mtu mzima ambaye hajazeeka, hivyo kwa maoni yangu kiongozi anayetufaa ni mtu tunayemuona ana nguvu, muadilifu, mchapakazi na anayetaka kutuongoza na sisi tunaona anatufaa, bila kujali kama ni kijana, mwanamke, mlemavu au ni wa dini gani, anatoka wapi, ili mradi ni mtanzania, kwa dhamira ya wazi huyo atatusogeza mbele na ndiye tutakayemtaka na si kwa sababu ya ujana au uzee wake,” alisema.
Sumaye, alimnukuu Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere kuwa, aliwahi kuzungumzia suala hilo wakati lilipojitokeza katika chaguzi zilizopita akisema; “Ujana si sifa, nani hajawahi kuwa kijana?’.
Sumaye alisema, ujana ni hatua ya binadamu ya kukua na haiwezi kuwa sifa ya urais, kwani sifa ni tofauti na ujana.
“Simaanishi kwamba vijana hawafai kuwa viongozi, ila kama yupo anayefikiria kwa maana anaitwa ‘fulani fulani’ anaona ana uwezo wa kuendesha hii nchi na watu wakakubali kwamba anao uwezo, ni muadilifu, anajua matatizo ya Watanzania na atasimamia maslahi ya umma, tutamchagua, lakini asiende pale kwa kigezo cha kwamba yeye ni kijana, kwa sababu hiyo si miongoni mwa sifa za uongozi na ukitaka uongozi kwa misingi hiyo, utakuwa hutufai,” alisema Sumaye.
Akizungumzia kuhusu nafasi za uongozi kwa vijana, Sumaye alisema kuwa, wapo wanaoshika nyadhifa mbalimbali ikiwamo bungeni, ukuu wa wilaya na hata kwenye vyama, kuna timu ya vijana wengi, hivyo kama wanania ya kubadilisha nchi wanaweza kubadili kwa kupitia nafasi hizo.
“Naamini vijana wengi hawakupewa uongozi serikalini, ukiachilia wale wa nafasi za uwakilishi wa vijana wanaoingia bungeni kwa kufuata sheria ya CCM, lakini kama mkuu wa Wilaya, Rais humteua kwa uwezo na si ujana wake, kwa hiyo suala la ujana au uzee lisitupotezee muda, kwa sababu lina nia ya kutuondoa kwenye ajenda bila sababu.
“Natoa wito kwa Watanzania tusiyumbishwe ili tuweze kumchagua Rais tunayemtaka bila ya kujali sifa za ujana, udini na jinsia, kwani si moja wapo ya sifa zinazotakiwa kwa rais anayetufaa,” alisema Sumaye.
Akifafanua madai kwamba wazee wamekuwa wakiwabana vijana kuchukua nafasi za juu, Sumaye alisema, hilo halina ukweli kwa sababu katika ngazi za Chama Cha Mapinduzi, zipo Jumuiya za Vijana ambazo zinatoa nafasi pana kwa kuwapa uwakilishi.
“Naamini iwapo vijana wanataka kuleta mabadiliko, hakuna wa kuwazuia, kwani tangu nimekuwa ndani ya chama hakuna hoja yoyote ya mabadiliko iliyotolewa na vijana ikapingwa na wazee,” alisema.
Kauli hiyo ya Sumaye, imekuja baada ya hivi karibuni, January kutangaza nia ya kuwania urais huku akitoa wito wa kuwataka wazee kukaa pembeni ili vijana walete mabadiliko chanya ya uongozi.
January alisema kuwa, ameamua kwa asilimia 90 kujitokeza kuwania urais katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 na asilimia zilizobaki zitategemea mambo mengine.
Katika ukurasa wake kwenye mitandao ya kijamii wa Facebook na Twitter, January alisema, uongozi wa kizazi kipya upo tayari kushika hatamu za uongozi na kuijenga Tanzania mpya, fikra mpya na maarifa mapya.
Alisema, mabadiliko yaliyotokea Tanzania, yalidaiwa na kuongozwa na vijana na kwamba, vijana nchini wanaweza kushika usukani wa kuleta mabadiliko wanayoyataka.
“Ukiona kijana anamwambia kijana mwenzake hana uzoefu, basi kazi ya kuleta mabadiliko ni kubwa zaidi na kutokuwa na uzoefu ni sifa ya kijana,” aliandika.
Alisema kuwa, tusi kubwa kwa Rais wa Marekani, Barack Obama mwaka 2008, lilikuwa ni kukosa uzoefu na kukosa rekodi, lakini tusi hilo liligeuka kuwa muziki kwa wapiga kura wa nchi hiyo.
“Tanzania mpya inahitaji viongozi wapya, mazoea mapya, fikra mpya na maarifa mapya. Inahitaji kuthubutu mambo makubwa, siyo kulinda uzoefu wa nyuma,” aliandika January.
Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger