Wizara
ya Nishati na Madini inapenda kutoa ufafanuzi kuhusu kikao cha Waziri
wa Nishati na Madini na Ujumbe wa Benki ya Dunia kilichofanyika tarehe
28.09.2016 kikihusishwa na kupandishwa kwa bei ya umeme kama
ilivyoripotiwa na magazeti ya Mwananchi ya tarehe 12.01.2017 lenye
kichwa cha habari “Prof. Muhongo alivyoshiriki kupandisha bei ya umeme” na la tarehe 13.01.2017 lenye kichwa cha habari “Prof. Muhongo awekwa mtu kati”.
Wizara
inapenda kuutaarifu Umma kuwa, imekuwa ikifanya vikao na wadau
mbalimbali wakiwemo Taasisi za Umma, Binafsi na Washirika wa Maendeleo
yakiwemo Mashirika ya Kifedha ya Kimataifa. Lengo la vikao hivyo ni
pamoja na kuhamasisha uwekezaji katika Sekta za Nishati na Madini
nchini.
Aidha,
tarehe 28/9/2016 Wizara ilifanya kikao na Ujumbe kutoka Benki ya Dunia
ikiwa ni mwendelezo wa vikao vya majadiliano kuhusu upatikanaji wa mkopo
wa Dola za Marekani Milioni 200 kwa ajili ya kuboresha uendeshaji wa
Shirika la Ugavi wa Umeme (TANESCO).
Kikao
hicho pia kilihudhuriwa na taasisi nyingine zikiwemo Wakala wa Nishati
Vijijini (REA), Shirika la Madini la Taifa (STAMICO), Shirika la
Maendeleo la Petroli Tanzania (TPDC), Shirika la Maendeleo ya Taifa
(NDC) na Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (EWURA).
Katika kikao hicho masuala yaliyojadiliwa yalikuwa ni;
1.
Upatikanaji wa umeme wa kutosha, uhakika na bei nafuu kwa ajili ya
kuchochea shughuli za maendeleo ya kukuza uchumi wa nchi ikiwemo
viwanda, biashara, kilimo na huduma za jamii;
2. Kuongeza ufanisi wa utendaji wa Shirika la Umeme (TANESCO); na
3. Kupunguza deni la TANESCO.
Katika
kulipunguza deni la TANESCO ambalo linakaribia Shilingi Bilioni 800
(takriban Dola za Marekani Milioni 363) na kuboresha shughuli za
utendaji za TANESCO, Benki ya Dunia ilijadiliana na Serikali ya Tanzania
kupitia Wizara ya Nishati na Madini ili kupata mkopo wa Dola za
Marekani Milioni 200. Hivyo, katika kikao hicho, hakukuwa na makubaliano
ya kupandisha bei ya Umeme kama ilivyoripotiwa na gazeti hilo.
Vile
vile, tunaomba kuutaarifu Umma kwamba Wizara ya Nishati na Madini kwa
niaba ya Serikali inafanya majadiliano na Benki ya Maendeleo ya Africa
(AfDB), Umoja wa Ulaya (EU), JICA (Japan), na Mashirika mengine ya fedha
kwa lengo la kutafuta fedha za kuboresha Sekta ya Nishati.
Imetolewa na;
WIZARA YA NISHATI NA MADINI
13.01.2017
0 comments:
Post a Comment