WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana,
Ajira na Walemavu, Jenista Mhagama amesema ratiba ya kuhamia Dodoma kwa
mawaziri, manaibu, makatibu wakuu na manaibu iko palepale.
Amesema watakaoshindwa kufanya hivyo, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa
atatoa mwongozo. Jenista alisema jana kuwa baada ya Februari 28, mwaka
huu kutafanyika tathimini na kuangalia utekelezaji wake umefikia wapi,
na kwamba kwa wale ambao hawatatekeleza agizo hilo, Waziri Mkuu Majaliwa
atatoa mwongozo.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa jana, Jenista alisema uamuzi ulitolewa na Rais John Magufuli uko palepale.
Alisema hata Waziri Mkuu amekuwa akisisitiza ratiba ya kuhamia Dodoma
kwa awamu ya kwanza Februari mwaka huu ambayo itahusisha mawaziri,
manaibu mawaziri, makatibu wakuu na manaibu wao na baadhi ya watumishi
wa wizara.
"Kazi yetu itakuwa ni kuangalia utekelezaji utakuwa umefikia wapi na
asiyetekeleza Waziri Mkuu atatoa mwongozo,” alisema Jenista.
Pia alisema amekuwa akikagua nyumba ambazo zinafanyiwa ukarabati kwa
ajili ya watumishi watakaohamia Dodoma ikiwemo nyumba za Mamlaka ya
Ustawishaji Makao Makuu (CDA) eneo la Kikuyu, ambapo ukarabati wake
unaendelea vizuri.
Alisema nyumba hizo za ghorofa, zitawezesha baadhi ya watumishi
kupata nyumba za makazi, ambapo pia taasisi nyingine zinaendelea na
ujenzi wa nyumba za watumishi.
Julai mwaka jana, Rais Magufuli alitangaza kuhusu serikali yake
kuhamia Dodoma kabla ya kumalizika kwa muhula wake wa kwanza wa miaka
mitano, na tayari Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alikwisha kuhamia katika
makao makuu hayo ya nchi yaliyotangazwa mwaka 1973.
Akiahirisha Mkutano wa Nne wa Bunge la 11 mwishoni mwaka jana, Waziri
Mkuu Majaliwa alisema serikali itahamia Dodoma kwa awali, na kueleza
kuwa awamu ya kwanza itakuwa kati ya Septemba 2016 hadi Februari, 2017
ikiwahusisha Waziri Mkuu, mawaziri, makatibu wakuu, manaibu makatibu
wakuu na walau idara mbili za kila wizara.
Alisema awamu ya pili itakuwa Machi 2017 hadi Agosti 2017, ya tatu
Septemba 2017- Feb 2018, ya nne Machi 2018- Agosti 2018, na ya tano
Septemba 2018-Februari 2019; na kwamba awamu hizo zitatumika kwa ajili
ya kuendeleza mchakato wa kuhamisha watumishi hadi wote wawe wamehamia
Dodoma.
0 comments:
Post a Comment