MKAZI wa mtaa wa Mageuzi, kata ya Ngokolo, manispaa ya Shinyanga,
Ibrahimu Daniel (42) amemuua mke wake, kwa kushindwa kuhifadhi vizuri
kachumbari na kupika mboga isiyo na kiwango.
Aidha mauaji hayo yaliyofanyika kwa kumporomoshea kipigo yalifanyika
kwa kuwa alipika chakula kingine wakati kilichobaki mchana kilikuwepo.
Aliyeuawa ni Stella Ibrahimu (39) na alipigwa baada ya mumewe Daniel
kurudi nyumbani na kuuliza kachumbari ambayo alikula jana yake ndipo
mtoto aliyekuwa akimlea Elizabeth Ibrahimu (13) alipomuonesha, lakini
hakuridhika nayo na kuanza kuuliza maswali kwa nini haikuhifadhiwa
vizuri.
Baadhi ya waandishi wa habari waliofika eneo la tukio walielezwa na
mtoto wa marehemu, Daniel Ibrahimu (12) kuwa baba yake alipofika
nyumbani saa moja usiku alimkuta yeye akiwa na Elizabeth ndipo alipoanza
kumhoji Eliza akimuuliza kachumbari yake iko wapi.
Daniel alisema baada ya Eliza kumuonesha baba yake kachumbari hiyo
aliyoila na kuibakisha Jumatatu wiki hii, aliiona imechacha na kuonekana
na uchafu, ndipo alitoka nje na kuchukua fimbo anayoihifadhi juu ya
nyumba na kutaka kuanza kumpiga lakini kabla ya kumpiga mtoto huyo
alichoropoka na kukimbia nje.
Aliendelea kusimulia kuwa baada ya kukimbia na binti huyo, mama yake
ambaye alikuwa kazini alifika nyumbani wakati huo mfarakano ukiendelea
na alimkuta baba yao akifoka na baada ya kuuliza kuna nini, aliambiwa
kwa nini hakupika mboga yenye kiwango na kwa nini alipika ugali mwingine
wakati kulikuwa na ugali uliobaki mchana.
“Mama alifika na kuanza kunywa chai lakini baba aliendelea kufoka
ndipo mama alimjibu kwa hasira ndipo alipomuuliza baba uliacha fedha ya
matumizi ya kuweza kupika mboga yenye kiwango, alianza kumpiga baadaye
alimpiga na kikombe na mateke akaanguka ndipo mimi nilikimbia kwa
majirani kuwataarifu mama anapigwa, walikuja na kukuta mama ameanguka
chini baba akiwa anamruka ruka,” alisema Daniel.
Baadhi ya majirani waliofika katika tukio hilo, Gloria Shija na
Retisia Mashalah, walisema kwa nyakati tofauti kuwa, walikuta baba huyo
amefunga mlango na walipomgongea afungue, alikataa na kusema kuwa kuna
kazi kidogo anaifanya wasubiri, lakini baada ya kuchungulia dirishani
walimuona anampuliza puani na masikioni huku akimmwagia maji ili
azinduke, baada ya kuona hazinduki.
Shija alisema kuwa waliingia ndani na kumkuta akiwa amemkalisha chini
huku akiwa ameinamisha shingo ambapo walimbeba na kumtoa nje,
walijaribu kummwagia maji tena lakini ilishindikana ndipo walichukua
uamuzi wa kumpeleka hospitalini walifika na kuanza kupimwa, lakini
alionekana tayari alishafariki muda mrefu.
Kwa mujibu wa majirani, waliporudi nyumbani, mwanaume huyo alionekana
kumtuma mara kwa mara mwanawe wa kiume na wakaingiwa na hofu na kutoa
taarifa polisi ambapo walifika na kuwachukua watoto wawili; Daniel na
Eliza kwa mahojiano.
Shangazi wa marehemu, Getruda Vitalis alisema ugomvi huo ulikuwa
ukitokea mara kwa mara. Mwenyekiti wa mtaa wa Mageuzi, Emmanuel Sama
alisema yeye alikuwa amelala nyumbani kwake aligongewa mlango na
kuambiwa kuna tukio la mwanamke kupigwa na mume wake na ana hali mbaya
ndipo aliamka na kwenda katika tukio.
Baada ya kuuliza aliambiwa chanzo ni kachumbari iliyobaki jana haikuhifadhiwa vizuri na mtoto waliokuwa wakimlea, Elizabeth.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Elias Mwita, alithibitisha
na kueleza kuwa mtuhumiwa anashikiliwa na Polisi. Alisema uchunguzi wa
awali katika mwili wa marehemu umeonesha kuwa na jeraha katikati ya
kichwa na waliruhusu usafirishwe kesho wilayani Ngara, Kagera kwa
maziko.
0 comments:
Post a Comment