Maiti
ya mtoto Haruna Kyando (9) ambayo ilikutwa nyumbani muda mfupi baada ya
wananchi kutoka makaburini kumzika, imezikwa kwenye makaburi ya Isanga
chini ya ulinzi wa askari wa Jeshi la Polisi nchini, huku waombolezaji
wakiaga mwili huo kwa kufunuliwa jeneza eneo la kichwani makaburini
hapo.
Aidha, Mchungaji wa Kanisa la Bonde la Baraka, ameingizwa lawamani kwa kupotosha umma.
Haruna
aliyekuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa kifafa tangu udogo wake, alikutwa
na wazazi wake Jailo Kyando (36) ambaye ni muosha magari na mkewe, Anna
Elieza (32) akiwa amefia usingizini Jumatatu wiki hii nyumbani kwao Mtaa
wa Igoma A, Kata ya Isanga jijini Mbeya.
Kilichowapa
taharuki wakazi wengi jijini hapa ni baada ya ndugu, jamaa na marafiki
wa familia ya Haruna walipotoka makaburini siku hiyo walikokwenda
kuzika, waliporejea nyumbani waliukuta mwili wa mtoto huyo ukiwa
umelazwa kwenye godoro, pale pale ulipowekwa wakati walipokuwa
wakiuandaa kuuweka kwenye jeneza.
Hatua
hiyo ilizua taharuki kubwa kiasi cha wananchi kutaka kufahamu ni kitu
gani kilichozikwa ndani ya jeneza na ndipo Jeshi la Polisi lilipoingilia
kati, kuzuia kufukuliwa kwa kaburi husika.
Hatua
hiyo ilisababisha vurugu na hatimaye saa tatu za usiku siku hiyo hiyo
ya maziko ya awali, Polisi wakalazimika kutumia mabomu ya machozi,
kutawanya watu waliofurika katika makaburi ya Isanga wakishinikiza
kaburi lifukuliwe.
Lakini
juzi baada ya kukamilishwa kwa taratibu husika, ikiwemo kupatikana kwa
kibali kutoka mahakamani, saa nne na nusu asubuhi, Polisi Mkoa wa Mbeya
walifika eneo la makaburi alipozikwa marehemu na kusimamia shughuli
nzima ya kufukua kaburi hilo.
Shughuli
hiyo iliyodumu kwa muda wa nusu saa kama ilivyokuwa siku ya kwanza,
ilihudhuriwa na mamia ya wakazi jijini hapa waliotaka kujua nini
kilichozikwa ilhali mwili ukiwa umehifadhiwa katika Hospitali ya Rufaa
Kanda ya Mbeya kwa wakati huo.
Nusu
saa baadaye jeneza la mtoto huyo lilitolewa nje ya kaburi na ndipo
Mwenyekiti wa Mtaa wa Igoma A, Fredy Mwaiswelo alipofunua jeneza na
kukuta ndani kukiwa tupu, hali iliyoashiria mwili wa marehemu haukuwekwa
ndani ya jeneza wakati wanakwenda kuzika.
Kutokana
na hali hiyo, Polisi kwa kushirikiana na baadhi ya vijana, walibeba
jeneza hilo na kuelekea nalo katika Kituo cha Polisi kwa ajili ya
uchunguzi zaidi kabla ya kuwakabidhi tena wanandugu mwili ili kuendelea
na taratibu za maziko kwa mara nyingine.
Baada
ya ndugu kukabidhiwa mwili, jeshi hilo pia lilisimamia maziko
yaliyofanyika upya saa 10 jioni katika kaburi lile lile la awali, lakini
tofauti na awali, kabla ya kuzika ulifanyika utaratibu wa ndugu, jamaa
na marafiki waliohudhuria, kuuaga mwili wa marehemu uliokuwa ndani ya
jeneza lililofunuliwa upande wa kichwani.
Kutokana
na mkanganyiko uliojitokeza, baadhi ya ndugu na majirani wa Mtaa wa
Igoma, walisema tukio hilo linaweza kuwa na sura mbili kwa maana ya
hujuma iliyofanywa kwa makusudi, ikilenga maslahi binafsi ya mtu
inayohusishwa na imani za kishirikina au bahati mbaya ya kuusahau mwili
wa marehemu.
Walisema
inaweza kuwa hujuma kutokana na kawaida ya misiba kabla ya maziko,
lazima ndugu watoe heshima za mwisho kwa marehemu, lakini kwa msiba huu
haikufanyika pamoja na baadhi ya ndugu kutohudhuria mazishi.
Akizungumza
nyumbani kwake jana pamoja na kukanusha tuhuma za kuhusisha tukio hilo
na imani za kishirikina, baba wa marehemu alisema mkanganyiko
uliojitokeza wakati taratibu za kuuandaa mwili zikifanyika pamoja na
uzushi uliofanywa na mchungaji, ambaye alisema hamjui kwa jina, ndiyo
vilivyokuza jambo hilo.
Alisema
kama ilivyo kawaida baada ya majirani kupata taarifa za msiba wakiwa
nyumbani hapo, walichanga fedha na kutuma watu kwenda kununua jeneza.
“Wananchi
walichanga hela wakanunua jeneza likaletwa nyumbani. Waliobeba jeneza
walilisukumiza tu kwenye chumba wakatoka, sisi tukaendelea na taratibu
nyingine za mazishi. Baadaye akaja mwenyekiti akasema toeni mwili wa
marehemu nje, wakatoa meza nje wakatuma vijana waende kuchukua mwili wa
marehemu ndani. Waliopeleka jeneza ndani na waliokwenda kulichukua ni
watu wengine. Jeneza likawekwa juu ya meza tukaendelea na mahubiri,” alisema Kyando.
Alisema
baadaye walikwenda kuzika na baada ya kuzika walirudi nyumbani kisha
wakala chakula na kunawa maji, kama ilivyo desturi ya misiba mingi
mkoani hapa.
“Tumenawa
maji tukakaa. Baada ya kukaa kuna mgeni akaingia katika chumba
tunacholala ambapo awali ndipo tulimlaza mtoto kwenye kigodoro,
alipoweka begi akakuta kuna blanketi.
"Alipolifunua
akashtuka akasema kuna nyoka watu wakaanza kukimbia ndani. Baadhi ya
watu wenye roho yenye hasira wakaamua kuingia ndani wakahakikishe kuna
nini,” alisimulia.
“Walipoingia
ndani ndipo wakakuta ni mwili wa mtoto yaani marehemu. Waliposema ni
mtoto wakipaza sauti watu wakajaa ndani. Ndipo waumini wa yule mchungaji
wakaanza kumpigia simu yule mchungaji baadaye akarudi.”
Alisema baada ya mchungaji huyo kufika, aliingia ndani na waumini wake na kuanza kuomba.
“Walipoomba
kwa muda mrefu ndipo mchungaji huyo alipotoka nje na kushika MIC na
kuuambia umati kuwa mtoto baada ya kuombewa amehema mara mbili na ndipo
watu wakaanza kulumbana,” alieleza.
“Kama
siyo mchungaji kuzusha yale wala yasingekuzwa mpaka kwenye mitandao
kiasi hiki. Sisi tunaamini walioagizwa kuchukua mwili walichukua jeneza
tupu pasipo kuwekwa mwili ndani yake na kwa kuwa baada ya kutolewa
jeneza hatukuingia ndani hivyo tuliuacha mwili nyumbani tukaenda kuzika
jeneza peke yake,” alibainisha.
Akizungumzia
suala la imani ya familia hiyo, Kyando alisema awali yeye na familia
yake yenye watoto wawili, walikuwa wakisali katika Kanisa Katoliki,
lakini kutokana na matatizo ya degedege yaliyokuwa yakimsumbua mwanawe
wa kwanza, mkewe aliamua kumpeleka mtoto huyo kwa mchungaji wa Kanisa la
Bonde la Baraka ili aombewe ikiwa ni sehemu ya kuhangaikia afya ya
mtoto.
“Tulikuwa
tunasali Roma, lakini kutokana na matatizo ya mtoto, mama yake akaamua
aanze kusali Kanisa la Bonde la Baraka ili aombewe. Hapo mimi nikaacha
kusali na ndiyo sababu hata katika ibada ya maziko ya mtoto ikabidi
tulishirikishe kanisa walikokuwa wanasali mama na mtoto,” alisema Kyando na kuongeza:
“Watu
wamezungumza maneno mengi sana, siwezi kubisha japo ni ya uzushi ila
wameongea kutokana na walivyosikia, ila ukweli naujua mimi na namwachia
Mungu.”
Naye
baba mkubwa wa marehemu, Saulo Kyando alisema jambo lililotokea
lilikuwa la kawaida na kilichotokea ni kukosekana kwa uratibu makini wa
msiba huo.
“Hili
jambo lilikuwa la kawaida sema kilichokosekana ni mtu ambaye angeliweka
jambo sawa, angekuwepo mtu wa kusimamia kila hatua yasingefikia hapa,” alisema Saulo.
Jeneza baada ya kufukuliwa kutoka kaburini
Mwenyekiti wa Mtaa wa Igoma pamoja na Baba wa Marehemu wakifunua jeneza kuhakikisha kama kulikuwa na mwili wa marehemu
Jeneza lililofukuliwa likiwa halina kitu ndani yake
Vijana wakiwa wanaondoa jeneza makaburini na kulipeleka kituo cha Polisi kwa ajili ya taratibu zingine
0 comments:
Post a Comment