MFANYABIASHARA Robert Mwikwabe, maarufu kama Ndugu, anashikiliwa na
polisi kwa tuhuma za kumpiga risasi ya kichwani na kusababishia kifo
papo hapo mwanafunzi wa kidato cha tatu wa shule ya sekondari Sirari,
Masaite Mrimi(17).
Kutokana na tukio hilo, Mwikwabe ambaye pia ni mmliki Hoteli katika mji
mdogo wa Sirari wilayani Tarime mkoani Mara, alinusurika kuteketezwa
yeye na familia yake Hali hiyo ilitokea baada ya wananchi kuamua kuchoma
moto lori la mfanyabiashara huyo na kwenda nyumbani kutaka kuchoma
hoteli.
Mashuhuda walisema tukio hilo ni la juzi mchana, jirani na nyumba
anayoishi mwanafunzi huyo, eneo la stendi mpya ya mabasi na malori ya
Ngerengere.
Walisema mfanyabiashara huyo alifika akiwa na lori lake likiwa na mawe
na alisimama na kutaka kuchukua pumba za mchele, zilizomwagwa na malori
yanayosafirisha ng’ombe kwenda nchini Kenya.
Eneo hilo ni jirani na nyumbani kwao marehemu, ambako kulitokea mzozo
kati ya Robert na wazazi wa mwanafunzi huyo. Kufuatia mzozo huo,
mwanafunzi huyo aliyekuwa na panga mkononi, alimtishia kumkata Robert,
ambaye alichomoa silaha yake aina ya bastola na kumpiga risasi kichwani
na kumsababisha kifo.
Baada ya tukio hilo, familia ya marehemu na wananchi walianza kumfukuza
Robert aliyeacha lori lake likiwa na mawe na kukimbilia lori lake
lingine la jirani. Kisha alikimbilia Kituo cha Polisi Sirari, kuokoa
maisha yake.
Umati mkubwa wa watu kutoka vijiji vya Ngerengere na Sirari, walikwenda
nyumbani kwa mfanyabiashara huyo kwa lengo la kutaka kuchoma moto hoteli
na nyumba.
Lakini, polisi na Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Glorius Luoga walifanya
juhudi kubwa kuwazuia wananchi hasa vijana, kuacha kuteketeza mali za
mfanyabiashara huyo yakiwemo magari, ambayo sasa yamehifadhiwa kituo cha
polisi kwa ajili ya usalama.
Kamanda wa Polisi Kanda Maalum Tarime-Rorya, Andrew Satta alithibitisha
kutokea kwa kifo cha mwanafunzi huyo na kwamba maiti imehifadhiwa katika
hospitali ya wilaya Tarime.
0 comments:
Post a Comment