Rais
John Magufuli ameendelea kupigilia msumari kwa watanzania na viongozi
wasiopenda kujishughulisha na kuwajibika na kutegemea zaidi fedha za
bure za umma.
Amehakikishia kuwa hali zao zitaendelea kuwa mbaya, isipokuwa kwa wale watakaowajibika na kujishughulisha.
Amesema wale wote wanaolalamika kuwa hawana fedha mfukoni kwa hivi sasa, walizokuwa nazo hazikuwa zao, ndio maana wanalalamika.
Katika hotuba zake mwaka jana katika sehemu mbalimbali nchini, Rais alisema wanaolalamika hawana hela mfukoni ni ‘wapiga dili’.
Rais
alibainisha kuwa Serikali ya Awamu ya Tano, itahakikisha inamaliza hali
mbaya iliyokuwa inalikumba taifa la watanzania, ambapo watu wachache
ndio waliokuwa wakinufaika na fedha za umma huku wananchi wengi
wakiendelea kuumia na umasikini.
Alisema
hayo mkoani Shinyanga jana wakati akizungumza na wananchi kuhusu
maendeleo ya mkoa huo na kumbukumbu ya maadhimisho ya Miaka 53 ya
Mapinduzi ya Zanzibar.
“Nimejitoa
sadaka kwa ajili ya nchi hii, mimi sikuwa na urais ila mmenipa nyie,
sasa nawaahidi mimi na serikali yangu tutawatetea kwa nguvu zote dhidi
ya mafisadi.
"Nasikia kuna watu wanalalamika kuwa eti fedha hamna, kwani zilikuwa zinauzwa sokoni?" alihoji.
Alisema
watu wote wanaolalamika kuwa fedha zimepotea mitaani, ni wale waliokuwa
wamezoea kupata fedha za bure bila kuzitolea jasho.
Aliwahakikishia
kuwa wataendelea hivyo hivyo kutaabika, huku wale waliokuwa
wakijishughulisha wakineemeka. Alisema fedha zilizotumiwa na mafisadi
kipindi cha nyuma ni nyingi mno, kwani kila serikali ikitenga na kutoa
fedha za maendeleo, zimekuwa zikiishia mikononi mwa mafisadi.
“Watu
walikuwa wanajipatia tu fedha bila kuzitolea jasho, unakuta mtu anaenda
nje kila siku, wapo waliofikia kufanyia mikutano ya taasisi zao za
ndani nje ya nchi, mfano pale Muhimbili (hospitali ya taifa) nilipoenda
nilikuta akinamama wanajifungulia chini huku fedha zipo lakini
zimetengwa kwa ajili ya starehe,” alifafanua.
Alisema
wakati serikali yake inaingia madarakani ilikuta nchi ina hali mbaya
hali iliyoilazimu asafishe kila kona ya idara, ndipo walipopatikana
watumishi hewa zaidi ya 18,000, wanafunzi hewa 65,000, mikopo ya elimu
ya juu hewa yenye thamani ya Sh bilioni 3.5.
Alisema hata fedha za Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF), zinazotolewa kwa kaya maskini, zilitolewa kwa kaya hewa 55,000.
Rais
alisema ni wakati sasa Watanzania na serikali kwa ujumla wakashirikiana
kuijenga Tanzania mpya, itakayomkomboa kila mwananchi akiwemo masikini,
kwani kutokana na utajiri ambao Tanzania inayo, imekuwa ikichekwa kwa
kuendelea kuwa masikini.
Utumbuaji majipu
Alisema
pamoja na kwamba wapo baadhi ya watu wanachukizwa na hatua ya utumbuaji
majipu kwa watumishi wasiowajibika, serikali yake itaendelea kuwatumbua
watumishi na viongozi wanaokwenda kinyume na maadili yao.
“Ni
bora nichukiwe na watu wachache kuliko kupendwa na wengi huku mambo
yakienda mrama. Wale wote wanaodai mtindo wangu wa kutumbua ni mbaya
hawa ndio majipu. Kabla ya utumbuaji watanzania walikuwa wanaishi maisha
ya ajabu, na kusisitiza kuwa alikuwa mtumishi wa serikali kwa kipindi
cha miaka 10 anajua anachoongea,” alisisitiza.
Aliomba
Watanzania wamuombee ili aweze kuendeleza jitihada zake za kupambana na
mafisadi kwani serikali yake ya awamu ya tano imejipanga kuendelea
kuongoza kwa ukali kwa faida ya watanzania wote wakiwemo wanyonge na
masikini.
“Lengo
langu ni kuhakikisha wale wote waliokuwa wakila na kuchekelea kipindi
cha nyuma wakati wenzao wanataabika, sasa waishi kama mashetani na wale
waliotaabika waishi kama wafalme,” alisema.
Hatua za maendeleo
Dk
Magufuli alisema kutokana na kutambua adha wanayoipata watanzania
kutokana na huduma mbovu, serikali yake imejitahidi kupambana na
kuboresha maendeleo mengi ikiwemo sekta za elimu, miundombinu usafiri na
afya.
Alitolea
mfano namna serikali hiyo ilivyofanikiwa kukusanya mapato kwa kubana
maeneo yote yenye ubadhirifu na kufanikiwa kuongeza mapato kutoka Sh
bilioni 31 hadi Sh trilioni moja, hali iliyosaidia serikali hiyo kununua
ndege sita, mbili zikiwa tayari zimewasili.
Pia
alisema serikali imefanikisha kusimamia elimu bure kwa kutenga kiasi
cha Sh bilioni 18.77 kila mwezi, zinazokwenda moja kwa moja shuleni kwa
ajili ya kuwezesha wanafunzi kusokma bure katika shule za msingi na
sekondari.
Alisema
pia serikali yake kwa kipindi kifupi, imefanikiwa kuongeza bajeti ya
afya na kufikia Sh trilioni 1.99 na kati ya fedha hizo bajeti ununuzi wa
dawa imeongezeka kutoka Sh bilioni 31 hadi Sh bilioni 250.
Mikakati
Aidha,
kiongozi huyo alisema serikali yake imejipanga kuendelea kuwaletea
maendeleo wananchi, ambapo pamoja na kununua meli mbili katika Ziwa
Victoria na Tanganyika, pia imeanza mchakato wa kujenga reli ya kisasa
ambayo imetengewa jumla ya Sh trilioni moja katika bajeti ya mwaka
2016/17.
Alisema
Tanzania imebarikiwa kuwa na rasilimali za kutosha ikiwemo bahari,
mito, maziwa, madini kama vile dhahabu na wanyama, lakini bado
imeendelea kuwa na umasikini.
Alisema
kutokana na hali hiyo, serikali yake imejipanga kuijenga Tanzania mpya
ikiwemo viwanda ili kuweza kutimiza lengo la kuifanya Tanzania kuwa
miongoni mwa nchi zenye kipato cha kati.
“Hapa
Shinyanga kuna mwekezaji ambaye ana takribani miaka 10 sasa tangu
nikiwa waziri wa mifugo na uvuvi na baadaye ujenzi, hajaendeleza kiwanda
cha nyama, naagiza uongozi wa mkoa wawekezaji kama hawa waondolewe
wapewe wengine tusonge mbele,” alisisitiza.
Pamoja
na mwekezaji huyo, pia alipotembelea mgodi wa Maganzo alipatiwa taarifa
za kuwepo kwa migogoro ya ardhi na kuwataka mawaziri wa ardhi na
mazingira, kushughulikia suala hilo haraka iwezekanavyo.
Maji
Akizungumzia
kero ya maji iliyowasilishwa mbele yake na Mbunge wa Shinyanga Mjini,
Steven Masele, Dk Magufuli alibainisha kuwa atamtuma Waziri wa Maji
kufuatilia bei inayotozwa kwa wakazi hao, ili kuwaondolea mzigo wa
kutozwa bei kubwa ya maji.
Hata
hivyo, Rais huyo aliweka wazi kuwa endapo atabaini bei inayotozwa kwa
wakazi hao, haiendani na bei zinazotozwa katika miji mingine,
atahakikisha ama anaipunguza au kuiongeza ili iendane na miji mingine.
Mapinduzi
Pamoja
na hayo, Dk Magufuli alizungumzia maadhimisho ya siku ya mapinduzi ya
Zanzibar na kubainisha kuwa kuanzia sasa serikali itakuwa inaadhimisha
sikukuu za kitaifa katika mikoa mbalimbali ili kila mtanzania afaidike
na sherehe hizo.
Alisema
yeye na Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohammed Shein walipanga kila mmoja
aadhimishe sherehe hizo katika maeneo tofauti, ambapo Dk Shein alikuwa
visiwani Zanzibar yeye akiwa Shinyanga.
“Watu
wamezoea wakisikia sherehe za kitaifa basi viongozi ni kulundikana
sehemu moja. Sasa hili hatutolifanya, hizi ni sherehe za kitaifa kila
mtanzania ana haki ya kuziadhimisha akiwa na viongozi wa kitaifa”
alisema.
0 comments:
Post a Comment