Tuesday, 10 January 2017

MAPENZI YAZIDI KUCHUKUA ROHO ZA WATU JIJINI MBEYA

...
Katika kile kinachoweza kuelezwa kuwa ni ubaya wa mapenzi, kijana mmoja mkazi wa Mbalizi Mbeya amefariki dunia kutokana na kile kinachodaiwa kuwa ni wivu wa mapenzi baada ya baba wa mpenzi wake kumvamia kijana huyo na kumshambulia.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya DCP Dhahiri Kidavashari amesema kuwa mnamo tarehe 07.01.2017 majira ya saa 03:00 asubuhi katika Kijiji cha Dimbwe kilichopo Kata ya Ulembo, Wilaya ya Kipolilsi Mbalizi, Mkoa wa Mbeya, mtu mmoja aliyefahamika kwa jina la VARENCY POSTA mkazi wa kijiji cha Dimbwe alifariki dunia akiwa anapatiwa matibabu katika kituo cha afya Ilembo baada ya kuchomwa kitu chenye ncha kali kichwani na mtu aliyefahamika kwa jina la MISIS EDWARD mkazi wa Dimbwe.

Inadaiwa kuwa chanzo cha mauaji hayo ni wivu wa mapenzi kutokana na binti wa mtuhumiwa kuwa na mahusiano ya kimapenzi na marehemu.

Inadaiwa kuwa mtuhumiwa kabla ya kutenda kosa hilo alimvizia njiani marehemu akiwa anatoka kuangalia mpira na kisha kumchoma kitu chenye ncha kali hali iliyosababisha kutokwa damu nyingi na kupelekea kifo chake akiwa anapatiwa matibabu.

Kidavashari amesema mtuhumiwa amekamatwa na mwili wa marehemu umefanyiwa uchunguzi na kukabidhiwa ndugu kwa taratibu za mazishi.

Katika matukio mengine, Kamanda Kidavashari ametoa taarifa nyingine za mauaji ambapo watu wawili wanaosadikiwa kuwa majambazi waliuawa na wananchi walioamua kujichukulia sheria mkononi baada ya kuvamia eneo la wachimbaji wadogo wa dhahabu wakiwa na silaha aina ya Short gun iliyotengenezwa kienyeji kwa lengo la kufanya unyang’anyi na ndipo walizidiwa nguvu na wananchi hao.

Pia amesema mtu mmoja aliyefahamika kwa jina la NURU ROMAN MWANG’OLELA Mkazi wa Ubaruku Wilaya ya Mbarali na mwenyeji wa Bujela Kisale Wilaya ya Kyela aliuawa kwa kupigwa mawe sehemu mbalimbali za mwili wake na kundi la watu waliojichukulia sheria mkononi kwa tuhuma za wizi.
Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger