Baada
ya kimya kirefu, hatimaye Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar
(ZEC), Jecha Salum Jecha amefunguka na kuelezea kuwa uamuzi aliouchukua
wa kufuta uchaguzi wa Zanzibar wa mwaka 2015 baada ya kubainika kuwa na
dosari, ulifanyika kwa kufuata taratibu, kanuni, Sheria na Katiba ya
Zanzibar.
Jecha
aliyasema hayo wakati akihojiwa na kipindi cha Funguka, kinachorushwa
na Kituo cha Televisheni ya Azam na kusisitiza kuwa, hana wasiwasi wala
hofu yoyote kwa hatua hiyo, aliyoichukua ya kufuta uchaguzi kwa kuwa
ilifuata misingi yote ya Sheria na Katiba.
Pamoja
na kwamba alikataa kujibu kwa undani kuhusu hatua yake hiyo na
kusisitiza kuwa mengi atayabainisha kwenye taarifa ya tume, alisisitiza
kuwa hakuwahi kutumika na chama chochote wala kuwasiliana na Rais Ali
Mohammed Shein kama inavyodhaniwa na wengi.
“Haya
yote yataonekana kwenye taarifa ya uchaguzi, siwezi kuongea hapa sasa
ila kiukweli utaratibu ulifuatwa. Matokeo yalifutwa kutokana na dosari
zilizojitokeza ikiwemo baadhi ya matokeo kujulikana kabla na kusababisha
baadhi ya vyama kulalamika,” alisisitiza Jecha.
Alieleza
kuwa matatizo na dosari za uchaguzi huo, yalianza kujitokea katika
kipindi cha kupokea matokeo ambapo matokeo yalitoka katika maeneo ya
Unguja, hayakubainika kuwa na matatizo, isipokuwa kwa matokeo yalitoka
katika maeneo ya Pemba.
Alisema
katika kura hizo za Pemba, ilibainika kuwa utaratibu wa kiufundi
ulifanyika kuharibu matokeo ya hesabu za kura baada ya kufanyika
urekebishaji wa kasoro wa mambo, ambayo hayakutakiwa yafanywe nje ya
sheria za uchaguzi.
Alisema
baada ya kutokea kwa dosari hizo, kwa upande wa tume kupitia yeye,
iliamua kufuta uchaguzi mzima ili kuepusha vurugu na mgongano wa kisiasa
huku Polisi ikifanya uchunguzi kuwabaini wahusika waliosababisha dosari
hizo katika matokeo ya uchaguzi.
Kuhusu
kushirikisha wajumbe wengine wa tume katika kufanya maamuzi ya kuufuta
uchaguzi, Jecha alibainisha kuwa tume nzima ya ZEC ilihusika katika
kufutwa kwa uchaguzi huo na ndio maana baada ya kufutwa taratibu za
uchaguzi mwingine zilitekelezwa vyema na tume hiyo.
Hata
hivyo, alibainisha kuwa katika kutangaza uamuzi wa kufuta uchaguzi huo,
alilazimika kufanya hivyo binafsi baada ya kuona hali ya matokeo hayo
inazidi kuwa mbaya na kwenda kinyume cha taratibu za uchaguzi.
Alibainisha
kuwa baada ya kufuta uchaguzi huo, ili kuleta usawa kwa vyama vyote,
tume hiyo ilisubiria vikao vya kutafuta mustakabali wa kisiasa visiwani
humo vilivyokuwa vikifanyika baina ya viongozi wa kisiasa wa vyama vyote
ndipo itangaze tarehe ya uchaguzi mpya.
“Tulikaa
kimya kwa takribani mwezi mmoja tukisubiri hatua zichukuliwe na
viongozi kupitia hivyo vikao vyao. Tulisubiri katika ule muda bila
kuvunja sheria, na baada ya kuona hakuna hatua zinachokuliwa dhidi ya
maamuzi yetu tulitangaza tarehe ya uchaguzi,” alieleza Jecha.
Mwenyekiti huyo alikanusha madai kuwa ametumika kufuta uchaguzi huo kwa maslahi ya CCM na Dk Shein. “Hapana,
Sijawahi hata mara moja kuitwa au kutafutwa na kiongozi yeyote wa
serikali, wala Rais sijawahi kuwasiliana na hata namba yake sina,” alifafanua.
Alisema
ingawa hajawahi kukutana na mtu yeyote anayemlaumu kuhusu uamuzi wa
tume hiyo wa kufuta uchaguzi, endapo kuna mtu bado ana malalamiko,
anaruhusiwa kuiandikia ZEC malalamiko yake na si yeye binafsi,
yatafanyiwa kazi.
Pamoja
na hayo, mwenyekiti huyo alisisitiza kuwa hata baada ya kuufuta
uchaguzi huo, kwa kuwa anaamini alifuata taratibu na sheria zote,
hakujificha wala kuogopa kitu, kwani aliendelea na shughuli zake kama
kawaida.
“Hadithi
zilikuwa nyingi, kila mmoja alifikiri alivyotaka yeye, mie nilikuwepo
Zanzibar natembea, lakini si kila mtu alikuwa ananiona. Redio za kijamii
kila moja ilikuwa inazungumza vyake, mwenyekiti yuko hivi, mwenyekiti
yuko wapi, mwenyekiti kesho ananyongwa mara nimepelekwa mahakama za
kimataifa yote hayo yalizungumzwa lakini mie nipo,” alisema.
0 comments:
Post a Comment