Mamlaka
ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imetoa tahadhari kwa watumiaji wa huduma
za mawasiliano juu ya utapeli unaofanywa kwa kutumia simu za mkononi.
Akizungumza
na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Kaimu Meneja wa
Mawasiliano kwa Umma wa TCRA, Semu Mwakyanjala alisema kumekuwa na
ongezeko la matapeli wanaoghushi utaratibu wa mawasiliano na kuwalaghai
watu kutuma pesa kwa simu za mkononi.
Mwakyanyala
alisema kumekuwa na ongezeko kubwa la matumizi ya huduma za kifedha na
kwa miezi miwili iliyopita ya Novemba na Desemba, 2016 kwa wastani kiasi
cha jumla ya fedha iliyopita katika mitandao ya kampuni zinazotoa
huduma za kifedha kwa njia ya simu za mikononi ni Sh trilioni 13.07.
Aliongeza
kuwa ni vyema wananchi wakazingatia mambo mbalimbali kabla ya kutuma
fedha, ikiwemo kutokutekeleza maagizo yoyote yanayohusu fedha kwa
mawasiliano ya simu hata kama yanatoka kwenye namba ya mtu anayemfahamu
badala yake ampigie aliyemtumia ujumbe kwa namba nyingine kufanya
uhakiki.
Pia
aliwataka wananchi pale wanapopokea taarifa kwa njia ya simu au ujumbe
mfupi wa maandishi kuwa ametumiwa fedha kwa makosa na kufuatiwa na
kutumiwa ujumbe mfupi unaofanana na ujumbe unaotumwa na watoa huduma na
kutakiwa kurudisha fedha hizo, asifanye haraka badala yake wachukue
tahadhari zote kujiridhisha na uhalali wa taarifa hiyo.
“Omba
taarifa fupi ya akaunti yako kwa mtoa huduma uhakiki miamala yako na
salio lako ikibidi wasiliana na kituo cha huduma kwa wateja cha mtoa
huduma wako kwa kuwa kumekuwepo na uhalifu wa kulaghai watoa huduma za
mawasiliano kwa kutumia ujumbe mfupi unaokaribia kufanana na ujumbe
unaotumwa na watoa huduma,” alieleza.
0 comments:
Post a Comment