Serikali imesema ipo kwenye mchakato wa kuajiri walimu 4000 wa masomo ya Sayansi na Hisabati.
Kauli hiyo imetolewa leo Jijini Dar es Salaam na Waziri
Mkuu Kassim Majaliwa wakati akiwa katika ziara yake ya kutembela wilaya
mpya za jiji hilo, akianzia na Kigamboni siku ya leo.
Majaliwa amesema mchakato wa ajira hizo unaendelea chini ya
Ofisi ya Rais Utumishi, na muda wowote kutoka sasa mchakato huo
utakapokamilika, majina yatatolewa na walimu hao kuajiriwa.
Kuhusu walimu wa masomo mengine, Waziri Mkuu amesema walimu
wa masomo mengine hususani ya sanaa wapo wa kutosha na kwamba wanapaswa
kusubiri kwakuwa wao wako wengi zaidi na hakuna uhaba na uhitaji wa
walimu hao wa masomo ya sanaa.
Hivi karibuni, Wizara ya Elimu iliwataka wahitimu wa ualimu
katika masomo ya sayansi na hisabati kutuma taarifa (CV) zao ili
izihakiki kabla ya ajira, mchakato ambao tayari umekamilika na majina
yalitumwa katika wizara ya utumishi.
Naibu Waziri wa Elimu, Mhandisi Stella Manyanya wiki mbili
zilizopita wakati akiongea na kituo cha EATV alisema kuwa kazi ya wizara
yake ilikuwa ni kuhakiki taarifa za wahitimu hao, na si kuajiri, huku
akibainisha kuwa zoezi hilo limekamilika na majina yako utumishi ambao
ndiyo watahusika na kuajiri.
Pia alisisitiza kuwa kama wizara ya elimu waliomba kupewa
walimu wa masomo ya Sayansi na Hisabati haraka kwa kuwa uhitaji wao ni
mkubwa zaidi na kuwataka wahitimu wote waliotuma taarifa zao, wasubiri
watapata majibu muda si mrefu.
Chanzo: mpekuzi huru
0 comments:
Post a Comment