WAZIRI
Mkuu, Kassim Majaliwa amemkabidhi hati ya shamba la mifugo la Manyara,
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Monduli, Stephen Ulaya baada ya
kubadilisha umiliki wa shamba hilo.
Umiliki
ulibadilishwa kutoka Taasisi ya Tanzania Land Conservation Trust (TLCT)
ambayo mwenyekiti wa bodi yake ni Mbunge wa zamani wa Monduli, Edward
Lowassa kwenda kwa wananchi wa vijiji viwili vya Elesilalei na Ortukai
vya kata ya Elesilalei, eneo la Makuyuni, wilayani hapa.
Hatua
ya kubadilishwa umiliki wa shamba hilo kwenda kwa wananchi ni baada ya
kilio cha muda mrefu kwa wananchi hao kudai kuwa Rais wa Awamu ya Tatu,
Benjamin Mkapa, aliagiza shamba hilo ligawiwe kwa wananchi lakini
haikuwa hivyo, badala yake watu wachache walijimilikisha kinyemela chini
ya wenyekiti wa bodi ya TLCT.
Majaliwa
alitangaza kukabidhiwa hati hiyo wakati alipomtembelea mwanzilishi wa
Shule ya Msingi Laibon, Leshuko ole Mapii, kata ya Elesilalei.
Alifika
kujionea hali halisi ya mwamko wa elimu kwa mzee huyo ambaye wajukuu
zake na watoto wake zaidi ya 102 wanasoma shuleni hapo pamoja na watoto
wengine wanaotoka jirani na eneo hilo.
Alisema
serikali imeamua kurudisha shamba hilo kwa wananchi wa vijiji hivyo
viwili baada ya Baraza la Madiwani na uongozi wa wilaya hiyo ya Monduli
kuridhia kwa pamoja umiliki wa shamba hilo kurudi kwa wananchi.
Alisema
shamba hilo lenye ukubwa wa ekari 44,930 lilikuwa likimilikiwa na TLCT
linalofadhiliwa na Shirika la African Wildlife (AWF), hivi sasa ni mali
ya wananchi na halmashauri ya Monduli ndio wataamua kupanga matumizi
bora ya ardhi.
Alisema
nyaraka zinazoonesha kuwa shamba hilo lililotolewa kwa wananchi wa
vijiji vya Elesilalei na Ortukai na Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu mwaka
1999 kwa ajili ya kilimo na ufugaji lakini hakuna kilimo chochote hapo
na badala yake TLCT ikajimilikisha shamba hilo kinyume na maagizo.
"Sasa
namkabidhi Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Monduli hati hii na
kuanzia leo(jana) umiliki wa shamba hilo utakuwa chini ya halmashauri na
wananchi mtaamua kupanga matumizi bora ya ardhi katika shamba hili
mliloteseka nalo kwa muda mrefu," alisema.
Alisema
serikali itawanyang'anya mashamba wale wote wanaomiliki bila ya
kuyaendeleza kwa kuwapa wananchi na kuhoji ni kwa nini wenye fedha
kuchukua mashamba mkubwa bila ya kuyaendeleza.
Awali
Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo kabla ya ujio wa Waziri Mkuu,
alifanya ziara katika shamba hilo na kuagiza uongozi wa wilaya ya
Monduli, mkoani Arusha na baraza la madiwani la wilaya hiyo kuhakikisha
wanabadilisha umiliki wa shamba hilo kwenda kwa wananchi wa vijiji
husika kama Rais mstaafu, Benjamini Mkapa, alivyoagiza.
Mbunge
wa Monduli, Julius Kalanga (Chadema) pamoja na Mwenyekiti wa
Halmashauri hiyo, Isack Joseph kwa nyakati tofauti waliishukuru serikali
kwa uamuzi huo na kuipongeza serikali kwa kujali maslahi ya wananchi
wake.
Mkurugenzi
wa TLCT, Boniface Ngimojiro alipopewa nafasi ya kusema neno kwa
wananchi hao, alisema taasisi hiyo inaongozwa na bodi ya wadhamini yenye
wajumbe wanane wakiongozwa na Mbunge wa zamani wa Monduli, Edward
Lowassa kama mwenyekiti wa bodi hiyo.
Aidha
alikiri kupata amri ya kubadilishwa umiliki wa shamba hilo kutoka
katika taasisi hiyo kwenda kwa wananchi wa vijiji hivyo viwili na
kusisitiza kuwa kwa sasa ameridhia shamba hilo kumilikiwa na wananchi.
Meneja
wa AWF, Fidelis Ole Kashe, alisema wamekuwa wakifanya kazi katika
mazingira magumu ndani ya shamba hilo pamoja na kufadhili miradi
mbalimbali ya maendeleo kwenye shamba hilo ikiwemo shule, zahanati,
ufugaji wa kisasa na machinjio.
Waziri
wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe, aliwasihi wananchi
hao kuheshimu njia za mapito ya wanyama katika eneo hilo ambalo
wanyamapori kutoka hifadhi za Tarangire, Manyara na Ngorongoro
wanalitumia kwa ajili ya kupita kwenye hifadhi hizo mara kwa mara.
0 comments:
Post a Comment