BODI
ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) imesema kuanzia mwanzoni
mwa Januari mwakani, itaanza kuchapisha majina na picha za wadaiwa sugu
kwenye vyombo vya habari waliohitimu katika vyuo mbalimbali vya elimu
ya juu kuanzia wale wa miaka 10 iliyopita.
Bodi
hiyo ilitoa muda wa zaidi ya siku 30 unaoisha kesho Desemba 30, mwaka
huu, kwa wadaiwa hao sugu kulipa madeni yao ndani ya muda huo,
vinginevyo hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yao, ikiwemo kulazimika
kulipia gharama za kuwasaka na kuendesha kesi.
Pamoja
na hayo, bodi hiyo pia kupitia Sheria ya Bodi ya Mikopo iliyofanyiwa
marekebisho hivi karibuni na Bunge, imeanza mkakati wa kuwabana waajiri
wasiotimiza wajibu wao kisheria kwa kuunda kikosi kazi cha kuhakiki
waajiriwa wasiowasilisha makato na majina ya waajiriwa waliokopa HESLB,
na adhabu yao itakuwa ni faini au kifungo cha miezi 36 jela.
Akizungumza
na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Mkurugenzi Mtendaji wa bodi
hiyo, Abdul-Razaq Badru, alisema baada ya kuisha kwa muda huo wa siku 30
walioutoa, wadaiwa wote sugu, ambao mpaka sasa hawajajisalimisha
wenyewe kwa hiari, kulipa madeni yao wataanikwa hadharani na picha zao.
“Tumeamua
kuchukua hatua hii ambayo tunaamini itasaidia watu kuwatambua wadaiwa
hawa wa bodi, na kuturahisishia kupata taarifa zao na kuwasaka ili
waturejeshee fedha zetu,” alisema Badru.
Aidha,
alisema nia ya kuchapisha majina na picha za wadaiwa hao ni kuutangazia
na kuutarifu umma juu ya watu wanaokwamisha wanafunzi wengine kukosa
fursa ya kupata mikopo ya elimu ya juu kwa kuwa fedha iliyopo bado
haitoshelezi.
Alisema
bodi hiyo ilitoa muda wa wiki nne kwa wadaiwa hao sugu na baadaye
kuwaongezea tena muda wa wiki mbili, unaoishia Desemba 30, mwaka huu,
hivyo kinachofuata ni utekelezaji kwa wale walioshindwa kuitumia fursa
hiyo ya kujisalimisha.
Mkurugenzi
huyo alisema baada ya muda huo kwisha na bodi hiyo kuanza kuchapisha
majina na picha za wadaiwa hao, wale watakaopatikana kwa kushindwa
kulipa madeni yao, watachukuliwa hatua za kisheria ikiwa ni pamoja na
kulipia gharama za usumbufu wa kuwatafuta.
Alisema
utaratibu wa kukopesha ni mfumo unaowezesha wanafunzi wengi zaidi,
kupata fursa ya kuendelea na masomo yao ya elimu ya juu, hivyo ni vyema
wanafunzi wote wanaopata fursa ya kukopa wahakikishe wanalipa kwa muda
muafaka uliowekwa kisheria.
Badru
alisema kwa mujibu wa marekebisho ya sheria hiyo ya Bodi ya Mikopo,
imewaongezea muda wa kuanza kulipa wanafunzi walionufaika na mikopo
kutoka miezi sita hadi miaka miwili ili kutoa fursa ya kujipanga na
kutafuta ajira.
Aidha,
alibainisha kuwa sheria hiyo pia imeongeza kiwango cha makato kwa
waajiriwa walionufaika na mikopo ya HESLB kutoka asilimia nane ya
mishahara yao hadi asilimia 15.
“Tunawashukuru
sana wadau kwa kuwezesha kutoa maoni yao yenye tija kwenye sheria hii
katika eneo hili sisi tulipendekeza kiwango cha makato kifikie hadi
asilimia 30 na zaidi, lakini kupitia maoni mbalimbali ya wadau wakiwemo
wa wabunge walipendekeza kiwango kiwe asilimia 15 tu,” alisema.
Alisema
ili kuweza kutimiza lengo la kuhakikisha kila mnufaika na mikopo hiyo
aliyeajiriwa analipa deni lake, pamoja na kuwabana wadaiwa, bodi hiyo
imeanza mkakati wa kuwabana waajiri wasiotimiza wajibu wao kisheria
kupitia marekebisho hayo ya sheria.
“Tumeunda
kikosi kazi kinachojumuisha timu ya wataalamu kutoka sehemu mbalimbali
nyeti, kitakachoanza kufanya kazi kuanzia Januari 2, mwaka huu, ya
kuhakiki kila ofisi ya waajiri sugu ili kubaini kama ama wamewasilisha
majina ya wanufaika wa mikopo hii au wanawakata bila kuwasilisha
michango hiyo kwa bodi,” alisema.
Alisema
waajiri watakaobainika kwenda kinyume na sheria hiyo kwa kutoisaidia
bodi kupata waajiriwa wanaodaiwa au kutowasilisha makato yao,
wataadhibiwa kwa mujibu wa sheria kwa kulipa faini isiyopungua makato
hayo waliyoshindwa kuyawasilisha na endapo watashindwa watakabiliwa na
adhabu ya kifungo cha muda wa miezi 36 jela.
“Lakini
pia sheria hii imewawajibisha wale waliokopa kuhakikisha wanapeleka
wenyewe taarifa zao kwa bodi ili waweze kuwekewa utaratibu wa makato,
yeyote atakayebainika kutowasilisha taarifa zake naye atawajibishwa,” alisisitiza.
Halikadhalika,
Badru alisema marekebisho hayo ya sheria, pia yamegusa wanufaika wa
mikopo hiyo ya elimu ya juu, ambao hawako kwenye mfumo rasmi wa ajira,
ambao nao wanatakiwa kurejesha kiasi kisichopungua Sh 100,000 kila
mwezi.
Akizungumzia
mafanikio tangu bodi hiyo itoe muda wa hiari kwa wadaiwa sugu kulipa
wenyewe madeni yao, Mkurugenzi huyo alisema makusanyo ya fedha,
yameongezeka kutoka Sh bilioni mbili mpaka nne kwa mwezi hadi Sh bilioni
nane.
Alisema
tangu muda huo utolewe jumla ya wanufaika 42,700 wamejitokeza wenyewe
kwa hiari na kulipa madeni yao huku wengine wakilipa deni lote na
wengine wakiyapunguza.
Hadi
sasa bodi hiyo ya mikopo ina jumla ya Sh bilioni 300 zilizoiva,
inazozidai kwa wadaiwa hao sugu na kati ya fedha hizo ni Sh bilioni 140
pekee ndio zimelipwa.
Kwa
mujibu wa HESLB kuanzia Juni, mwaka huu, jumla ya wanafunzi 379,179
wamenufaika na mikopo ya elimu ya juu inayotolewa na bodi hiyo tangu
ianzishwe Juni, mwaka 1994 na jumla ya Sh trilioni 2.6 zimeshatolewa kwa
wanafunzi hao.
Jumla
ya wahitimu wa elimu ya juu wa zamani 238,430 walionufaika na mikopo ya
HESLB, wanatakiwa kuanza kulipa madeni yao, ambayo ni kiasi cha Sh
trilioni 1.4, baada ya muda waliotakiwa kulipa kwa mujibu wa sheria
kuisha.
0 comments:
Post a Comment