Mwandishi
wa kujitegemea wa kituo cha televisheni cha ITV, Halfani Lihundi
ameachiwa kwa dhamana kutoka katika kituo cha Polisi cha Changamoto, Usa
River wilayani Arumeru mkoani Arusha alikokuwa anashikiliwa tangu juzi,
na kutakiwa kuripoti kituoni hapo Desemba 27, mwaka huu.
Alikuwa
anashikiliwa kwa amri ya Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Alexander Mnyeti,
baada ya kuripoti habari inayoelezwa na mkuu huyo wa wilaya kuwa haikuwa
sawa na kuamuru kukamatwa kisha, kulala mahabusu na hatimaye kufanikiwa
kutoka jana saa tisa alasiri.
Awali,
waandishi wa habari wa Arusha walikusanyika kituoni hapo ili kujua
hatma ya mwenzao na baadaye kuamua kwenda kumuona Waziri wa Ardhi,
Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi ili kumweleza kuwa mwenzao
amekamatwa kwa sababu ya migogoro ya wananchi.
Wakati
Lukuvi anatoka kwenye kikao cha kujadili migogoro ya ardhi
kilichofanyika ukumbi wa Mkuu wa Mkoa wa Arusha, waandishi waliimba
wimbo wenye lengo la kufikisha ujumbe kuwa, wanataka wenzao aachiwe
huru. Waliimba; “Solidarity Forever, Bring Back Halfani Lihundi.”
Lukuvi
alisema hahusiki na suala hilo na kuwasihi wanahabari kwenda naye Usa
River kwenye mkutano ambapo Mnyeti atatoa tamko juu ya suala hilo.
Lakini
Mnyeti alipokuwa akitoka kikaoni hapo aliulizwa na waandishi kuhusu
suala hilo na kosa lipi limefanya Lihundi kushikiliwa Polisi, lakini
hakuzungumza chochote na kuelekea kwenye gari lake kusubiri msafara wa
Lukuvi.
Awali,
ilidaiwa kuwa Mnyeti ndiye aliyeamuru Lihundi akamatwe kwa madai ya
kuandika habari za uchochezi za kijiji cha Leguruki, Arumeru.
Alisema
alipotaka kujua kosa analoshitakiwa nalo Lihundi, alijibiwa hana kosa
ila yupo kwa amri ya Mkuu wa Wilaya. Hata hivyo, RB ya Polisi Usa River
4763/2016 inaonesha ana kosa la uchochezi.
0 comments:
Post a Comment