CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimesema hadi sasa hakijui alipo msaidizi wa Mwenyekiti wa chama hicho, Ben Saanane.
Kimevitaka vyombo vya dola, kuchukua hatua za haraka kuhakikisha msaidizi huyo anapatikana haraka.
Saanane
inadaiwa alitoweka katika mazingira ya kutatanisha tangu Novemba 18,
mwaka huu. Juhudi za kumtafuta katika vituo vya polisi, hospitalini na
vyumba vya kuhifadhia maiti, zimefanyika bila mafanikio.
Kauli
hiyo imetolewa na Mwanasheria Mkuu wa chama hicho, Tundu Lissu wakati
akizungumza na waandishi wa habari kuhusu Saanane ambaye hajulikani
aliko.
Alisema hata wao hawajui alipo, hawafahamu kama yuko hai au ameshikiliwa mahali. Kwamba wanachokijua ni kwamba hawajui aliko.
“Katika
mazingira haya, tunaiomba serikali na vyombo vyake vya ulinzi, ituambie
kama imemkamata na inamshikilia Ben Saanane tuanzie hapo…lakini kama
hawajamkamata na hawamshikilii, serikali na vyombo vyake watueleze
mawasiliano yake ya mwisho yalikuwa lini, na nani, wapi na yalihusu
nini,” alisema.
Alisema
kwa kuwa serikali ndiyo yenye udhibiti wa mipaka yote nchini, iwaeleze
kama kuna rekodi yoyote inayoonesha Ben aliondoka nchini kwa kupitia
mipaka hiyo, kama ni mipaka ya nchi kavu, majini au viwanja vya ndege.
Katika
hatua nyingine, alisema pamoja na majibu hayo, lakini pia wanaitaka
serikali pamoja na vyombo vyake vya dola, kufukua miili ya watu
waliokufa katika mto Ruvu na ifanyiwe uchunguzi ili wajulikane watu hao
ni akina nani, ili isije kuwa miongoni mwa watu hao ni Saanane.
Lissu
alisema kuwa mawasiliano ya mwisho kati ya Saanane na Mbowe, yalikuwa
ni Novemba 14, mwaka huu wakati Saanane akiwa Dar es Salaam na
mwenyekiti huyo akiwa Dodoma.
“Alimwambia
mwenyekiti uko wapi, akamwambia nakwenda kwenye maziko ya Samuel Sitta,
mawasiliano ya mwisho ni ya tarehe 14 Novemba,” alisema Lissu.
Alisema
pamoja na kwamba Saanane alikuwa ni msaidizi wa Mbowe katika masuala ya
kisiasa na kijamii, lakini hakuwa akitembea na mwenyekiti huyo na
kwamba shughuli zake alikuwa akifanyia katika Makao Makuu ya chama
hicho.
Lissu
alisema kuwa wapo watu wanahoji inawezekanaje Mwenyekiti hajui mahali
alipo msaidizi wake, lakini wanapaswa kufahamu kuwa Mbowe hakuwa
akitembea na Saanane.
Alisema
baada ya maziko ya Sitta, viongozi wote wa chama hicho walikuwa
wakizunguka katika mikoa mbalimbali kwa ajili ya kufanya shughuli za
chama, lakini katika kipindi chote hicho, mwenyekiti huyo hakuwa na
msaidizi wake huyo, kwa kuwa hatembei naye na si jambo la ajabu.
“Baada
ya hizi ziara, tulienda nchi za nje…katika kipindi chote hiki
Mwenyekiti hakuwa na Ben na vilevile nataka niweke hii vizuri,
Mwenyekiti hakupata wasaa wa kusema Ben yuko wapi, kwa sababu hatembei
naye, hayuko naye muda wote.”
“Sasa
kuna watu wanaosema Mwenyekiti ndiye anayejua, atuambie yuko wapi,
Mwenyekiti hajui, mimi sifahamu aliko Ben, tungekuwa tunafahamu
tungeshasema,” alisema.
Alisema
kwa mara ya kwanza alipigiwa simu na mdogo wake Ben, aliyemtaja kwa
jina la Dorice Desemba 4, lakini hakumpata na alimtumia ujumbe kumwambia
kuwa kaka yao Ben amepotea, hawajui aliko na alikuwa akitaka ushauri
ambapo alimjibu waliripoti jambo hilo polisi na kwenye vyombo vya
habari.
Alisema si kwamba wamenyamaza kimya, kwa kuwa wanajua alipo msaidizi huyo na kwamba watu wanaodai hivyo si sahihi.
Alitaka
mtu yeyote mwenye taarifa kuhusu Saanane alipo, azitoe taarifa hizo
hadharani, polisi, kwenye chama, vyombo vya habari au kwa ndugu zake.
0 comments:
Post a Comment