WAZIRI
wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako,
ametoa masharti mapya ya ajira za ualimu nchini, huku akisema Serikali
haitaajiri walimu wa masomo ya sanaa (arts) kwa kuwa wapo wa kutosha.
Akizungumza
mjini Dodoma jana wakati akifungua mkutano mkuu wa mwaka wa Wakuu wa
Shule za Sekondari Tanzania (TAHOSSA), Profesa Ndalichako, alisema
Serikali kwa sasa haiwezi kuajiri walimu wa masomo hayo kwa kuwa inataka
kuajiri walimu wa masomo ya sayansi na hisabati ambao idadi yao ni
ndogo.
“Pamoja
na uamuzi huo mpya, ajira za walimu wapya wa masomo ya sayansi nazo
zimebadilika kwani wale wote waliohitimu ualimu wa sayansi na hisabati,
wanatakiwa watume vyeti vyao kabla ya kupangiwa kituo cha kazi.
“Kuhusu
wale walimu wa ‘arts’, kule tuna walimu wa ziada ambao tutajaribu
kuwapanga kutokana na shule, kwani wengi walikuwa wamepangwa shule moja.
Kwahiyo, tutaangalia utaratibu wa kuwapanga kulingana na mahitaji,’’ alisema Profesa Ndalichako.
Akizungumzia
suala la ubora wa elimu nchini, Profesa Ndalichako aliwataka walimu
wakuu hao kuhakikisha wanasimamia ubora wa elimu kwa kuwa wao ndio
wanaowaandaa wanafunzi kabla hawajaenda vyuoni.
“Vilevile
pelekeni takwimu sahihi za wanafunzi waliopo katika shule zenu
kuisaidia Serikali katika kupanga bajeti ili iweze kutoa fedha sahihi.
“Hapa
kuna kimbembe, yaani wakati mwingine huwa najifanya nimepoteza takwimu
ya shule fulani, nikiziomba na kutumiwa, zinakuwa ni tofauti na zile za
mwanzo.
“Hili nawaomba mkalisimamie ili iwe rahisi kwetu kupanga bajeti yenye tija,’’ alisema.
Kuhusu
ujenzi wa maabara katika shule za sekondari, waziri huyo alisema kwamba
kutokana na nyingi kukamilika, Serikali itatoa vifaa vya maabara
kuanzia Januari mwakani baada ya kuwa vimeingia nchini kutoka
vilikoagizwa.
Awali,
akisoma risala ya walimu hao, Rais wa TAHOSSA, Bonus Nyimbo, aliiomba
Serikali itoe waraka wa kupiga marufuku matumizi ya simu kwa wanafunzi
shuleni kwa kuwa zimekuwa zikichangia kushuka kwa ufaulu kwa baadhi ya
wanafunzi.
“Ili
kuboresha elimu, tunaiomba Serikali itoe waraka wa kupiga marufuku
matumizi ya simu kwa wanafunzi kwani simu nyingi tunazozikamata tunakuta
mule hakuna taaluma,’’ alisema Nyimbo.
Kwa
upande wake, Mkurugenzi wa Global Education Link, Abdulmalik Molel,
ambaye pia kampuni yake ilipewa tuzo ya heshima katika kuendeleza elimu
nchini, alisema ni jukumu la kila mmoja kutimiza wajibu wake ili
kuiendeleza elimu ya Tanzania.
“Kila
mmoja anapaswa kutimiza wajibu, wazazi, walezi na walimu, waambieni
wanafunzi wasiwe na ‘expectation’ (matarajio) makubwa kwani wanapokuwa
na matarajio hayo, wakienda vyuo vikuu wanakuwa wasumbufu,” alisema.
Wakati
hayo yakiendelea, juzi taarifa ilitolewa jijini Dar es Salaam na Katibu
Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Maimuna
Tarishi, ikisema kwamba, walimu wahitimu wa masomo ya sayansi na
hisabati waliohitimu shahada na astashahada mwaka 2015, wanatakiwa
kuwasilisha nakala za vyeti vya elimu ya sekondari vya kidato cha nne na
sita na taaluma ya ualimu kwa uhakiki.
Pamoja na hayo, hivi karibuni Serikali ilitangaza kusitisha ajira zote nchini ili kukabiliana na wimbi la watumishi hewa.
Sambamba
na uamuzi huo, nyongeza za mishahara kwa watumishi wa Serikali nazo
zilisimamishwa ili kukabiliana na watumishi hao hewa ambao walikuwa
wakiingizia hasara Serikali.
0 comments:
Post a Comment