WIZARA ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imesema
inakusudia kuwasilisha muswada wa sheria bungeni mwakani,
itakayowalazimisha wahitimu wa udaktari kupangiwa kwenye kituo chochote
cha afya na Serikali, ambako watafanya kazi katika kipindi kisichopungua
miaka miwili.
Kwa mujibu wa Naibu Waziri wa wizara hiyo, Dk Hamis Kigwangalla huenda
muswada huo, ukawasilishwa rasmi katika Bunge la Februari mwakani.
Dk Kigwangalla aliyasema hayo Dar es Salaam jana wakati alipozungumza na
waandishi wa habari kuhusu mafanikio ya sekta ya afya katika kipindi
cha mwaka mmoja cha uongozi wa serikali ya awamu ya tano na mikakati ya
kuboresha zaidi sekta hiyo katika miaka ijayo.
Alisema endapo sheria hiyo mpya itapitishwa na bunge hilo, inakusudia kubadili muundo mzima wa watumishi wa sekta ya afya.
“Sheria hii, itaweka kipindi cha lazima cha national service (utumishi
wa umma) na kila daktari anayehitimu kwa sababu amesomeshwa na kodi za
watanzania, atalazimika kupangiwa kwenye kituo chochote cha serikali
ambako atafanya kazi kwa kipindi kisichopungua miaka miwili kwa lazima”.
Naibu waziri huyo, alisema katika mipango na matarajio ya wizara hiyo
kwa mwaka ujao wa 2017, pia wanatarajia kutunga sheria ya kuhakikisha
kila mtanzania anakuwa na bima ya afya ya lazima.
Alisema katika kutekeleza azma hiyo kwa kipindi cha mwaka mmoja,
serikali imefanikiwa kuwakatia bima wazee wote waliopo nchini
wanaokadiriwa kufikia takribani milioni mbili na nusu.
“Bado utaratibu huu wa kuwakatia bima unaendelea katika halmashauri
zingine, lakini tunakoelekea tunaweka sheria ili jambo hili lisiwe tu ni
agizo la serikali bali litambulike na kutekelezwa kisheria,”
alisisitiza Dk Kigwangalla.
Alisema katika sheria hiyo mpya kutakuwa na kifungu cha sheria
kitakachobainisha makundi yote yanayotakiwa kukatiwa bima kwa usimamizi
wa halmashauri zao.
Aidha Dk Kigwangalla alisema pia wizara hiyo ina mpango wa kuhakikisha
inarasimisha suala la matibabu bure kwa makundi maalumu kwa kulitambua
kisheria, ili liweze kutekelezwa na kuwafikia walengwa.
Alisema kwa mujibu wa sera ya afya ya taifa, wazee wote wenye miaka
zaidi ya 60, watoto wenye umri chini ya miaka mitano pamoja na watu
wenye magonjwa sugu kama vile saratani, shinikizo la damu, sukari na
pumu wanapaswa kupata huduma bure.
“Jambo hili lipo na linatambulika kisera, lakini leo hii bado makundi
haya yanaishia kuwaona madaktari bure lakini wanalipia dawa na wakati
mwingine huduma, tutakapoingia na kutunga sheria hii mpya mwakani, hili
litakuwa jambo la kisheria, na tutasimamia utekelezaji wa sheria hiyo,”
alisisitiza.
Akizungumzia mipango ya wizara hiyo chini ya usimamizi wa serikali ya
awamu ya tano, naibu waziri huyo alisema, wizara hiyo imejipanga
kuboresha zaidi huduma za afya, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha huduma za
afya zinafika hadi vijijini.
Alisema katika kipindi cha awamu ya kwanza ya serikali ya awamu ya tano
wizara ya afya, imejipanga kuhakikisha inaongeza vituo vya afya kutoka
489 vilivyopo hadi kufikia vituo vya 1,000 ambavyo vyote au kwa asilimia
kubwa vitakuwa pia vinatoa huduma muhimu za upasuaji kwa akinamama na
upasuaji wa dharura.
“Kwa mwaka unaokuja matarajio yetu ni kuhakikisha tunaongeza idadi ya
vituo vya afya vinavyotoa huduma za upasuaji kwa wajawazito, lakini pia
ni lazima kuwe na huduma za uchunguzi wa magonjwa kupitia maabara na
huduma za upasuaji,” alifafanua.
Alisema kupitia mpango huo, serikali itajenga timu za upasuaji katika
kila kata zitakazokuwa na wataalamu wa kila fani inayotumika katika
upasuaji, kuanzia fani ya usingizi, uuguzi katika vyumba vya upasuaji na
madaktari wa upasuaji.
“Kwa sasa kuna vituo vya afya 489 na vilivyokuwa vinatoa huduma ya
upasuaji ni vituo 113 sasa tunataka vituo vyote vitoe huduma hiyo kwa
akinamama na upsuaji wa dharura,” alisisitiza.
Alisema tayari katika mwaka ujao, wizara hiyo imeilekeza mikoa na wilaya
zote kutenga angalau kituo kimoja na kukiingiza kwenye bajeti
itakayokuja mwakani, ili kuongeza idadi ya vituo vya afya vifikie hadi
700. Pamoja na hayo naibu huyo waziri alibainisha kuwa katika mwaka wa
kwanza wa utekelezaji wa serikali ya awamu ya tano katika sekta ya afya,
kumekuwa na mafanikio makubwa katika sekta hiyo, ikiwemo kuboreshwa kwa
huduma za afya na upatikanaji wa vipimo na tiba.
“Katika awamu hii, viongozi wakuu wamekuwa wakifuatilia kwa karibu
maendeleo ya sekta ya afya, hata Rais John Magufuli mwenyewe alifanya
ziara kadhaa katika hospitali kubwa ikiwemo Hospitali ya Taifa ya
Muhimbili (MNH) hali iliyochangia kuimarika kwa kasi kwa sekta hiyo ya
afya,” alisema.
Oktoba mwaka huu, Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi,
Stella Manyanya alisema serikali iko katika mkakati wa kuwabana
wanafunzi wanaopewa mikopo katika fani za kipaumbele, wanapohitimu
masomo yao, kutumikia katika utumishi wa umma nchini kwa muda fulani ili
kuhakikisha dhamira ya serikali ya kuwapa kipaumbele inatimia.
Fani hizo ni sayansi za tiba na afya, ualimu wa sayansi na hisabati,
uhandisi wa viwanda, kilimo, mifugo, mafuta, gesi asilia, sayansi
asilia, mabadiliko ya tabianchi, sayansi za ardhi, usanifu majengo na
miundombinu.
Hatua hiyo inatokana na serikali kubaini kuwapo wanafunzi wanaosomea
fani hizo ili kupata mikopo, lakini baada ya kumaliza hukimbilia kufanya
kazi nyingine au nje ya nchi, hivyo upungufu wa wataalamu
waliowakusudia kubaki kama ilivyo.
0 comments:
Post a Comment