MATUMIZI ya njia za asili za uzazi wa mpango ni makubwa zaidi katika mkoa wa Dar es Salaam ikilinganishwa na mikoa mingine.
Matokeo muhimu ya Utafiti wa Afya ya Uzazi na Mtoto na Viashiria vya
Malaria Tanzania wa mwaka 2015/2016(TDHS-MIS), yameonesha kwamba mkoa
huo unaongoza kwa asilimia 18.3 katika matumizi hayo ya asili ya uzazi
ikifuatiwa na Mjini Magharibi, kwa asilimia 15.5 na Iringa asilimia
14.5.
Aidha mikoa yenye matumizi madogo ya njia za asili za uzazi wa mpango
chini ya asilimia mbili ni pamoja na Tabora yenye asilimia 1.4, Mtwara
na Mwanza zote zikiwa na asilimia 1.8 na Geita asilimia 1.9.
Utafiti huo umefanywa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) na Ofisi ya
Mtakwimu Mkuu wa Serikali Zanzibar kwa kushirikiana na Wizara ya Afya,
Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Tanzania Bara na Wizara
ya Afya kwa Zanzibar.
Akiwasilisha matokeo hayo, Meneja wa Takwimu za Jamii kutoka Ofisi ya
Taifa ya Takwimu, Sylvia Meku, alisema kuwa njia za asili zinazoongoza
katika mkoa huo ni njia ya kuhesabu siku (kalenda) ambayo ni asilimia
12.4 ikifuatiwa na njia ya kukatisha mshindo au kumwaga nje ambayo ni
asilimia 5.9.
Hata hivyo, alisema kwa ujumla matumizi ya njia za kisasa za uzazi wa
mpango ni ya juu katika maeneo ya mijini kwa asilimia 35 kuliko maeneo
ya vijijini ambayo ni asilimia 31 ikiwa ni tofauti ya asilimia nne. Meku
alisema matumizi ya njia za kisasa yapo juu kabisa mkoani Lindi kwa
asilimia 52 na yapo chini kabisa katika mkoa wa Kusini Pemba wenye
asilimia saba.
Alisema matumizi ya njia za kisasa za uzazi wa mpango kwa wanawake
walioolewa yanaongezeka sambamba na kuongezeka kwa utajiri wakati
asilimia 35 ya wanawake walioolewa katika kaya tajiri sana hutumia njia
za kisasa kwa asilimia 20 tu.
Alisema matumizi ya njia za kisasa za uzazi wa mpango yameongezeka zaidi
ya mara nne tangu utafiti wa kwanza wa TDHS, kutoka asilimia saba mwaka
1991-1992 hadi asilimia 32 mwaka 2015-2016.
“Ukuaji huu wa matumizi ya njia za uzazi wa mpango ulitokea kwa kiasi
kikubwa katika kipindi cha miaka kumi iliyopita ambapo matumizi ya njia
za uzazi wa mpango miongoni mwa wanawake walioolewa yalikuwa ni asilimia
20 katika utafiti wa mwaka 2004-2005 TDHS,” alisema.
Asilimia uzazi wa mpango Alisema matumizi ya sasa ya uzazi wa Mpango
yanaonesha kwamba takribani wanawake wanne kati ya 10 ambao ni sawa na
asilimia 38 walioolewa wenye miaka 15-49 kwa sasa wanatumia njia yoyote
ya uzazi wa mpango huku asilimia 32 wakitumia njia ya kisasa na sita
wanatumia njia za asili.
Meku alisema njia ya kisasa inayotumika zaidi kuliko zote ni sindano kwa
asilimia 13 ikifuatiwa na vipandakizi kwa asilimia saba na vidonge kwa
asilimia sita. Aidha, utafiti huo unaonesha kwamba miongoni mwa wanawake
wenye miaka 15-49 wanaojamiiana na ambao hawako katika ndoa, matumizi
ya uzazi wa mpango ni ya kiwango cha juu.
“Zaidi ya nusu ambayo ni asilimia 54 ya wanawake hao wanatumia njia
yoyote ile ya uzazi wa mpango, asilimia 46 wanatumia njia za kisasa na
asilimia nane wanatumia njia za asili,” alisema.
Alisema mipira ya kinga (kondomu) ya kiume na sindano ni njia
zinazotumiwa zaidi na wanawake katika kundi hilo kwa asilimia 15 kila
moja ikifuatiwa na vipandikizi ambavyo ni asilimia nane na vidonge
asilimia sita.
Kuhusu Dar es Salaam kuongoza kwa mpango wa uzazi wa asili na sababu,
Meku alisema utafiti mwingine hasa kwa mikoa inayoonesha kuwa na
asilimia kubwa ya matumizi ya njia za asili za uzazi wa mpango
unahitajika ili kubaini ni kwanini wanawake wengi wanapendelea njia hiyo
kuliko njia za kisasa.
Watu wanasemaje?
Hata hivyo, gazeti hili lilifanya mahojiano na baadhi ya wanawake na
wanaume waliopo kwenye ndoa na kubainisha kwamba wanatumia njia tofauti
katika kuhakikisha wanajikinga kupata mimba zisizotarajiwa.
Akizungumzia hilo, Sophia Nelson alisema kuwa anatumia njia ya asili ya
kalenda baada ya kubaini kuwa njia za kisasa zina madhara kwake.
“Mimi niliwahi kutumia vidonge nikawa napata shida ya mzunguko wangu wa
siku unaharibika, hivyo baada ya kuacha nikaona mzunguko wangu umerejea
katika hali ya kawaida,” alisema.
Kwa upande wake, Hawa Salim alisema yeye hutumia njia ya uzazi wa mpango
wa kisasa na ameweka vipandikizi kwa miaka sita na hajaona madhara
yoyote badala yake anaifurahia ndoa yake.
Naye David John alisema kuwa wamekuwa wakitumia njia ya uzazi wa mpango
wa asili na mke wake kwa kufuata kalenda na wakati mwingine
inapolazimika hufanya mshindo nje.
Gazeti hili pia lilimtafuta mtaalamu wa afya ya uzazi ambaye hakutaka
jina lake litajwe wala kituo chake cha kazi na kubainisha kwamba njia za
uzazi wa mpango za kisasa ni nzuri na salama kama mtu atafuata ushauri
wa wataalamu, lakini huwa na madhara kwa ambao hawajafuata ushauri.
“Wapo watu wanaolalamika kwamba njia za uzazi wa mpango za kisasa zina
madhara, hii si kweli... nawashauri mtu unapotaka kuzitumia ufike kwenye
vituo vyetu na uonane na mtaalamu kwa ajili ya vipimo na ushauri ndipo
uanze kutumia njia hizi lakini mtu anapoamka na kuanza kutumia bila
uchunguzi anaweza kuona kwamba njia hizi ni mbaya,” alisema.
Dar wana kila sababu
Gazeti hili lilibaini pia kuwa kutokana na maendeleo ya teknolojia,
elimu nyingi ya matumizi ya njia za asili imeeleweka kwa wakazi wa Dar
es Salaam na pia uelewa wao kutokana na elimu na nidhamu katika tendo la
ndoa, vinawasaidia.
Aidha, pamoja na elimu hiyo inayotolewa, pia imebainika kuwa baadhi
taasisi zikiwemo za dini, imani zao haziruhusu waumini wao kutumia njia
za uzazi wa mpango wa kisasa na hivyo kuwaelimisha namna bora ya kutumia
njia za uzazi za asili ikiwemo kufuata kalenda.
Miongoni mwa dini Waislamu na wakristo. Kwa wakatoliki, inaaminika kuwa
matumizi ya njia za uzazi wa kisasa zinazowataka watu waweke vitanzi,
ameze vidonge baada ya kujamiiana na kuweka vijiti, ni sawa na kuua
hivyo wamekuwa na madarasa Msimbazi Center na maeneo mengine ya majimbo
yake kote nchini kuelimisha waumini wao namna bora ya kutumia njia za
uzazi wa mpango wa asili.
Imani hiyo inaeleza kuwa, mbegu ya mwanaume inapokutana na yai la
mwanamke tayari uzima unatungwa na kiumbe ambacho ni binadamu kinakuwa
kiumbe hai tangu dakika hiyo.
Baadhi wa wanandoa watatu waliozungumza na gazeti hili wa kanisa hilo,
walithibitisha kufundishwa hivyo na kutumia njia ya asili kwa muda wa
zaidi ya miaka 15 kwa mafanikio makubwa.
0 comments:
Post a Comment