Watu
wawili wamefariki dunia na wengine 26 kujeruhiwa kwenye ajali
iliyohusisha basi la kampuni ya National Express T.662 DEF, baada ya
kuacha barabara na kupinduka zaidi ya mara tatu katika eneo la kijiji
cha Tumuli, wilaya ya Mkalama mkoani Singida.
Waliofariki ni dereva wa basi hilo Athumani Idd (47) mkazi wa Mabibo jijini Dares Salaam na mwalimu wa shule ya msingi Malunga aliyefahamika kwa jina moja la Janet (anakadiriwa kuwa na umri wa miaka 29).
Habari
zilizopatikana jana eneo la tukio, zimedai kuwa katika siku za hivi
karibuni mwalimu Janet alimpeleka mama yake jijini Dar es salaam kwa
ajili ya kupatiwa matibabu.
Imedaiwa
kuwa baada ya kufika Dar es Salaam, aligundua kuwa amesahau kuchukua
kadi ya bima ya afya, na hivyo akalazimika kurudi Iramba.
Jana
asubuhi Janet alichelewa basi la National Express katika kituo cha
Kyengenge na kuamua kukodi bodaboda kulifukuzia basi hilo na kufanikiwa
kulikuta kituo cha Malunga. Baada kupanda basi hilo, dakika chake
baadae, basi hilo lilipata ajali na kulaliwa na basi kichwani.
Watu
hao wamefariki dunia papo hapo na miili yao ipo katika chumba cha
kuhifadhia maiti cha hospitali ya mkoa mjini Singida. Basi hilo lilikuwa
linatokea New Kiomboi, likielekea jijini Dar.
Akizungumza
kwenye eneo la tukio, Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Singida , ACP
Debora Daudi Magiligimba, alisema ajali hiyo imetokea Desemba, 30 saa
12.45 asubuhi katika eneo la kijiji cha Tumuli.
Alisema ajali hiyo pia imesababisha majeruhi 26 ambao wamelazwa katika hosipitali ya mkoa kwa ajili ya kupatiwa matibabu.
Kamanda
Magiligimba alisema uchunguzi wa awali unaonyesha kuwa ajali hiyo kwa
kiwango kikubwa imesababishwa na mwendo kasi na uzembe.
“Eneo
hili ilipotokea ajali hii kuna mteremko na kona kali. Kutokana na
mwendo kasi, dereva alishindwa kulimudu na hivyo kuacha barabara na
kuingia kwenye korogo la mto, na kuruka juu kisha kupinduka mara tatu,”
alisema.
Kwa
upande wake mganga mkuu mkoa wa Singida, Dk. John Mwombeki, alikiri
kupokea miili ya watu wawili waliofariki dunia kwenye ajali ya basi la
National Express, pamoja na majeruhi 26.
“Kati
ya majeruhi hawa, mmoja dada Joyce tumempa rufaa kwenda hospitali ya
taifa Muhimbili kutokana na sehemu yake ya mwili ya chini kutokufanya
kazi. Majeruhi 10 wao tunaendelea kuwafanyia uchunguzi” alisema Dk. Mwombeki.
Mmoja
wa majeruhi hao mfanyakazi wa shirika la TBC jijini Dar es Salaam,
Victor Elia, alisema pamoja na kupoteza kila kitu, anamshukuru Mungu kwa
kupona kufa kwenye ajali hiyo mbaya.
“Kilichonisaidia
ni kufunga mkanda … abiria wenzangu wote ambao hawakufunga mikanda ndio
walioumia zaidi wakiwemo waliopoteza maisha. Ajali hii kwa vyovyote
imechangiwa na mwendo kasi,” alisema Victor ambaye ni mtayarishaji na mtangazaji wa TBC.
Kondakta
wa basi hiyo, Nicolaus Apolinari (23) mkazi wa jijini Dar es Salaam,
alisema ajali hiyo imechangiwa na utelezi uliosababishwa na mvua kubwa
iliyonyesha katika eneo hilo.
0 comments:
Post a Comment