MAHAKAMA Kuu Kanda ya Dodoma imetengua
uamuzi wa Baraza la Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom) ya kumfukuza mwanachuo
Phillip Mwakibinga na kuamuru arudishwe ili kumalizia masomo yake.
Uamuzi huo ulitolewa jana na Naibu Msajili wa Mahakama Kuu, John Chaba
kwa niaba ya Jaji Awadhi Mohamed aliyekuwa akisikiliza shauri hilo.
Mwakibinga alikuwa akisoma Shahada ya Kiswahili mwaka wa tatu wakati
akisimamishwa na alikuwa Waziri Mkuu wa Kitivo cha Sayansi ya Jamii.
Katika uamuzi huo, mahakama ilisema mlalamikaji hakupewa nafasi ya
kusikilizwa na hivyo kukiuka haki ya asili ya mlalamikaji. Pia
mlalamikaji hakupewa haki ya kusikilizwa na hakuandikiwa mashtaka rasmi.
“Baraza liliegemea upande moja bila kumhoji wala nafasi ya kusikilizwa na kujitetea,” alisema.
Mwakibinga alifukuzwa Udom Januari 14, mwaka jana, kwa madai ya kuongoza
mgomo ambapo siku hiyo baraza la chuo lilikaa na kumfukuza bila kupewa
nafasi ya kusikilizwa.
Alifungua kesi Mahakama Kuu Kanda ya Dodoma kutaka mahakama kutengua
uamuzi huo. Kwa mujibu wa wakili wa Mwakibinga, Elias Machibya alisema
awali waliomba ruhusa ya kufungua kesi na wakapewa Februari 5, mwaka
jana wakiomba kutengua maombi ya baraza la Chuo Kikuu cha Dodoma.
“Tulipata kibali cha kufungua kuomba kutengua maamuzi ya Chuo Kikuu cha Dodoma kwa kumfukuza,” alisema.
Alizitaja sababu kuu tatu za kupinga mwanafunzi huyo kufukuzwa chuo kuwa
ni pamoja na kutopewa nafasi ya kusikilizwa, hakuna hatua za nidhamu
zilizochukuliwa, walimfukuza wakidai aliwahi kuhusika na migomo ya
nyuma.
Alidai barua ya kumfukuza ilisainiwa na Profesa Shaban Mlacha.
Januari 14, mwaka jana uongozi wa Udom ulimfukuza Mwakibinga ambaye
wakati huo alikuwa Waziri Mkuu wa Serikali ya wanafunzi, Kitivo cha
Sayansi ya Elimu ya Jamii, na kupewa barua ya kusimamishwa kutokana na
kosa la kuhamasisha mgomo.
Uongozi huo ulisema Mwakibinga amefukuzwa kabisa kwa kuwa alishawahi
kujihusisha na mgomo wa mwaka 2010/2011 akafukuzwa lakini akakata rufaa
na kuomba msamaha kwenye Kamati nidhamu.
“Baada ya kukata rufaa Kamati ikamuonea huruma ikamrudisha kabla ya
kurudi alitakiwa aje na kiapo kutoka kwa mwanasheria kwamba
hatajihusisha na mgomo tena lakini akarudia tena kosa hilo."
Mwakibinga amesema amefurahia uamuzi huo kwani ndio sababu ya msingi ya
kufungua kesi na mahakama imetenda haki. Alisema anasubiri barua ya
hukumu ambayo itatoka kesho ndipo taratibu zake za kurudi chuo
zitakapoanza.
0 comments:
Post a Comment