WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amewahimiza wakazi wa vijiji saba wilayani Ruangwa
waharakishe kufyatua matofali ili waanze ujenzi wa zahanati na yeye
atawachangia mabati.
Ametoa ahadi hizo jana
(Jumatano, Desemba 28, 2016) wakati akizungumza na wananchi wa vijiji
vya Namilema, Mbuyuni, Nandandara, Namkonjera, Muhuru, Chikundi na
Chibula na viongozi wa wilaya ya Ruangwa, mkoa wa Lindi ambako anapita
kuwasalimia wananchi wa jimbo lake na kuhimiza kazi za maendeleo.
Waziri
Mkuu yuko Ruangwa kwa siku nne kwa mapumziko ya mwisho wa mwaka.Alisema
sera ya Serikali ni kuwa na zahanati kwa kila kijiji na kituo cha afya
kwa kila kata na kwamba umefika wakati wa kuanza kutekeleza kaulimbiu ya
jimbo hilo inayosema “Ruangwa kwa maendeleo, inawezekana.”
Katika
kuhimiza ujenzi wa zahanati hizo, alichangia mabati kati ya 50 na 150
kwa kila kijiji na akawahimiza wahakikishe wanakamilisha mapema ujenzi
wa maboma ili aweze kutimiza ahadi yake ya mabati.
Alisema
katika awamu iliyopita, alikazania sana suala la elimu kwa kusimamia
ujenzi wa nyumba za walimu na madarasa kwenye shule ambazo hazikuwa na
madarasa ya kutosha. Pia alisimamia ukarabati wa majengo chakavu katika
baadhi ya shule.
“Kuanzia
awamu hii na miaka minne iliyobakia, mkakati wangu ni kusimamia
upatikanaji wa maji safi na suala la kuboresha sekta ya afya katika
jimbo zima nikishirikiana na uongozi wa Halmashauri yetu,” alisema.
Pia
alimwagiza Mganga Mkuu wa Wilaya hiyo, Dk. Japhet Simeo ahakikishe
anawasiliana na viongozi wa vijiji hivyo ili wapatiwe michoro ya ramani
zilizoidhinishwa na Wizara ya Afya.
Wakati
huohuo, Mkurugenzi wa kampuni ya Umemejua ya Baraka Solar Specialist,
Bw. Ansi Mmasi alisema atajitolea kuweka mfumo wa umemejua wa watts 300
pamoja na nyaya zake kwenye zahanati inayotaka kujengwa kwenye kijiji
cha Namilema.
Alisema
anaishukuru kwa kuwapa kazi makandarasi wazawa na akawataka wakandarasi
wenzake watumie vifaa bora na imara pindi wanapopewa kazi ya kutoa
huduma na taasisi mbalimbali ikiwemo halmashauri na idara za Serikali.
“Tujitahidi
kufanya kazi hizi kwa weledi na tutumie vifaa bora na imara ili watu
wanaotarajia huduma zetu waweze kuridhika na kuendelea kuwa na umani na
wakandarasi wazawa kwamba tunaweza kufanya kazi nzuri na zenye ubora
unaotakiwa,” alisema.
Naye
Mkurugenzi wa kampuni ya ujenzi ya Wanyumbani Construction, Bw. Fakihi
J. Bakili alisema atachangia mifuko 50 ya saruji kwa ajili ya ujenzi wa
zahanati hiyo ya kijiji cha Namilema. Pia alichangia mifuko 100 kwenye
zahanati ya kijiji cha Manokwe na mifuko mingine 50 kwa ajili ya ujenzi
wa zahanati ya kijiji cha Chikundi.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
0 comments:
Post a Comment