WALIMU wa Sayansi watakaoajiriwa na serikali, watalazimika kutuma vyeti vyao kabla ya kupangiwa kituo cha kazi.
Hiyo ni sehemu ya mabadiliko katika utaratibu wa ajira wenye lengo la
kuimarisha ufundishaji kwa waliohitimu Ualimu wa Sayansi na Hisabati.
Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi,
Profesa Joyce Ndalichako, wakati akifungua Mkutano Mkuu wa Mwaka wa
Wakuu wa Shule za Sekondari Tanzania (Tahossa).
Pamoja na kuzungumzia mabadiliko hayo katika mfumo wa ajira, alisema ni
nia ya serikali kuimarisha elimu ya sekondari, ikiwa ni pamoja na
kuimarisha ufundishaji wa masomo hayo ya Sayansi.
Aidha, Profesa Ndalichako aliwataka Walimu wakuu nchini, kusimamia ubora wa elimu kutokana na wao kuwa karibu na wanafunzi.
Akifafanua, alisema walimu wakuu wanawajibu wa kuwa wasimamizi na
wakaguzi wa kwanza wa wanafunzi ili kuiboresha elimu ya Tanzania,
wakizingatia kuwa elimu ya Sekondari ni kiungo muhimu katika kuendeleza
elimu nchini.
Vile vile, aliwataka wakuu hao kupeleka takwimu sahihi za wanafunzi
waliopo katika shule zao ili kuisaidia serikali katika kupanga bajeti
ili iweze kutoa fedha sahihi.
“Hapa kuna kimbembe wakati mwingine huwa najifanyisha nimepoteza takwimu
ya shule fulani nikitumiwa inakuwa tofauti na ile ya mwanzo, niwaombe
walimu mkalisimamie hili ili iwe rahisi kwetu kupanga bajeti yenye
tija,’’ alisema.
Prof. Ndalichako alisema kutokana na maabara nyingi kukamilika, serikali
itatoa vifaa vya maabara kuanzia Januari mwaka mwakani. Katika mkutano
huo, Waziri pia aliwaomba Makatibu Tawala na Wakurugenzi, kuwalinda
walimu wanaofuata kanuni, taratibu na sheria katika utendaji kazi wao na
kudhibiti wanasiasa kuingilia masuala ya elimu.
Pia aliwataka walimu wakuu kuwa na mahusiano mazuri na jamii inayowazunguka pamoja na kufanya usafi katika shule zao.
Akisoma risala, Rais wa Tahossa, Bonus Nyimbo aliiomba serikali itoe
waraka wa kupiga marufuku matumizi ya simu kwa wanafunzi shuleni, kwani
imekuwa ikichangia kushusha ufaulu wa baadhi ya wanafunzi.
Nyimbo ambaye ni Mwalimu Mkuu wa Shule ya Sekondari Mwenge ya mkoani
Singida, aliiomba serikali iajiri pia walinzi, watumishi na madereva ili
waweze kufanya kazi kwa ufasaha. Alisema changamoto nyingine,
wanayokabiliwa nayo ni baadhi ya wanachama kutoelewa vizuri katiba
pamoja na kutokulipa ada kwa wakati.
“Kwa upande wake Mkurugenzi wa Global Education Link, AbdulMalik Molel
ambaye kampuni yake ilipewa tuzo ya heshima katika kuendeleza elimu
nchini”, alisema ni jukumu la kila mmoja kutimiza wajibu wake ili
kuiendeleza elimu ya Tanzania.
0 comments:
Post a Comment