POLISI
mkoani Morogoro imewafikisha mahakamani watu saba kati ya 12, kujibu
tuhuma za kumjeruhi kwa kumchoma mkuki mdomoni hadi kutokea shingoni,
Augustino Mtitu (35).
Walipandishwa
kizimbani jana katika Mahakama ya Wilaya ya Kilosa huku wengine watano,
wote wakazi wa kitongoji cha Upangwa wilayani Kilosa wakisubiri
kufikishwa mahakamani baada ya uchunguzi kukamilika.
Kamanda
wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Ulrich Matei, alisema jana alipokuwa
anazungumzia msako uliofanywa na polisi na kufanikisha kukamatwa kwa
watuhumiwa hao baada ya kutokea kwa tukio hilo Desemba 25, mwaka huu,
majira ya saa tano asubuhi eneo la kitongoji cha Upangwa, Kijiji cha
Dodoma Isanga, Kata na Tarafa ya Masanze wilayani Kilosa.
Kamanda
Matei alisema katika msako huo, watu 12 walikamatwa na saba kati yao
tayari wamefikishwa mahakamani. Wengine watano watafikisha mahakamani
baada ya kukamilika kwa uchunguzi.
Hata
hivyo, Kamanda huyo aliwataja majeruhi wa tukio hilo mbali na Mtitu
ambaye bado anaendelea na matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa
Morogoro, kuwa ni George Andrew (68) aliyejeruhiwa kichwani.
Wengine
ni Yohana Wisa (26) aliyejeruhiwa mkono wa kulia, Mathayo Elia (34)
aliyejeruhiwa kichwani na bega la kushoto, Josephat Mtitu (55)
aliyejeruhiwa begani na shavuni na mwingine ni Paulo Thomas (56)
aliyejeruhiwa mbavu na mkono wa kushoto.
Wote
ni wakazi wa kijiji cha Dodoma Isanga na wanaendelea vizuri. Hivi
karibuni, baadhi ya wafugaji wa jamii ya kimasai waliwashambulia kwa
silaha za jadi na kuwajeruhi watu sita akiwemo Mtitu mara baada ya
kukamata mifugo ya mtu mmoja aitwaye Ngoyoni Kimang’ati, iliyokuwa
ikiharibu mahindi shambani.
0 comments:
Post a Comment