Sunday, 18 December 2016

CCM washinda Meya, Naibu Meya Kigamboni

...

UCHAGUZI wa kumpata Meya wa Manispaa ya Kigamboni jijini Dar es Salaam, umefanyika na hatimaye Diwani wa Kata ya Pemba Mnazi kutoka Chama cha Mapinduzi (CCM), Maabadi Hoja amechaguliwa kuwa Meya wa kwanza.
Uchaguzi huo ulifanyika jana kwenye ukumbi wa Chuo Kikuu cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere jijini Dar es Salaam.
Katibu Tawala wa Wilaya ya Kigamboni, Rahel Mhando, ambaye alikuwa msimamizi wa uchaguzi, alisema mgombea huyo wa CCM ndiye aliyeshinda.
Washiriki wengine walitoka vyama vya CCM, Chama cha Wananchi (CUF) na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema). Mhando alisema Hoja alipata kura tisa dhidi ya Celestine Maufi (CUF) aliyepata kura tano na kura moja iliharibika.
Pia, Mhando alisema katika uchaguzi huo, Amini Sambo ambaye ni Diwani wa Kata ya Kibada, pia kutoka CCM, alishinda nafasi ya Naibu Meya, akipata kura 10 dhidi ya Ernest Mafimbo wa CUF, aliyepata kura tano. “Tunashukuru uchaguzi umefanyika vizuri Kigamboni, sasa tumepata Meya na Naibu Meya,” alisema Mhando.
Uchaguzi wa Meya na Naibu wake kwa upande wa Kigamboni, umefanywa baada ya Wilaya ya Temeke kugawanywa na kuwa wilaya mbili za Temeke na Kigamboni.
Mhando alieleza kuwa uchaguzi huo ambao ni wa mara ya kwanza kwa halmashauri hiyo, ulifanyika kwa amani bila kuwapo na malalamiko.
Mbunge wa Kigamboni, Dk Faustine Ndungulile, baada ya kumalizika kwa uchaguzi huo, alisema uchaguzi ulifanyika bila tatizo lolote na kwamba baada ya uchaguzi kuisha, kinachofuata ni kazi.
Alisema kwa muda mrefu mambo mengi katika halmashauri hiyo, yalisimama kwa kukosa Baraza la Madiwani. Akizungumza na gazeti hili, meya huyo, Hoja alisema anajipanga kuiweka Halmashauri hiyo mpya kimji. Aliahidi kuanza na kusimamia mipangomiji na miundombinu.
“Manispaa yetu ni mpya na haijapangwa, tunataka kuiweka kimji zaidi na tutaanza na mipangomiji kwani kuna ujenzi holela na pia tutasimamia miundombinu,” alisema Hoja.
Hii si mara ya kwanza kuchaguliwa kushika nafasi hiyo. Alichaguliwa kuwa Meya wa Manispaa ya Temeke mwaka 2010 baada ya kushinda udiwani wa kata hiyo kwa mara ya kwanza.
Baada ya kufanyika uchaguzi mkuu mwaka jana, Hoja alipata tena udiwani katika kata hiyo, lakini aliposhindania nafasi ya meya, hakushinda nafasi hiyo. Lakini, baada ya Temeke kugawanywa kuwa wilaya mbili za Temeke na Kigamboni, Hoja amegombea tena na kushinda.
Kwa upande wake, akihojiwa, Naibu Meya mpya, Sambo, anasema hii ni mara ya kwanza kushika nafasi ya udiwani. Alichaguliwa mwaka jana.
Sambo alisema anaishukuru Serikali kwa kusogeza huduma karibu, kwa kuifanya Kigamboni kujitegemea kama halmashauri.
Alisema yeye na viongozi wenzake watashirikiana na serikali, kuifanya halmashauri hiyo mpya kuwa ya mfano. Halmashauri ya Kigamboni inaundwa na kata tisa za Pembamnazi, Kimbiji, Somangila, Kisarawe, Kibada, Vijibweni, Kigamboni, Mjimwema na Tungi.
Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger