TAARIFA KWA UMMA
Mnamo tarehe
26 na 27 Desemba, 2016 baadhi ya mitandao ya kijamii imeandika taarifa
zenye nia ya kupotosha Umma ambazo Sekretarieti ya Ajira inapenda
kuzitolea ufafanuzi kama ifuatavyo;-
1. Sekretarieti ya Ajira inapenda kutoa ufafanuzi
kufuatia hoja iliyoandikwa katika baadhi ya mitandao ya kijamii ya
tarehe 27 Desemba, 2016 zenye vichwa vya habari vinavyosomeka “Waliofaulu usaili ajira serikalini kufutwa” na “Taarifa kwa waliokuwa wakisubiri kupangiwa vituo vya kazi kabla ya ajira kusitishwa serikalini”
zikidaiwa kutolewa na Taasisi hii katika majibu ya hoja za mwezi
Novemba, 2016 katika utaratibu wake wa kujibu hoja za kila mwezi kama
ifuatavyo;-
Kwa mujibu wa kumbukumbu za Sekretarieti ya Ajira
tangu mwezi Juni, 2016 Serikali ilipositisha Ajira hapakuwa na orodha
ya waombaji kazi waliokuwa wakisubiri matokeo ya usaili, kwa kuwa
usaili wa mwisho ulioendeshwa na Sekretarieti ya Ajira ulifanyika mwezi
Mei, 2016 na waombaji waliofaulu walipangiwa vituo vya kazi kwa idaidi
ya nafasi zilizokuwepo.
Aidha, kwa wale ambao walifaulu na hawakuweza
kupangiwa vituo vya kazi kutokana na kukosekana kwa nafasi zilizokuwepo
walihifadhiwa katika kanzidata (Database) ambayo hudumu kwa muda cha
miezi sita (6) baada ya matokeo ya usaili husika kutolewa.
Baada ya ufafanuzi huo hususani aya ya tatu
Sekretarieti ya Ajira ingependa kufafanua zaidi namna kanzidata ya
waliofaulu usaili inavyotumika ili kuweza kuwa na uelewa wa pamoja kwa
wadau na jamii kwa ujumla ili kuepusha kupokea ama kusikia taarifa
zisizo rasmi zenye nia ya kupotosha Umma zinazojitokeza mara kwa mara
hususani katika baadhi ya mitandao ya kijamii.
Kanzidata ya waliofaulu usaili:
Kwa mujibu wa Kanuni za Uendeshaji wa shughuli za
Sekretarieti ya Ajira za mwaka 2016, Kanuni ya 21. (1) - (5) imefafanua
juu ya kanzidata kama ifuatavyo;-
(1) Baada ya waombaji waliofaulu usaili kuwapangia
vituo vya kazi, orodha itakayobaki itatunzwa na Katibu katika kanzidata
ili pale itakapotokea fursa ya ajira orodha hiyo iweze kutumika.
(2) Orodha ya waombaji walioko kwenye kanzidata
itatumika kujaza nafasi wazi kulingana na mahitaji ya Waajiri. Hata
hivyo, wakati wa upangaji, Katibu atazingatia mpangilio wa matokeo ya
alama za ufaulu wa mwombaji kwa aliyepata alama za juu zaidi ya wengine
kufikiriwa kwanza.
(3) Sekretarieti itatangaza nafasi wazi za ajira na
kufanya usaili endapo orodha iliyotunzwa katika kanzidata itakuwa
imekwisha au haina mtumishi mwenye utaalam au sifa zinazohitajika na
Mwajiri.
(4) Endapo katika orodha iliyotajwa kwenye Ibara ya
21(2) kutakuwa na waombaji waliopata alama zinazolingana, utaratibu
ulioainishwa katika Ibara ya 14(1) utazingatiwa.
(5) Orodha ya kanzidata itadumu kwa kipindi cha miezi sita (6) tangu kuidhinishwa kwa matokeo na Wajumbe wa Sekretarieti.
2. Sekretarieti ya Ajira pia
inapenda kutoa ufafanuzi kwa taarifa nyingine iliyoandikwa katika
mitandao ya kijamii yenye kichwa cha habari kinachosema “Mhe
Rais Magufuli nakuomba Sekretarieti ya Ajira uifute maana haina majukumu
sasa hivi lengo la Sekretarieti ya Ajira ni kutangaza kazi na ........”. kama ifuatavyo;-
Ni vyema wadau wa Sekretarieti ya Ajira na Jamii
kwa ujumla ikafahamu kuwa Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma
ilianzishwa kupitia Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Utumishi wa Umma
Na. 18 ya mwaka 2007 kifungu cha 29 (1). Kwa mujibu wa Sheria ya
Utumishi wa Umma Na. 8 ya mwaka 2002 kama ilivyorekebishwa na Sheria Na.
18 ya mwaka 2007 kifungu cha 29 (6) (a-f) na Sera ya Menejimenti ya
Ajira toleo Na. 2 la mwaka 2008 Sekretarieti ya Ajira ina majukumu
yafuatayo;-
i. Kutafuta wataalam wenye ujuzi maalum na
kuandaa mfumo wa kuhifadhi taarifa (kanzidata) za wataalam hao ili
kurahisisha utaratibu wa kuwaajiri pindi wanapohitajika,
ii. Kuandaa orodha ya wahitimu wa Vyuo Vikuu
na Wataalam Weledi (Professionals) kwa madhumuni ya kurahisisha rejea na
ujazaji wa nafasi wazi za ajira katika Utumishi wa Umma,
iii. Kutangaza nafasi wazi za kazi zinazotokea katika Utumishi wa Umma.
iv. Kuhusisha wataalam maalum (Appropriate experts) kwa ajili ya kufanya usaili kulingana na mahitaji,
v. Kutoa ushauri kwa Waajiri kuhusu masuala mbalimbali yanayohusiana na ajira,
vi. Kufanya kazi nyingine yoyote inayoendana
na majukumu yake kadri itakavyoelekezwa na Waziri mwenye dhamana ya
Utumishi wa Umma.
Kutokana na ufafanuzi huo Sekretarieti ya Ajira
ingependa jamii ifahamu mbali na jukumu la kuendesha mchakato wa Ajira
ina majukumu mengine inayoyatekeza kama yalivyoainishwa hapo juu kwa
mujibu wa Sheria.
Riziki V. Abraham
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano, Sekretarieti ya Ajira.
27 Desemba, 2016.
0 comments:
Post a Comment